Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Januari 28, 2021 anatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa Hati ya Maelewano (MOU), inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani unaojumuisha Bandari tofauti ikiwemo bandari ya mizigo, uvuvi, mafuta na gesi asilia, chelezo pamoja na Mji wa kisasa, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Utiaji saini huo unatarajiwa kufanyika Ikulu jijini Zanzibar kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakayesaini Hati hiyo anatarajiwa kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Amour Hamil Bakari ambapo kwa upande wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman anatarajiwa kusaini Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Sheikh Mohammed Al-Tooq ambaye ataongoza ujumbe wa watu watatu.
Utiaji saini Hati ya Maelewano inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi katika Bandari hiyo ya Mangapwani ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kutekeleza Sera yake ya Uchumi wa Buluu.
Aidha, hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi kuelekea siku 100 tangu alipoapishwa kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.