Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif awaeleza wananchi walivyojiimarisha na Rais Dkt.Mwinyi kuwaletea neema

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameanza ziara yake kwa kukutana na wananchi wa makundi mbalimbali ambao ni viongozi wa Serikali,viongozi wa dini,watu mashuhuri, wazee, vijana na wanawake kutoka Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, anaripoti Mwandishi Diramakini (Pemba).
Baada ya ukaribisho kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahor Masoud, Makamu wa Kwanza wa Rais ameanza kwa kutoa nasaha zake kwa Wananachi ambapo ameeleza kwa upana historia ya Zanzibar kabla na baada ya Uhuru, mkazo zaidi ulikuwa ni juu ya athari za siasa za mivutano ambazo zimekuwa zikiathiri ustawi wa Zanzibar.

Maalim Seif katika mazungumzo hayo ya Januari 2, 2021 amesisitiza kwamba sisi sote tuna maslahi mapana na hatma ya Zanzibar, na kama maslahi yakiwa mazuri sote tutanufaika, na maslahi yakiwa mabaya basi sote tutaathirika, hivyo lazima tutambue sisi ni ndugu na Zanzibar ndio nyumbani kwetu, tusishiriki kuibomoa nyumba yetu.

Kwa kusisitiza hilo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif amesema, 

"Wazanzibari tumepewa neema kubwa ya umoja, hata lugha yetu ya kuwasiliana ni moja ya Kiswahili, na hata dini waliowengi wanaabudu dini sawa, hii inaonesha kwamba hili ni taifa lililoshikamana na hii ni tunu ya Taifa, kwa hiyo nawasihi sana Wananchi wenzangu asitokee mtu wa nje akaleta chokochoko na kulichafua Taifa hili, kwani gharama ya kuirudisha amani itakuwa kubwa sana,"amesema Makamu huyo wa Rais.

Maalim Seif amesema suala la ushirikiano katika nchi haliepukiki kwani Zanzibar inahitaji umoja na mshikamano wa hali ya juu, na ndio maana mpaka sasa kuna Serikali ya Umoja wa kitaifa, hii ni kuonesha kwamba maendeleo ya Zanzibar yataletwa na Wazanzibar wenyewe.
Maalim Seif pia amewaambia wananchi hao kwamba, "Mfano mzuri wa mshikamano ni ule uliodumu kati ya mwaka 2010 mpaka 2015 ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambapo maisha ya utulivu na hali ya amani katika nchi yalionekana wazi, hivyo ushirikiano ni muhimu kwa Taifa,"amesema.

Maalim ametoa msimamo wake wazi kwa kusema, "Mbali na yote yaliyotokea Mimi Maalim Seif na mwenzangu Rais Husein Mwinyi tumesafiana nia na lengo letu kwa sasa ni kujenga nchi hii, kuweka umoja na mshikamano na dhamira yetu kuu nikuipeleka nchi hii katika hatma njema kwa maslahi yetu na vizazi vyetu,"amesema.

Maalim Seif amesisitiza kwamba suala la maendeleo litafikiwa ikiwa katiba ya Zanzibar itafuatwa kikamilifu, na kuheshimiwa kwa kuhakikisha Wananchi wote wanapata haki sawa sambamba na kupiga vita rushwa na ubaguzi.

Katika kukazia suala la maendeleo, Maalim Seif amewaelekea viongozi wa Serikali kwa kuwaambia kwamba, "Mafanikio ya Zanzibar yatakuja kwa kutenda haki sawa na uadilifu kwa wananchi, na hili litafanyika kwa kuweka itikadi za vyama vyuma na kutumikia wananchi kwa usawa, na kila kiongozi ajue wajibu huo na atende haki, na hili ni kuanzia kwa viongozi wakuu wa nchi mpaka ngazi za chini (Sheha wa Shehia),"amesema.

Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa fursa kwa makundi hayo ya wananchi kuuliza maswali, kutoa maoni na ushauri kwa Serikali.

Kwa kumalizia alitoa ufafanuzi wa hoja za Wananchi kuhusu ajira, na maisha bora kwa wananchi kwa kusema, Serikali imetoa tamko la kupunguza kodi kwa wawekezaji watakaokuja kuwekeza kisiwani Pemba, na ni jambo ambalo litaweza kuzalisha ajira za kutosha kwa wananchi wa kisiwani humo kupitia viwanda vitakavyojengwa, lakini pia lengo la Serikali ni kuhakikisha kisiwa cha Pemba kinainuka kiuchumi na kufanana na kisiwa cha Unguja ili Zanzibar yote iwe sawa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news