Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia viongozi wawili wa mpira wa miguu nchini baada ya kupatikana na makosa ya kimaadili, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyoonwa na Mwandishi Diramakini ambayo imetolewa na Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, Januari 27, 2021.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Lipuli FC,Julius Leo ambaye amefungiwa miaka mitatu na faini ya shilingi milioni tatu, kwa mujibu wa kifungu cha 73 (4) cha mwongozo wa maadili wa TFF, Toleo la 2013.
"Mlalamikiwa (Julius Leo) alitiwa hatiani kwa makosa mawili, kutoa taarifa za uongo kuhusu kiasi ambacho klabu ya Lipuli ilikuwa inaidai TFF ikiwa ni zawadi ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho (Federation Cup), wakati kosa la pili ni kukosa umakini, ni katika kutunza nyaraka za siri za kiofisi, ivyo kusababisha barua rasmi ya TFF kupelekwa kwenye mitandao ya kijamii,"imeeleza taarifa hiyo iliyoonwa na Mwandishi Diramakini.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Afisa Habari wa Klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya kifungu cha 73 (8)(a) cha mwongozo wa maadili wa TFF, toleo la 2013 kwa kutotii uamuzi wa Kamati ya Maadili dhidi yake.