Ibrahim Kashatila (29) ambaye ni Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima kilichopo mjini Namanyere, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Picha ikionyesha mfano wa kisima. (Mtandao).
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Theopista Mallya amesema, taarifa za kupotea kwa marehemu zilitolewa na mkewe Januari 23,2021 na juhudi za kumtafuta ziliendelea na ndipo Januari 27 majira ya saa 11:30 jioni zilitolewa taarifa za mwili wa kijana huyo kupatikana kwenye kisima akiwa amekufa.
Amesema kuwa, marehemu alitoka nyumbani kwake Januari 23, mwaka huu akienda matembezini na kuwa toka siku hiyo hakuonekana nyumbani wala kazini kwake na taarifa zilitolewa Polisi na juhudi za kumtafuta ziliendelea hadi pale mwili wake ulipopatikana kwenye kisima kilicho karibu na baa moja mjini Namanyere inakosadikika kuwa alikuwa wakinywa pombe na ulipatikana baada ya siku nne.
Kamanda Mallya amesema kuwa, uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaendelea ili kuweza kubaini chanzo cha kifo hicho na kuwa wao kama Polisi kwa sasa wanasubiri taarifa ya kitabibu ambayo wataiunganisha na taarifa za kiuchunguzi.
Amesema kuwa, sasa ni mapema sana kwao kuzungumza mambo kwa kina lakini uchunguzi ukikamilika watatoa taarifa kamili ya tukio hilo.
Ndugu wa marehemu walikabidhiwa mwili kwa ajili ya maziko kabla ya hatua za awali za uchunguzi kukamilika.
Tags
Habari