Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Hati ya Maelewano (MOU) kati yake na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari huko Mangapwani/Bumbwini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa Saini ya Maelewano (MoU) kuhusu mpango mkuu wa Ujenzi wa Bandari na Mji wa Kisasa Mangapwani na Bumbwini Zanzibar.(kulia kwa Rais) Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg. Amour Hamil Bakari na (kushoto kwa Rais) Mkurugenzi Mkuu wa Oman Investment Authority (OIA) Sheikh.Mohammed Al Taooqi, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Kwa mujibu wa hati hiyo ya maelewano Bandari hiyo inatarajiwa kujumuisha Bandari tofauti ikiwemo bandari ya makontena na mizigo mchanganyiko, bandari itakayohudumia meli za uvuvi, bandari ya mafuta na gesi, bandari ya kuhudumia mafuta na gesi asilia, chelezo ya matengezo ya meli pamoja na Mji wa kisasa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameshuhudia utiaji saini huo uliofanyika leo Januari 28, 2021 Ikulu jijini Zanzibar kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza baada ya kumalizika utiaji wa Saini Hati ya Maelewano (MoU) ya ujenzi wa Bandari ya Mwangapwani na ujenzi wa Mji wa Kisasa Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyesaini Hati hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakari na kwa upande wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman aliyesaini ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Sheikh Mohammed Al-Tooqi ambaye aliongoza ujumbe kutoka mamlaka hiyo ya Oman.
Mara baada ya utiaji saini wa Hati hiyo ya Maelewano, katika hotuba yake aliyoitoa Rais Dkt. Mwinyi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari vilivyokuwepo katika hafla hiyo amesema kuwa, safari ya kuijenga Zanzibar sasa imeanza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza baada ya kumalizika utiaji wa Saini Hati ya Maelewano (MoU) ya ujenzi wa Bandari ya Mwangapwani na ujenzi wa Mji wa Kisasa Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Amesema kuwa, Serikali inaanza na bandari kwa sababu ndio uchumi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba bandari hiyo itakuwa kubwa na ya kisasa.
“Sasa tumeanza safari yetu ya maendeleo na moja ya miradi ya kwanza kabisa kwa Serikali ya Awamu ya Nane utakuwa ni huu,”amesema Dkt. Mwinyi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mwanasheria Mkuu Zanzibar.Dkt. Mwinyi Talib Haji na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Mhe.Rahma Kassim Ali, wakifuatilia hutub ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi, baada ya kumalizika zoezi la utiaji wa saini ya maelewano ya Ujenzi wa Bandari Mangapwani na Mji wa Kisasa Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza uharaka wa jambo hilo huku akieleza kuwa kuna bandari mbili zimekusudiwa ikiwemo ile ya Mpigaduri ambayo patajengwa bandari ya uvuvi ambapo mapema ya wiki ya mwanzo ya mwezi ujao utiaji saini Hati ya Maelewano wa bandari hiyo utafanyika.
Amesema kuwa, bandari hiyo haitokuwa ya uvuvi pekee bali itahusisha miundombinu, viwanda pamoja na vyuo vya masuala ya bahari na bandari hiyo itakuwa ni tofauti na mipango iliyokuwa hapo awali.
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) baada ya kumalizika kwa utiaji wa Saini ya Hati ya Maelewano (MoU) kuhusu Mpango Mkuu”Master Plan “ ya Ujenzi wa Bandari na Mji wa Kisasa Mangapwani na Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar..(Picha na Ikulu).
Ameongeza kuwa, Bandari ya Malindi lengo ni kuifanya iwe ya utalii, kwani ina eneo dogo na tayari hivi sasa imo ndani ya sehemu ya uhifadhi wa Mji Mkongwe.
Amesema kuwa, shughuli zote za biashara zikiwemo biashara za usafiri na usafirishaji zitahamia Mangapwani na eneo hilo la Malindi liwe eneo la kitalii ambapo mandhari ya eneo hilo itabadilika ambapo pia, utalii wa Mji Mkongwe nao utabadilika.
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) baada ya kumalizika kwa utiaji wa Saini ya Hati ya Maelewano (MoU) kuhusu Mpango Mkuu”Master Plan “ ya Ujenzi wa Bandari na Mji wa Kisasa Mangapwani na Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbin wa Ikulu Jijini Zanzibar..(Picha na Ikulu).
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza azma yake ya kuwa mambo hayo yaliyokusudiwa kufanyika kwa haraka ili Zanzibar iweze kuwa ni kitovu cha biashara pamoja na utalii.
Ameeleza mambo makubwa na mazuri ambayo yatakuwepo katika eneo la mradi wa Mangwapwani na kuipongeza Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman kwa kukubali kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika maono mapya ya kuwa na bandari ya kisasa.
Ameeleza matarajio yake ya kufanyika kwa haraka kazi hiyo ili utekelezaji wake uanze mara moja na kusisitiza kwamba itakuwa ni busara iwapo kazi hiyo itafanyika ndani ya miezi mitatu kwani hakuna miaka mingi ya kuzungumza na kuna miaka mitano ya kutekeleza na kuomba ifanyike kwa muda huo badala ya miezi sita iliyopo kwenye Mkataba kwani anaamini Mamlaka hiyo iko tayari na Serikali nayo iko tayari.
Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe.Rahma Kassim Ali, akizungumza wakati wa Utiaji Saini ya Maelewano (MoU) kuhusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari na Mji wa Kisasa Mangapwani na Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 28-1-2021.(Picha na Ikulu).
Mapema Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali amesema kuwa, ujenzi wa Bandari unaotarajiwa kufanyika Mangapwani/Bumbwini ni moja ya dhana sahihi ya kuimarisha uwekezaji na hatimae kuleta matokeo bora kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema kuwa, Mpango Mkuu huo unakusudio la kuubadilisha muonekano wa hivi sasa katika maeneo ya Mangapwani/Bumbwini ambapo pia, Serikali itajenga Mji wa Kisasa utakaojumuisha huduma mbalimbali zitakazosaidia uendeshaji wa bandari hizo.
Aidha, kwa maelezo ya Waziri huyo katika maeneo hayo patatengwa eneo maalum la ujenzi wa viwanda.
Amesema kuwa, baada ya Mpango huo kukamilika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaelekeza nguvu zake katika kuutekeleza pamoja na kufungua milango ya kuwashirikisha na kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza katika ujenzi wa bandari hizo na maeneo hayo ikiwemo ujenzi wa viwanda.
Aidha, amesema kuwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaahidi kutekeleza maelekezo ya Rais na kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uaminifu katika kusimamia na kutekeleza yaliyoainishwa katika hati hiyo ya maelewano.
Sambamba na hayo, Waziri huyo ameeleza kwamba tangu kuanza kwa uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imefungua fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kusimamia uwekezaji zenye maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Oman Investment Authority (OIA) Bw. Sheikh.Mohammed Al Taooqi, akizungunza kabla ya kutowa maelezo mafupi ya Ujenzi wa Bandari na Mji wa Kisasa Mangapwani na Bumbwini Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman, Sheikh Mohamed Al Taooqi ameeleza azma ya mamlaka hiyo ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza mpango huo.
Ameeleza mafanikio makubwa yatakayopatikana baada ya kukamilika kwa mpango huo huku akisisitiza ushirikiano wa pamoja katika kuhakikisha jambo hilo linafanyika kwa haraka huku akieleza utayari wa mamlaka hiyo kuanza kazi.
Utiaji saini Hati ya Maelewano inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi katika Bandari ya hiyo ya Mangapwani ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kutekeleza Sera yake ya Uchumi wa Buluu.
Aidha, hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi kuelekea siku mia tokea alipoapishwa kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.