Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yanaonesha ukakamavu, uzalendo na utayari wao katika kuipigania nchi yao sambamba na kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akizungumza na vijana wanaoshiriki Matembezi ya Maadhimisho ya sherehe za Miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakati wa hafla ya mapokezi ya vijana hao katika Wilaya ya Magharibi “B” Unguja katika Skuli ya Msingi Mwera.(Picha na Ikulu/ Diramakini).
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo katika hotuba yake ya kuyapokea matembezi ya bijana hao wa CCM ya kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, hafla iliyofanyika Mwera, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mama Mariam Mwinyi ameeleza lengo lake la kuwapongeza na kuwatia moyo vijana hao kwa kuwatia faraja wazazi wao kutokana na ushiriki wao huo huku akisema kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuyatangaza Mapinduzi ya Zanzibar nchini kote.
Ameeleza kuwa, mbali ya kutembea vijana hao wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo kufanya usafi katika maeneo kadha wakati wakiwa katika matembezi hayo ambapo hatua hiyo inaonesha wazi jinsi wanavyomuunga mkono Rais Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha maeneo yote yanakuwa safi.
Pia, Mama Mariam Mwinyi amewapongeza vijana hao kwa hatua zao za kujumuika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii ikiwemo ujenzi wa skuli hatua ambayo wamekuwa wakiiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane katika maendeleo ya nchi.
Akitoa salamu za Rais Dkt. Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa, Rais Dkt. Mwinyi yuko pamoja na vijana hao na anawaunga mkono kutokana na juhudi zao na yuko tayari kushughulikia changamoto zinazowakabili zikiwemo zile za ajira, elimu na nyinginezo.
Aidha, Mama Mariam Mwinyi akiwa kama mama amewaasa vijana kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya kwani yanapotosha vijana na yamekuwa yakipoteza nguvu kazi ya Taifa kwani asilimia kubwa ya watu wa Zanzibar ni wale waliozaliwa baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 wakiwemo vijana.
Amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita suala zima la uzalilishaji wa wanawake na watoto na kuwataka kutojingiza katika masuala hayo na kusema kwamba akiwa ni mzazi mambo hayo yamekuwa yakimuumiza sana.
Hivyo, amewataka vijana hao kuwa mabalozi na kuwa macho kwani wengi wanaotenda mambo hayo wamo katika jamii, na kutaka wailinde nchi hayo sambamba na kuwafichua waovu wote wanaotenda mambo hayo.
Sambamba na hayo, amewataka vijana kujitahidi kufahamu Sera na vipambele vya nchi ili waweze kujua fursa ziko wapi na kujua nchi inakwenda wapi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kufuata fursa za uchumi wa buluu ambao ndio uliopewa kipaumbele hivi sasa hapa nchini.
Amesema kuwa, iwapo watafahamu Sera na kupata habari juu ya mikakati ya Serikali hatua hiyo itasaidia kutambua na hatiamae kuweza kupata ajira na hatimae kupata kipato.
Mama Mariam Mwinyi alikubali ombi la vijana hao kuwa mlezi wa matembezi hayo na kuahidi kuwapelekea zawadi maalum sambamba na kupokea maombi ya kuwasidia wale vijana wa CCM wanaotoka nje ya Zanzibar kwa kuwawezesha kufika na kushiriki kikamilifu katika matembezi hayo ya kila mwaka.
Sambamba na hayo, amewatakia kila la heri washiriki wote wa matembezi hayo na kueleza kuwa yuko tayari kuwaunga mkono ili kutekeleza malengo ya kuyaenzi na kuyatunza Mapinduzi matukufu ya Januari 12. 1964.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa ambaye pia ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Mwita Maulid amempongeza Mama Mariam Mwinyi kwa ujio wake huo na kueleza jinsi vijana walivyofarajika huku akieleza jinsi vijana hao wanavyoyaenzi Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kupitia matembezi hayo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (CCM) Zanzibar, Mussa Haji amesema kuwa Matembezi hayo yalizinduliwa Januari 5, 2021 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla huko Pwanimchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kuwa, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umekuwa na desturi ya kufanya Matembezi kila mwaka yakiwa na lengo la kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ambapo pia, hufikisha ujumbe kwa jamii pamoja na kufanya shughuli kadhaa za kijamii.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameeleza shughuli mbalimbali walizozifanya vijana hao katika matembezi ya mwaka huu ikiwemo ujenzi wa miradi ya maendeleo pamoja na kufanya usafi.
Ameongeza kuwa, vijana hao wapatao 800 ni kutoka Mikoa yote ya Tanzania ambapo kila Mkoa umetoa mwakilishi wakiwa na lengo la kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Januari 12, 1964.