Mwanafunzi Said Yusuph Robert aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Luholongoma, Kata ya Kafunzo, Halmashauri ya Buchosa, mkoani Mwanza, ambaye anatokea kijijini katika familia isiyo na uwezo, amefanikiwa kufanya vizuri katika matokeo yake ya mtihani wa taifa wa darasa la saba kwa kupata alama 'A' katika masomo yake yote, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Said amechaguliwa kwenda kuendelea na masomo ya sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne) katika Shule ya Sekondari Kibaha iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Uwezo wa mtoto huyo ulimkuna Mbunge wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, ambaye aliamua kumchukua ili kumsaidia katika majukumu ya masomo yake ikiwa ni pamoja na kumlipia ada na gharama za masomo mpaka atakapohitimu masomo yake.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumpongeza na kumuaga mwanafunzi huyo katika ofisi za makampuni ya Global Group zilizopo Sinza-Mori jijiji Dar es Salaam, leo Jumanne, Januari 12, 2020, Shigongo amesema siyo watoto wote waliofeli masomo vijijini hawana akili, bali mazingira duni ndiyo yanayosababisha watoto hao washindwe mitihani lakini wana akili nyingi.
"Tumemfanyia hili jambo kuwatia moyo vijana wengine, kumheshimu mtoto huyu Said, lakini pia ajue kwamba ana kazi kubwa katika safari yake ya masomo huko anakokwenda. Sisi kama wazazi, watoto wa namna hii lazima tuwasapoti kwa sababu wanaweza kuja kuwa hazina ya taifa letu hapo baadaye.
"Haijalishi umezaliwa mahali gani katika taifa hili, tambua kuwa una akili na una uwezo, usikilize maneno ya watu wala usiangalie mazingira, tambua Mungu alikuumba kwa mfano wake na unaweza kufanya chochote na kuwa chochote unachotaka. Kama iliwezekana kwetu na historia zetu inawezekana na kwa wengine.
"Kama taifa lazima tubebane, twende chini pamoja na tupande juu pamoja, kama taifa lazima tujifunze kwenda mbele pamoja, gusa maisha ya mtu usitegemee kulipwa, sababu unayemsaidia atamsaidia mwingine, tukiendelea kufanya hivyo maisha yetu yatabadilika ndani ya muda mfupi.
Akizungumza, Said amesema: "Nimesoma Shule ya Msingi Luholongoma katika mazingira magumu sana, lakini Mungu ndiyo amepanga kila kitu mpaka nikafaulu na kupangwa kuja kusoma Shule ya Sekondari Kibaha.
Said akizungumzia mazingira aliyotoka na kumshukuru Mungu kwa kumwinua huku akiamini kuwa atafanya makubwa zaidi siku zijazo.
"Pili namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kusikiliza ombi langu, sina maneno mengi ya kusema lakini nawaomba Watanzania wote waniombee, tuweke juhudi katika jambo tunalofanya, tutafanikiwa kwa uwezo wa Mungu."
Aidha, wakizungumza kwa ajili ya kumpa neno la ushauri kama wazazi na walezi, wafanyakazi wa Global Group wamemsihi Said asijiunge na makundi mabaya afikapo shuleni, badala yake andeleze ratiba na tabia yake ileile aliyokuwa nayo kijijini ya kujisomea kwa bidii na kumuomba Mungu amuongoze katika masomo yake ili atimize ndoto zake.
Baada ya kukamilishiwa mahitaji yake, Saidi ameondoka leo kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana Wenye Vipaji Maalum Kibaha kwa ajili ya kwenda kuanza rasmi masomo yake.
Tags
Habari