Mwenyekiti CCM Mara (No.3) akemea chuki, ubinafsi wa viongozi wa Serikali mkoa dhidi ya chama

Viongozi wa Mkoa wa Mara kuanzia ngazi za chini hadi juu wametakiwa kudumisha umoja na mshikamano na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hatua ambayo itawezesha usimamizi wa shughuli za maendeleo ya wananchi kwenda kwa kasi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) wakati akihutubia kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini hapa.

Amesema, ndani ya mkoa huo kuna baadhi ya viongozi wa Serikali ambao wamekuwa hawana ushirikiano kwa viongozi wa chama kila wanapofuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, jambo ambalo linatoa picha mbaya na hata kukwamisha juhudi za Rais Dkt.John Magufuli za kuwaletea wananchi maendeleo.

“Mshikamano baina ya viongozi wa chama na Serikali unasaidia sana katika kusimamia shughuli za maendeleo. Hivyo panapotokea watu wenye chuki kwa wengine, wanajenga matabaka ambayo ni doa na hatari kwa mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya wananchi hapa Mara,”amesema Kiboye.

Katika hatua nyingine, Kiboye amesema hawatakubali kuona viongozi wa Serikali wanaokwamisha maendeleo ya wananchi, hivyo alisisitiza suala la utekelezaji wa ilani ya chama hicho ufanyike kwa ufanisi ili kufikia matokeo chanya haraka.

"Hakikisheni mnasimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kuanzia ngazi za chini hadi juu, hilo ndiyo jukumu letu kubwa, maana imani waliyotuonyesha wananchi ya kutupa ridhaa tunapaswa kuwahakikishia kuwa, hawakukosea kwa kuwa tunasimamia na kutekeleza kikamilifu ahadi zilizomo katika ilani ili kuharakisha maendeleo yao,"amesema Kiboye.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wana CCM kwa kazi nzuri ambayo waliifanya na kukiwezesha chama hicho kupata ushindi wa kishindo kuanzia ngazi za madiwani, wabunge na Rais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka jana.

"Kila wilaya ninawapongeza kwa sababu nadhani kila mmoja wenu anajua kuwa, kuanzia miaka sijui mingapi huko CCM haijawahi kupata ushindi huu wa kihistoria, katika mkoa huu na majimbo yote.

"Kwa sababu tumemuweka Mungu mbele na kujituma katika kufanya kazi kwa bidii, tumefanikisha ushindi mkubwa, hivyo nawapongeza sana. Kamati tendaji ya mkoa na jimbo ilijituma, lakini nampongeza pia Rais wetu Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa chama, Mangula walitutembelea, tuliona walifanya kazi kubwa sana, kipekee nampongeza Rais wakwa sababu hata kazi alizozifanya alituwezesha kupata ahueni kwa kufanya kazi nzuri alizofanya.

"Ndiyo maana kila mmoja alikuwa anasema Magufuli...Magufuli, tunawapa kura kwa sababu Magufuli amefanya kazi nzuri.Mungu aendelee kumsaidia kwa sababu utendaji kazi wake uliotukuka umetupa heshima kubwa Mkoa wa Mara,"amesema Kiboye.

Amesema, kila mmoja anapaswa kuisimamia Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kuanzia ngazi ya chini hadi juu unafanyika kwa wakati.

"Huu ni mwaka wa kazi, na chama cha mapinduzi tujenge chama, na mimi mwaka huu siwezi kusimama kutetea mtu wa Serikali, nyie wajumbe ndiyo wenye maamuzi. Twendeni tukafanye kazi,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news