Rais Dkt.Mwinyi: Nendeni mkasikilize wananchi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuwasisitiza viongozi aliowateua kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto walizonazo,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mheshimiwa Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo Januari 29, 2021 wakati akitoa salamu zake kwa wananchi wa kijiji cha Nungwi mara baada ya kuungana nao katika sala ya Ijumaa huko katika Masjid Rahman iliyopo Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia na kuzungumza na Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya kumaliza kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid Rahma Nungwi.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi amesema kuwa kuna kila sababu kwa viongozi wake wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Mikoa kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Amesema kuwa, amegombea nafasi ya Urais kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuwasikiliza matatizo yao, kero zao zikiwemo huduma za jamii kama vile afya, elimu, maji na nyinginezo ambapo hivi sasa amekuwa akifanya mikutano kadhaa na wadau wa sekta hizo kwa azma ya kutatua changamoto zilizopo.

Amesema kuwa, changamoto hizo zinashughulikiwa na kusisitiza kwamba tayari alishawaambia wateule wake wakati akiwaapisha kwamba washuke chini wakawashughulikie wananchi changamoto zao za ardhi, kuondoa dhulma na changamoto nyinginezo.

Amewapa maagizo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Wilaya Kaskazini A, wakutane na uongozi kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kijiji cha Nungwi na kuwataka wakatatue na yale yaliyo chini ya uwezo wao wamjuulishe ili ayafanyie utatuzi.

Amesema kuwa, ana dhima ya kuhakikisha ana tenda haki kwa wananchi wote bila ya kujali uwezo wao kifedha, itikadi zao za kisiasa kwani yeye ni Rais wa Zanzibar na ana wajibu wa kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali matabaka, rangi, dini wala kabila.

“Ninaomba muendelee kuniombea dua ili Mwenyezi Mungu aniwezeshe kwa dhamira yangu njema niweze kutekeleza yale ninayokusudia katika kuwaletea wananchi maendeleo, niweze kuondoa dhuluma na kuweza kuwatendea haki wananchi wote wa Zanzibar,”amesema Dkt.Mwinyi.

Amewaomba wananchi wote wa Zanzibar kuendeleza amani iliyopo kwani hakuwezi kupatikana maendeleo iwapo amani itatoweka kwani imekuwa ni utamaduni kwamba kila ikikaribia uchaguzi amani hutetereka.

Amesema kuwa, jambo hilo linaathiri sana kidugu, kidini na kimaendeleo na kusema kwamba wananchi na viongozi wa dini waliombwa kuiombea nchi amani.

Amesema kuwa, kwa kiwango kikubwa hivi sasa nchi ina amani, hivyo ni wajibu wa wananchi wote kuiendeleza amani iliyopo.

Kwa upande wa umoja, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni kawaida kwamba umoja hutetereka kutokana na kutokuwepo kwake kutokana na itikadi za kisiasa.

Ameongeza kwamba, baada ya uchaguzi viongozi waliamua kukaa pamoja na kuridhiana na kuwaunganisha Wazanzibari ili kuondokana na mitafaruku iliyokuwepo kwani dini inataka watu waishi pamoja na inatakatasa mifarakano.

Amesema kuwa, ilifikia wakati watu walikuwa hawazikani, walipeana talaka kwenye ndoa kwa sababu ya kisiasa, hivyo ikaonekana hayo hayapaswi kundelezwa.

Kutokana na hali hiyo, ikaonekana hilo haliwezekani na ndipo viongozi walikaa na kuzungumza juu ya suala hilo ambapo safari hii hakukuwa na mtu kutoka nje kwa ajili ya kuwaunganisha wala kukaa kamati kubwa kubwa za chama ama serikali bali walikaa viongozi wenyewe wa vyama vyao wakajadiliana pamoja.

Amesema kuwa, kwa makusudi walikubaliana kuwaunganisha wananchi kwa kuanzia kwenye vyama vyao, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, na tayari imeshaundwa na mategemeo yake kwamba wananchi nao wataungana katika kuunga mkono juhudi hizo.

Amesisitiza kurudi katika umoja, mafundisho ya dini ya Kiislamu yanayosisitiza umoja na amani licha ya kuwepo wachache waliokuwa hawajakubaliana na hali hiyo.

Amesisitiza haja ya kuendelea kuelimishana kwamba umoja una umuhimu mkubwa katika Taifa lolote duniani.

Pia amesema kuwa baada ya kuwa na amani na umoja kinachofuatana ni kuwaletea wananchi maendeleo wanayoyataka.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa matarajio ya wananchi ni makubwa sana katika kuwaletea maendeleo na kuondosha dhulma na kufanikisha mambo wanayoyahitaji.

Mapema Sheikh Hassan Jani Masoud akisoma khotba ya sala ya Ijumaa alisema kuwa wananchi wa Nungwi wataendelea kumuombea dua Rais Dkt. Mwinyi usiku na mchana ili Mwenyezi Mungu amlinde hasa kutokana na kazi kubwa anazozifanya za kuwapigania wanyonge.

Sheikh Hassan amesema kuwa, wananchi wana matumaini makubwa ya kiongozi wao huyo katika kupigania haki na wanampongeza kwa jitihada zake hizo.

Sambamba na hayo, kwa niaba ya wananchi wa Nungwi Sheikh Hassan ameomba uongozi wa serikali kukutana na viongozi wa kijiji chao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili.

Sheikh Hassan amesisitiza haja ya kuendeleza maadili ya Kiislamu, kulinda amani pamoja na kusimamia haki za wanyonge.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amemtembelea Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita Alhaj Dkt. Aman Abeid Karume huko nyumbani kwake Mbweni nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news