Kaimu Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba SC, Selemani Matola amesema kuwa kilichowafanya wapoteze kwenye mchezo wao wa fainali dhidi ya watani zao wa jadi Yanga SC ni matokeo ya mpira ndani ya uwanja.
Simba kwenye Kombe la Mapinduzi ilitinga hatua ya fainali kwa kushinda mechi zake zote tatu ila ilikwama kusepa na taji la Mapinduzi baada ya kushindwa kuwafunga watani zao wa jadi Yanga.
Fainali hiyo iliyochezwa visiwani Zanzibar, Uwanja wa Amaan, dakika 90 zilikamilika kwa sare ya bila kufunga ila kwenye mikwaju ya penalti Simba ilikosa penalti mbili zilizopigwa na Meddie Kagere na Joash Onyango.
Kwa upande wa Yanga ni penalti moja ilikoswa iliyopigwa na Tonombe Mukoko na kufanya Yanga ishinde kwa mabao 4-3.
Matola amesema kuwa, kilichotokea Uwanja wa Amaan ilikuwa ni sehemu ya matokeo ya mpira jambo ambalo hawawezi kulibadilisha.
"Wachezaji walipambana ndani ya uwanja kusaka matokeo ila haikuwa bahati yetu kuweza kutwaa ubingwa hivyo hakuna chaguo.
"Kwa kilichotokea ni maumivu lakini ikumbukwe zile zilikuwa penalti na hakuna fundi linapofika suala la penati hakuna namna ya kubadilisha," amesema.
Yanga inakuwa imefikisha jumla ya mataji mawili ya Kombe la Mapinduzi huku Simba ikiwa na mataji mawili ya Kombe la Mapinduzi.
Tags
Michezo