Mancherster United, Arsenal zatoka sare dimba la Emirates

Manchester United imeendelea kupoteza alama katika mechi nne za Ligi Kuu nchini England baada ya mchezo wa Januari 30, 2021 dhidi ya Arsenal kumalizika kwa sare tasa, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanange huo wa nguvu umepigwa katika dimba la Emirates ambapo mshambuliaji wa Manchester United, Edinson Cavani amepata nafasi mbili za wazi, lakini ulinzi wa kikosi cha kocha, Mikel Arteta uliweza kumdhibiti.

Pia Arsenal walikuwa na nafasi ya kupata goli kupitia kwa Alexandre Lacazette ambaye mpira wa kutengwa uligonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya shuti la Emile Smith Rowe kuokolewa na kipa David de Gea lakini shuti la Nicolas Pepe kutoka sentimita chache.

Matumaini ya United kuwania ubingwa yameanza kufifia kwa sababu wako nyuma ya vinara wa ligi Manchester City na pengo la alama 3 huku City wakiwa na mechi moja ya ziada.

Katika mtanange huo, mlinda mlango Bernd Leno wa Arsenal alifanya kazi ya ziada katika vipindi vyote viwili vya mechi na kuwanyima Edinson Cavani, Fred na Marcus Rashford nafasi za wazi ambazo vinginevyo, zingempa kocha Ole Gunnar Solskjaer ushindi muhimu wa ugenini.

Aidha, Arsenal katika mtanange huo waliwakosa wachezaji wake Pierre-Emerick Aubameyang, Kieran Tierney na Bukayo Saka, hivyo kumtumia Martin Odegaard kwa mara ya kwanza tangu akamilishe uhamisho wake kwa mkopo kutoka Real Madrid.

Kwa upande wa Manchester United wamelazimika kumuondoa kiungo Scott McTominay uwanjani katika kipindi cha kwanza na nafasi yake ikazibwa na Anthony Martial.

Hata hivyo, Manchester United kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 41, tatu nyuma ya viongozi Manchester City ambao wana mchuano mmoja zaidi ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimechezwa na Manchester United.

Manchester City awali iliwapa kichapo Sheffield United cha bao moja kwa ubuyu katika dimba la Etihad. Wakati Manchester United wakiendeleza rekodi ya kutoshindwa ugenini, Arsenal nao wameendeleza rekodi ya kufanya vizuri katika mechi saba zilizopita huku wakikosa kufungwa katika mitanange mitano kati ya sita iliyopita.

Gunners wanashikilia sasa nafasi ya nane kwa alama 31, sita nyuma ya mabingwa watetezi Liverpool waliopo katika nne bora kwa sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news