Rais Dkt.Mwinyi:Endeleeni kuniunga mkono na kuniombea tuweze kuharakisha maendeleo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaomba wananchi wa Zanzibar wamuunge mkono katika kutekeleza azma yake ya kuiletea maendeleo Zanzibar sambamba na kupambana na ufisadi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisikiliza hotuba ya Sala ya Ijumaa ikitolewa na Sheikh Khalid Ali Mfaume Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, kabla ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Miembezi jijini Zanzibar na kushoto kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Januari 15, 2021 huko katika Msikiti wa Ijumaa Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamu kwa Waislamu mara baada ya kukamilisha Sala ya Ijumaa. 

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dkt.Mwinyi amesema kuwa, uungwaji mkono pamoja na dua vinahitajika kutokana na wanaofanya hayo wananufaika na pale panapozuiwa kutofanya na wao watatafuta la kufanya.

Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba, amegombea nafasi hiyo kwa azma ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar ambapo katika kutekeleza hayo yapo mambo ambayo yatafanywa na kuwaudhi watu kwa hivyo, uungwaji mkono unahitajika kwani yatakayofanywa yatawanufaisha wengi. 

Amesema kuwa, kwa hatua zinazochukuliwa hivi sasa maendeleo na mafanikio makubwa yatapatikana kwa sababu mambo muhimu ikiwemo amani na umoja yapo nchini licha ya wachache ambao hawajakubali na kueleza kwamba watazidi kuelimishwa.

Ameushukuru uongozi wa msikiti huo ambao una historia kubwa katika misikiti ya Mji wa Zanzibar pamoja na kuisifu hotuba ambayo imeeleza mambo mengi huku akiahidi kushirikiana na waumini hao katika kuuendeleza msikiti huo. 

Amesema kuwa, tokea aingie madarakani viongozi wamekuwa wakiwasisitiza wananchi kuwa wamoja hatua ambayo itapelekea kupatikana maendeleo yanayotarajiwa kwani ili kupata maendeleo ni lazima kuwepo kwa amani, umoja na uwajibikaji.

Amesema kuwa, viongozi wa siasa wameweza kuhubiri amani na umoja kwa vitendo kwa kuungana na kujenga Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa dhamira ya kuleta umoja katika nchi.

Alhaj Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa dini kwa kuhubiri amani na umoja hapa nchini. 

Kwa upande wa uwajibikaji Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa jambo hilo halina mtu maalum bali kwa kila mmoja anatakiwa kuwajibika wakiwemo viongozi na wale wasiokuwa viongozi, waliokuwa nje na ndani ya Serikali wote wanatakiwa wawajibike.

Amesema kuwa, kukua kwa uchumi kunahitaji kila mmoja kufanya kazi sambamba na uwajibikaji kwa kila mtu kwa azma ya kupata manufaa na maendeleo endelevu. 

Katika salamu zake hizo, amesema kuwa, kuwepo kwa amani, umoja na kila mtu akiwajibika mafanikio yatapatikana lakini wakitokea wabadhirifu, wazembe, wezi wa fedha za serikali na wala rushwa hapatakuwa na maendeleo.

Pia amesema kuwa, kwa makusudi jukumu limechukuliwa katika kuhakikisha hayo yote yanapigwa vita kwa nguvu zote na kuwataka wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono katika jambo hilo pamoja na kuwaombea dua viongozi wanaopambana. 

Amewashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kuwepo kwa umoja, amani na mshikamano nchini na kuwaona wananchi wakiwa na muelekeo wa kuwajibika katika nchini yao na kueleza imani yake ya kuona kila mtu anawajibika. 

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume ambaye pia ni Imamu wa msikiti huo amesema kuwa , Mwenyezi Mungu anasema kwamba hakika Waumini wote ni ndugu na vyema ikatafutwa suluhu pale wanapokosana sambamba na kumcha Mwenyezi Mungu ili wapate kurehemewa.

Amesema kuwa, suluhu ni jambo jema na migongano haina neema kwani Mwenyezi Mungu amekuwa akisisitiza umoja huku akieleza wale waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu wakiwemo walarushwa, wezi na wabadhirifu hivyo akitokea kiongozi wa kupambana na hayo ni vyema akaombewa dua. 

Wakati huo huo, Alhaj Dkt. Mwinyi alifika nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Tano Dkt. Salmin Amour Juma kwa ajili ya kumjulia hali na kuzungumza nae.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news