Mpango wa JIFUNZE unaotekelezwa na shirika la UWEZO Tanzania na Champion Chanzige umeanza kuleta mafanikio katika sekta ya elimu kupitia mfumo shirikishi uliohusisha walimu, wazazi na wanafunzi na hivyo kusaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuhesabu kwa siku thelathini tu katika shule tano teule zilizopo wilayani Kisarawe mkoani Pwani, anaripoti Ahmad Nandonde (Diramakini) Kisarawe.
Mratibu wa mradi wa Jifunze wilayani Kisarawe,
Bi. Gega Bujeje. (Picha na Diramakini).
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mradi wa JIFUNZE Kisarawe, Gega Bujeje alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hii na kueleza kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa sana ya kielimu wilayani humo na hii ni kutokana na mahusiano mazuri yaliyotopkana na mafunzo maalum yaliyotolewa kwa walimu wa mpango huo.
Gega amesema awali kabla ya kuingia kwa mpango wa JIFUNZE suala la ushirikiano kwa baadhi ya wazazi na walimu na hata wanafunzi hakikua kitu cha kawaida lakini tangu ulipoingia mradi huu hali imebadilika na hii imeendelea kuwa chachu ya walimu kuongeza ufanisi katika ugundishaji.
Amesema, ilikua ni aghalabu kuona mwanafunzi anasimama na kumpokea mwalimu au hata wazazi kufika tu shuleni kuulizia maendeleo ya mtoto wake hatua ambayo imekua ikichangia kwa kiasi kikubwa mdororo wa elimu kwa wanafunzi.
Aidha Gega ameongeza kuwa, ushirikishwaji wa wazazi umetoa mwamko kwa walimu kuongeza hari ya kuendela kuwafundisha tofauti na hapo awali.
‘’Suala la ushirikishwaji wa wanafunzi kwakweli umesaidia sana kuongeza idadi ya wanafunzi kwani mbinu ambazo hutumiwa na walimu wetu ni zile ambazo walimu hutumia zaidi michezo nyimbo na hata ilifika wakati wanafunzi wetu walikua wanapata chakula wakiwa masomoni hivyo ilisaidia sana watoto kusoma kwa hari,’’amesema Gega.
Amesema, kwa kupitia njia ya ushirikishwaji walimu huwafundisha watoto na hata wakati mwingine huwa sehemu ya mchezo kwani huimba na kucheza pamoja.
Amesema wakati mwingine kinachofurahisha zaidi ni pale walimu wanapowapa nafasi wanafunzi kusogea ubaoni na kutoa mifano juu ya kile walichofundishwa huku walimu hao wakitumia lugha nzuri ya kuwafundisha wanafunzi hao.
Mmoja wa wazazi wenye watoto walionufaika na mpango wa JIFUNZE, bw. Selemani Kinguruwe amesema hatua ya mpango huo kuwashirikisha wazazi kumewapa fursa ya wao kama wazazi kujiona sehemu muhimu sana ya kuwafikishia watoto elimu kwani sasa wanakagua walichokisoma watoto wao pindi tu wanapotoka shuleni.
Kinguruwe amesema, yeye kama mzazi suala la kuangalia mtoto amefanya nini shuleni halikua la kwake bali alichokijua ni kwamba ameshampeleka mtoto shuelni hivyo suala la kusoma au kaelewa halimuhusu.
‘’Kwakweli sasa najiona nimebandilika sana nafuatilia mwenendo wa mtoto kuanzia asubuhi mpaka anaporejea shuleni na nasema sitaki masihara katika elimu kwani mimi sikusoma na mwanagu asisome haiwezekani. ‘’Mtoto kabadilika sana hivyo akawashauri wazazi wengine kuendelea kuwapa nafasi watoto, lakini pia kukagua madaftari ya watoto wao,"amesema.
Tags
Habari