Assalamu Aleikum
Shukurani
Namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi na vyote viliomo ndani yake, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kusherehekea maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Hii ni siku ya kipekee kwangu kwa kuwa haya ni maadhimisho ya kwanza tangu niingie madarakani kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Nilitamani kuwa sherehe hizi ziwe na shamrashamra kama ilivyozoeleweka kutokana na umuhimu wake.
Hata hivyo, tumelazimika kuzifanya kwa namna tofauti kutokana na athari za ugonjwa wa COVID-19 ulioikumba nchi yetu na ulimwengu kwa ujumla .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa mara alipowasili viwanja vya Mnazi Mmoja katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,sherehe zilizofanyika leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwapungia mkono Wananchi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi waliopita katika viwavja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar leo katika Sherehe za maadhimisho ya Kilele cha miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Nawapongeza na kuwashukuru viongozi na wananchi nyote wa Mikoa yote
ya Unguja na Pemba kwa ushirikiano wenu mkubwa katika shughuli mbali
mbali za maadhimisho haya.
Ushiriki wenu viongozi na wananchi ni
kielelezo muhimu cha jinsi tunavyoyaenzi Mapinduzi yetu.
Ni
jambo la faraja kuona kwamba tunaadhimisha sherehe zetu tukiwa katika
umoja na mshikamano baada ya maridhiano ya kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa;
Nakuombeni wananchi nyote bila kujali itikadi ya chama au dini
tuungane kwa pamoja katika kudumisha mshikamano na upendo miongoni
mwetu.
Ndugu Wananchi, Tuna kila sababu ya kuyaenzi Mapinduzi
yetu kwa sababu ndicho chombo kilichotuvusha kutoka katika dhoruba za
kutawaliwa na kubaguliwa katika nchi yetu.
Kwa mnasaba huu, leo ni siku
muhimu sana katika historia ya Zanzibar, ambapo miaka 57 iliyopita,
wakulima na wafanyakazi wanyonge walikataa madhila ya kubaguliwa.
Walifanyaa Mapinduzi kudai haki zao za msingi za kujiendeshea maisha yao,
kama vile huduma za afya, elimu na elimu. Vile vile, walidai haki ya
kuitumia ardhi kwa kilimo chenye tija na kupata makaazi bora, kupata
ajira zenye staha na heshima na kupinga dhulma nyengine kadhaa
walizokuwa wakitendewa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwapungia mkono Wananchi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi waliopita katika viwavja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar leo katika Sherehe za maadhimisho ya Kilele cha miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Wananchi wafanyabishara wadogo wadogo wakiwa na bango lao kwa kumpomngeza Rais,Dkt.Hussein Ali Mwinyi wakati walipopita katika maandamano ya kusherehekea kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnzi Mmoja jijini Zanzibar.
Askari wa kikosi cha Polisi wakipita kwa mwendo wa Route March wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnzi Mmoja Jijini Zanzibar.
Askari wa kikosi cha Polisi wa usalama barabarani wakipita kwa maonesho ya Amsha Amsha ya Mapinduzi mwendo wa Route March wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnzi Mmoja Jijini Zanzibar.
Maonesho ya Amsha Amsha ya Mapinduzi mwendo wa Route March Gari za Vikosi vya Uluinzi wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnzi Mmoja Jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdalla mara alipowasili viwanja vya Mnazi Mmoja katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,sherehe zilizofanyika leo (wengine kutoka kulia) Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe.Amani Abeid Karume na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi (katikati) Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdalla (wa pili kushoto) na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe.Amani Abeid Karume (kulia) mara alipowasili viwanja vya Mnazi Mmoja leo katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe.Amani Abeid Karume na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi (katikati) mara alipowasili viwanja vya Mnazi Mmoja leo katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) pamoja na Viongozi wa Kitaifa wakisimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa wa Taifa wa Zanzibar,Afrika Mashariki na Wimbo wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wimbo Maalum wa “Sisi Sote Tumegomboka” katika katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar .
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ wakisimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa wa Taifa wa Zanzibar,Afrika Mashariki na Wimbo wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wimbo Maalum wa “Sisi Sote Tumegomboka” katika katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitoa hutuba yake fupi kwa Wananchi wa Zanzibar katika Sherehe za kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zilizofanyika leo viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar.
Wananchi mbali mbali waliohudhuria katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitoa hutuba yake fupi katika Sherehe za kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zilizofanyika leo.[Picha na Ikulu] 12/01/2021.
Ikumbukwe kuwa nchi ambazo zinategemea utalii kama tulivyo sisi zimeathirika zaidi. Kwa hivyo, busara na hekima zimetuelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya sherehe hizi tuzielekeze katika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji safi na salama. Ieleweke kuwa hali hii ni ya mpito, tunatarajia katika kipindi kijacho, sherehe hizi zitafanyika katika utaratibu uliozoeleka.
Wananchi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar.
Ndugu Wananchi, Tunapoadhimisha Sherehe za Mapinduzi kwa kutimiza miaka 57, tuna wajibu wa kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi, walioongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Tunawakumbuka na kuwashukuru kwa ushujaa wao wa kuzipigania haki zetu, kuleta usawa na maelewano na kuondosha kila aina ya pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Zanzibar.
Tunamuombea dua Jemedari wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na Viongozi wenzake walioongoza Mapinduzi hayo kwa ajili ya kuwakomboa wanyonge wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar na kuwarejeshea utu na heshima yao.
Kwa wale viongozi waliotangulia mbele ya haki, tunamuomba Mwenyezi Mungu awarehemu na awaweke mahali pema peponi, Amin. Kwa wale walio hai, Mwenyezi Mungu awape umri mrefu na afya njema.
Siku zote tutawakumbuka, tutawaenzi, tutawashukuru na tutawaombea dua kutokana na jitihada zao na mapenzi kwa nchi yao, yaliyotupelekea kuwa huru.
Ndugu Wananchi, Leo tunafikia kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 57 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, tukiwa na furaha kubwa.
Sherehe hizi zinatukumbusha umuhimu wa kuendelea kuyalinda, kuyatetea na kuyadumisha Mapinduzi yetu, kama tulivyofanya katika miaka iliyopita kwa mafanikio makubwa.
Ndugu Wananchi, Katika kipindi hiki cha miaka 57 ya Mapinduzi, tunasherehekea kuwepo kwa hali ya amani, umoja na maendeleo makubwa yaliyopatikana.
Tuna wajibu mkubwa wa kuuenzi na kuuendeleza umoja na mshikamano wetu, ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu.
Nafarajika sana kuona wananchi wa Zanzibar wameungana na Serikali yao katika kipindi cha miaka 57, kwa kuyatekeleza malengo ya Mapinduzi yetu na kupatikana maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kwa hakika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeweza kuyatekeleza na kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi kwa ufanisi mkubwa.
Katika miaka 57 iliyopita, tumeweza kufanya mambo mengi kwa mafanikio.
Ni haki ya kila mmoja wetu kujivunia mafanikio hayo na kuyaendeleza kwa manufaa yetu na vizazi vya baadae.
Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu wote, kuwa sisi Serikalini tutaendelea kufanya kila tuwezalo kwa ajili kujenga, kulinda na kudumisha umoja na mshikamano wetu ambao ndio msingi mkuu wa kuwepo kwa amani na utulivu nchini.
Tutaendelea kukemea kwa nguvu zetu na uwezo wetu wote vitendo vinavyosababisha kuharibu umoja na mshikamano wetu.
Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au kikundi cha watu watakaojihusisha na vitendo vya kuvuruga amani ya nchi yetu.
Naomba Wazanzibari wenzangu mtuelewe hivyo. Napenda kusisitiza na kuwasihi kuwa tuendelee kuaminiana, kuheshimiana na kuvumiliana na kusahau tofauti zetu.
Ndugu Wananchi, Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea kuchukua juhudi kubwa za kufufua uchumi wetu.
Hatua kwa hatua, hivi sasa, tunaendelea kushuhudia ongezeko la makusanyo. Kwa mfano, tayari makusanyo yemeanza kuongezeka kutoka bilioni 22 mwezi Oktoba hadi kufikia bilioni 36.9 mwezi wa Disemba, 2020 yaliyokusanywa na ZRB. Ni matuamini yetu kwamba hali hii itazidi kuimarika katika miezi inayofuata.
Ndugu Wananchi, Sekta ya utalii imeendelea kuimarika, ambapo tuliweka lengo la kupokea watalii 250,855 ifikapo Disemba 2020, baada kuzingatia mwenendo wa mardhi ya COVID 19 ndani na nje ya nchi yetu.
Hadi Novemba 2020 jumla ya watalii 212,050 wametembelea Zanzibar sawa na asilimia 85 ya makadirio.
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta hii bado tunayo fursa ya kuindeleza.
Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nane itasimamia kwa karibu uratibu, utangazaji na uendelezaji wa sekta hii ili itoe mchango mkubwa zaidi kwa Wazanzibari na uchumi kwa ujumla.
Hivi sasa, tunalitafutia ufumbuzi tatizo lililojitokeza la kuchelewa kupatiwa wageni huduma za msingi wanapofika katika Uwanja wa ndege na kuwasababishia usumbufu.
Kadhalika, suala la kuwepo kwa huduma za zimamoto za uhakika kiwanjani hapo litashughulikiwa ipasavyo na kero nyingine kadhaa zinazowakuta watalii wanapoingia nchii tutazipatia ufumbuzi.
Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wageni wetu wanafurahia makaazi yao Zanzibar.
Jambo ambalo litachochea kupata watalii wengi wanaokaa Kwa muda mrefu na kupendelea kuja tena Zanzibar wanapohitaji kufanya hivyo.
Vilevile, tutahakikisha sekta ya utalii inakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya uchumi wa buluu (blue economy).
Ndugu Wananchi, Kwa upande wa biashara, jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 62,221,261,713, zilisafirishwa kwenda nje ya nchi, Januari hadi Novemba mwaka 2020, ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 33,277,617,078, mwaka 2019 kwa kipindi kama hicho.
Ndugu Wananchi, Mchango wa sekta ya viwanda katika jumla ya Pato la Taifa umeongezeka kufikia asilimia 18.9 mwaka 2019.
Serikali itaendelea na juhudi za kushajihisha wawekezaji wa ndani na nje, kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda.
Kwa lengo la kuvutia wawekezaji, |Serikali imeanza kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara kuelekea eneo huru la uwekezaji la Micheweni, Pemba.
Kadhalika, Serikali kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa au kuingizwa Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
Ndugu Wananchi, Katika kipindi cha miaka 57 ya Mapinduzi tunajivunia kuimarika kwa huduma za elimu ambapo kabla ya Mapinduzi ya 1964, zilikuwa chache, zikitolewa kwa ubaguzi na zilikuwa za kulipia.
Hivi leo, huduma za elimu zimeimarika kwa kiwango kikubwa sana. Skuli za msingi na za sekondari zimeongezeka kwa kiwango kikubwa sana na pia tumeanzisha vyuo vikuu hapa hapa Zanzibar.
Katika kipindi hiki cha miaka 57 ya Mapinduzi, Zanzibar imeweza kuwa na wataalamu wengi wa fani mbali mbali ambao wanachangia katika nguvu kazi ya kusogeza mbele mipango yetu ya maendeleo. Haya ni mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano ambayo tunajivunia..
Katika jitihada ya kuongeza madarasa ya kusomea, Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza ujenzi wa skuli za ghorofa katika ngazi zote za elimu pamoja na kujenga vituo vya mafunzo ya amali kwa mujibu wa mahitaji ya wananchi wetu.
Aidha, Serikali inaendelea kulishughulikia suala la ununuzi wa vifaa vya elimu ikiwemo madawati kwa ajili ya skuli zote za Unguja na Pemba.
Tunatarajia tatizo la upungufu wa madawati katika skuli zetu , litamalizika mwaka katika kipindi kifupi kijacho.
Ndugu Wananchi, Juhudi kubwa na za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuziimarisha huduma za afya.
Tayari nimeshafanya mazungumzo na wataalamu, watabibu na wahudumu wa sekta ya afya kufahamu changamoto zao ili tuweze kuzipatia ufumbuzi kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
Kadhalika, kutokana na upungufu wa madaktari bingwa, madaktari na wataalamu wengine wa afya, Serikali itafanya jitihada maalum za kuwasomesha madaktari na wataalamu mbali mbali wa sekta ya afya katika kiwango cha Shahada na Stashahada katika vyuo tofauti vya ndani na nje ya nchi.
Aidha, tutaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya ili kuondoa tatizo linalolalamikiwa na wananchi wanaofuata huduma hizo.
Vilevile, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya hapa hapa Zanzibar, Serikali inatarajia kujenga hospitali kubwa ya rufaa na ya kufundishia katika eneo la Binguni, ambayo itakidhi mahitaji ya wataalamu, vifaa na uwezo wa kimiundombinu. Mchakato wa ujenzi wa hospitali hiyo, umeshaanza.
Ndugu Wananchi, Pamoja na jitihada za Serikali inazochukua katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kama vile umeme na maji safi na salama, bado mahitaji ya huduma hizo kwa wananchi ni makubwa.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha sehemu zote ambazo hivi sasa zinakosa huduma za umeme na maji zinapata huduma hiyo kwa mujibu wa mahitaji ya wananchi.
Aidha, Serikali itafanya mapitio ya miradi yote ya maji na umeme, Unguja na Pemba, ili kuona malengo ya kuanzishwa kwake yanapatikana na tija ya miradi hiyo inawafikia wananchi ipasavyo.
Ndugu Wananchi, Pamoja na changamoto zilizopo, wananchi wanaendelea kupata fursa nzuri ya kuitumia ardhi kwa ajili ya kuendeleza maisha yao kwa kilimo, ujenzi wa nyumba bora na kadhalika. Tayari nimeshawaelekeza watendaji wangu ikiwemo Wizara ya Ardhi kushirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kumaliza migogoro yote ya ardhi ifikipo mwisho wa mwaka huu wa 2021.
Sitopenda kusikia kuwa kuna mwananchi analalamikia kudhulumiwa ardhi yake. Lazima haki za wananchi wetu ziheshimiwe na zizingatiwe ipasavyo.
Ndugu Wananchi, Serikali itaendelea kutoa mkazo katika kilimo ili kuwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na pia kuwa na ziada kwa ajili ya viwanda vyetu.
Kadhalika serikali itaimarisha miundombinu ya umagiliaji maji katika mabonde yanayolima mpunga ili kuondokana na utegemezi wa kilimo cha kutegemea mvua.
Vile vile, elimu kwa wakulima itaimarishwa kupitia mashamba darasa na maonyesho ya kilimo yanayofanywa kila mwaka Unguja na Pemba ili kuongezeka uzalishaji.
Ndugu Wananchi, napenda kukumbusha wananchi wenzangu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuendeleza sekta ya uchumi wa buluu ambayo ndio njia muhimu itayowezesha nchi yetu kupata maendeleo ya uchumi kwa kasi tunayoitaka.
Kupitia uchumi huo wa bahari unaofungamanisha sekta mbalimbali zikiwemo uvuvi, ufugaji wa kisasa wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki,ukulima wa mazao ya baharini, uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na sekta ya utalii.
Sekta zote hizo zitasaidia sana kutoa ajira za kudumu kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Aidha, uchumi wa buluu utachangia sana kuongeza mapato yatokanayo na kodi na ada mbali mbali.
Ndugu Wananchi, Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha miundomibu ya usafiri na usafirishaji. Serikali ya Awamu ya Nane, itaendelea na uimarishaji wa miundombinu hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara katika maeneo ambayo huduma hiyo haijafika ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kuimarisha maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo. Katika kufikia lengo letu la kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, tutaimarisha huduma za Uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume na Uwanja wa Pemba.
Vilevile, bandari ya Malindi na ile ya Wete na Mkoani Pemba zitaendelea kuimarishwa kwa kununuliwa vifaa vipya vya kuchukulia na kupimia makontena pamoja na vifaa vya kukagulia mizigo na abiria wanaopita kwenye bandari hizo.
Serikali ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mangapwani. Sambamba na jitihada hizi, usimamizi wa shughuli za bandari na viwanja vyetu vya ndege utaimarishwa.
Ndugu Wananchi, Nafahamu mchango mkubwa unaotolewa na watumishi wa umma katika kujenga nchi yetu. Wote tunafahamu kuwa ipo Mipango na Mikakati iliyoandaliwa kuhakikisha kuwa malengo yetu ya kuimarisha uchumi na huduma za jamii inafikiwa.
Ni muhimu kila mmoja wetu akatambua kuwa sote tunayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa. Kila mtumishi anapaswa kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Hayati John Kenedy aliyekuwa Rais wa Marekani mwanzoni mwa miaka ya 1960, aliwahi kuwaasa wananchi wake kuwa wasiulize “Amerika imewafanyia kitu gani”, na badala yake, wajiulize “wao wameifanyia nini Amerika”.
Maneno haya yana maana kubwa kwetu kama Wazanzibari, na hivyo hata watumishi wetu wa umma, wanapaswa kujiuliza kuwa “tumeifanyia nini Zanzibar”.
Ndugu Wananchi, Nimetumia maneno haya ya Hayati Kennedy kutokana na mantiki yake ya kushajiisha uzalendo. Tunakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta za kiuchumi na kijamii;- miundombinu isiyoridhisha, vijana wetu hawana ajira, skuli hazina madawati na walimu wa kutosha, maji hayapatikani kwa kiwango kinachotakiwa, na huduma za afya hasa kwa akina mama na watoto bado hazijaridhisha.
Wakati Serikali ikiwekeza katika Sekta za vipaumbele kama ilivyoainishwa katika Dira ya maendeleo ya 2050, ni wazi kuwa kutakuwepo umuhimu wa kuwa na uwiano kati ya uwekezaji huo, na uwajibikaji wa watumishi wa umma.
Serikali imedhamiria kurejesha nidhamu ya kufanya kazi na kutokomeza mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha binafsi.
Katika tafsiri pana zaidi, hatua hizo zinalenga kukuza utamaduni wa uadilifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa uhodari, bidii na ufanisi mkubwa.
Kamwe watumishi wa Umma wasisahau kuwa wao ni watumishi, sio mabwana, wa wananchi.
Wawatumikie kwa ufanisi, kwa uaminifu na kwa heshima wakitambua kuwa huo ndio wajibu wao.
Ndugu Wananchi, tunafahamu kuwa rushwa ni adui wa haki na kikwazo kikubwa cha maendeleo ya jamii na taifa.
Nchi ikiwa imegubikwa na vitendo vya rushwa itakosa maendeleo stahiki na watu watadhulumiwa haki zao.
Hizo ndizo sababu kuu zilizoifanya Serikali yetu ichukie rushwa na kuchukua hatua za kupambana na uovu huu, tangu kufanyika kwa Mapinduzi miaka 57 iliyopita.
Kazi hiyo ngumu na yenye changamoto nyingi hivi sasa inaongozwa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA), lakini ni lazima tuwaunge mkono.
Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha chombo hiki ili kiweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Tutahakikisha ZAECA inakuwa na mtandao mpana zaidi na ofisi kila Mkoa na kila Wilaya, watumishi wameongezeka na vitendea kazi pia.
Ndugu Wananchi, Naomba wananchi waendelee kutoa taarifa zitakazosaidia kuwatambua na kuwakamata watoaji na wapokeaji rushwa.
Tukumbuke kuwa mafanikio katika mapambano haya hayategemei Serikali au ZAECA peke yake. Ni mapambano ambayo jamii ikijihusisha kwa ukamilifu ushindi mkubwa utapatikana.
Kadhalika, napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa taasisi na idara zote za Serikali zinazohusika moja kwa moja katika vita dhidi ya rushwa zitimize ipasavyo wajibu wao.
Aidha, pakiwepo na ushirikiano mzuri na mshikamano wa dhati miongoni mwetu kwa hakika ushindi utapatikana. Tukifanya hivyo nina imani kwamba tutapata mafanikio makubwa zaidi tena kwa haraka.
Maendeleo ya Vijana
Ndugu Wananchi, Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua na kuthamini sana nafasi na mchango wa vijana katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu.
Ndio maana, Serikali inawekeza sana katika kuwapatia elimu na mafunzo ya kazi. Serikali imeamua katika mwaka ujao wa fedha kuongeza uwezo wa bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili iweze kuwahudumia vijana vizuri zaidi.
Tutaendelea kuongeza bajeti hiyo ili Wizara iweze kuwaongezea vijana mitaji ya biashara kupitia Mfuko wa uwezeshaji.
Nawasihi vijana watakaopata mikopo kupitia Mfuko huu pamoja na Mifuko mingine ya uwezeshaji wahakikishe wanaitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa na kuirejesha kwa wakati ili wengine nao wapate.
Ndugu Wananchi, Tokea kuingia madarakani nimekuwa nikisisitiza na kufuatilia suala la usafi nchini mwetu. Bado maeneo mbali mbali ya nchi yetu ni machafu na hayaendani na sifa ya Zanzibar duniani. Kazi ya kuweka nchi yetu katika hali ya usafi ni yetu sote.
Kwa hivyo, naendelea kuwakumbusha wananchi wenzangu wajibu wa kuweka maeneo yetu katika hali ya usafi.
Pindi kila mtu atatimiza wajibu wake basi tutafanikiwa ndani ya muda mfupi sana. Wakuu wa Mikoa na Wilaya lazima waandae utaratibu maalumu wa kushirikiana na Manispaa na Mabaraza ya Miji pamoja na wananchi katika kushughulikia usafi wa miji na maeneo yao.
Usafi wa miji na maeneo yetu tunayoishi isiwe unafanywa kama tukio lakii iwe ni jambo la kudumu na kuendelezwa.
Ndugu Wananchi, nchi yetu ina changamoto nyingi za kimazingira. Mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani sambamba na uhaba wa wataalam wa kutosha ni mambo tunayotakiwa kuyazingatia na kuyapatia msisitizo.
Lazima tukubali kubadilisha aina ya maisha tunayoishi na kuhamasisha wananchi kutumia teknolojia mpya hasa zinazosisitiza matumizi ya nishati zisizoathiri mazingira katika shughuli za kila siku katika maisha yetu.
Kwa upande wake, Serikali yetu imejiandaa kupanua matumizi ya gesi asilia kwa kupikia na matumizi mengine ili tupunguze uzalishaji wa gesi mkaa kwa kiasi kikubwa na kunusuru misitu yetu.
Kadhalika, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuendeleza upandaji wa miti na kujenga matuta ili kuzuia kuingia maji ya chumvi katika mashamba ya kilimo na maeneo ya makaazi ya watu.
Ndugu Wananchi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuuimarisha Muungano wetu.
Vile vile, tutahakikisha kuwa tunashirikiana katika mambo yasiyokuwa ya Muungano kama tunavyofanya sasa kwa faida ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mimi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunatambua uzito wa dhamana mliyotupa Watanzania, katika kuhakikisha kuwa Muungano wa Tanzania, unadumu na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa Awamu zilizotangulia.
Nakuhakikishieni wananchi nyote, kwamba Serikali zetu mbili, zitaendelea kuchukua hatua, ili nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na ibaki kuwa nchi ya amani na utulivu.
Ndugu Wananchi, Maendeleo yetu yanategemea sana kuwepo kwa amani na usalama nchini.
Jukumu la kulinda amani na usalama wa nchi yetu ni letu sote kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Navipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kuilinda nchi yetu na mipaka yake.
Napenda niwahakikishie wananchi na wageni wanaoitembelea nchi yetu kwamba nchi yetu iko salama na kwamba Serikali zetu mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wao wa kikatiba na kisheria katika kulinda amani, utulivu na maisha ya wananchi na mali zao.
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa hutuba yake fupi katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar sherehe zilizofanyika leo viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar .
Natumia fursa hii kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika jitihada zake za kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi, uhujumu wa uchumi, dawa za kulevya na kuzilinda raslimali za nchi yetu.
Sote ni wajibu wetu tumuunge mkono katika vita hivi kwa kuzingatia kuwa rushwa ni adui mkubwa wa haki na ni adui wa jitihada zetu za kuleta maendeleo nchini.
Ndugu Wananchi, namalizia risala yangu kwa kutoa shukurani na pongezi kwa viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na watumishi wote kwa jitihada zao katika kuwatumikia wananchi kwa moyo wa uzalendo hadi kuyafikia mafanikio tuliyoyapata. Wito wangu ni kwamba tuongeze kasi katika kutekeleza wajibu wetu kwa misingi ya haki, uadilifu na utumishi bora na kuwatumikia wananchi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao.
Natoa shukurani maalumu kwa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa inayoongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah, kwa uongozi wake mahiri na kuhakikisha kuwa maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yamefanikiwa.
Ndugu Wananchi, ni muhimu sana kuendelea kuyalinda, kuyatetea na kuyadumisha Mapinduzi yetu, kama tulivyofanya katika miaka iliyopita kwa mafanikio makubwa.
Tuendelee kuiombea nchi yetu amani, umoja na mshikamano, ili tuzidi kupiga hatua za maendeleo.
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kunisikiliza