Mechi ya fungua mwaka baina ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga SC inatarajiwa kuchezwa Januari 13, 2021 katika dimba la Amaan mjini Unguja katika Jiji la Zanzibar ikiwa wawili hao wanawania Kombe la Mapinduzi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mchuano wa nusu fainali baina ya Simba SC na Namungo FC katika kuwania Kombe la Mapinduzi ndani ya dimba la Amaan jijini Zanzibar. (Picha SC/Diramakini).
Pengine hiyo kwa sasa ni kati ya mechi kali ambazo zinasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki wa pande mbili hizo ambao mara nyingi wamekuwa wakionyesha kuwa kila mmoja yupo imara.
Hii ni orodha ya mabingwa Mapinduzi CUP
Mwaka Bingwa Mshindi wa Pili
2007 Yanga SC Mtibwa Sugar
2008 Simba SC Mtibwa Sugar
2009 Miembeni KMKM
2010 Mtibwa Sugar Ocean View
2011 Simba SC Yanga SC
2012 Azam FC Simba SC
2013 Azam FC Tusker FC
2014 KCCA Simba SC
2015 Simba SC Mtibwa Sugar
2016 URA Mtibwa Sugar
2017 Azam FC Simba SC
2018 Azam FC URA FC
2019 Azam FC Simba SC 2-1
2020 Mtibwa Sugar Simba SC 1-0
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC furaha yao ya kuingia katika fainali hizo imenogeshwa na Miraji Athuman na Meddie Kagere baada ya kuisaidia klabu hiyo kuzima ndoto za Namungo FC katika kusonga mbele.
Awali Wanajangwani, Yanga SC walitangulia kufuzu nusu fainali ilipocheza na Azam FC na kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya matokeo ya dakika 90 zikimaliza kwa sare ya bao 1-1.
Baadae Wekundu wa Msimbazi, Simba SC walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo FC baada ya safu ya ulinzi kujichanganya na kuwapa mwanya nyota wa Simba kufunga.
Meddie Kagere ambaye ana mabao mawili kwenye mashindano haya ndiye alianza kutikisa nyavu za Namungo baada ya kipa Nourdine Balora kutoka golini hivyo kumpa kazi rahisi Kagere kufunga ikiwa ni dakika ya sita tangu kuanza kwa mchezo huo.
Miraji ambaye amefikisha mabao manne sasa na ndiye anaongoza kwa mabao kwenye mashindano hayo alifunga bao la pili dakika ya 40 akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na Francis Kahata.
Tukirejea kwa upande wa Wanajangwani, wamefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 dhidi ya Azam FC katika dimba la Amaan mjini Unguja.
Yanga SC ikichuana na Azam FC katika michuano ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi ndani ya dimba la Amaan jijini Zanzibar. (Picha na YSC/Diramakini).
Winga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tuisila Kisinda alianza kuifungia Yanga SC dakika ya 52, kabla ya mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa kuisawazishia Azam FC dakika ya 67.
Aidha, katika mikwaju ya penalti kipa Benedict Haule aliokoa penalti moja tu, ya kwanza iliyopigwa na mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong lakini za Kisinda, Mkongo mwingine kiungo Tonombe Mukoko, mabeki Paul Godfrey 'Boxer', Abdallah Shaibu 'Ninja' na kiungo mzawa, Zawadi Mauya zikampita.
Kipa Mkenya wa Yanga SC aliokoa penalti mbili, ya kwanza iliyopigwa na kiungo mzawa Awesu Awesu na ya mwisho iliyopigwa na beki Mghana, Daniel Amoah - lakini za beki Mzimbabwe, Bruce Kangwa, viungo Mnyarwanda Ally Niyonzima, mzawa Mudathir Yahya na beki Mganda, Nicholas Wadada zikampita.
Mara ya mwisho Yanga SC kufika Fainali Kombe la Mapinduzi ilikuwa ni mwaka 2011 wakafungwa na mahasimu wao, Simba SC 2-0 mabao ya Shijja Mkina na Mussa Mgosi.
Kwa ujumla Yanga SC imecheza fainali ya Kombe la Mapinduzi mara mbili tu, nyingine mwaka 2007 walipochukua ubingwa kwa kuifunga Mtibwa Sugar.
Tags
Michezo