Rais Dkt.Mwinyi:Umoja wetu unazidi kutupa nguvu ya kusonga mbele zaidi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imedhamiria kuendeleza amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar ambayo inakwenda sambamba na misingi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt.Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 21, 2021 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ukiongozwa na Mkurugenzi wake, Joseph Butiku uliofika Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar pamoja na kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mhe. Joseph Butiku (kulia kwa Rais) akiwa na ujumbe wake walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo leo Januari 21, 2021.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeweza kuimarisha amani, umoja na mshikamano hapa Zanzibar hatua ambayo ni chachu ya maendeleo na imekuwa ikisisitizwa siku zote na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Amesema kuwa, hivi sasa kumekuwepo maelewano na ushirikiano mkubwa kati ya viongozi pamoja na wananchi walio wengi wa Zanzibar hali ambayo imepelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano tokea kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hapa nchini.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo imefikiwa kutokana na maridhiano yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo lengo na madhumuni yake makubwa ni kuendeleza umoja, amani na mshikamano ili Zanzibar izidi kupata maendeleo na wananchi wake wazidi kuelewana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa baadhi ya vitabu vya historia ya Mwalimu Julius Nyerere na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mhe.Joseph Butiku, baada ya kumaliza mazungumzo yao alipofika Ikulu jijini Zanzibar leo Januari 21, 2021.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuipongeza taasisi hiyo ya Mwalimu Nyerere kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ndani na nje ya nchi pamoja na Jumuiya za Kimataifa.

Amesema kwamba, taasisi hiyo imekuwa na mahusiano mazuri na Serikali zote mbili, ushirikiano na taasisi za kidini pamoja na vyama vya siasa ambapo imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na yenye kuleta tija.

A,etumia fursa hiyo kuipongeza taasisi hiyo kwa midahalo mizuri inayoiendesha ikiwemo ile inayozungumzia masuala ya amani ambayo imekuwa ikitoa maelekezo kwa wananchi katika suala zima la kusimamia amani, umoja na mshikamano nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mhe. Joseph Butiku (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo. (Picha na Ikulu/Diramakini). 

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kueleza kwamba taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zina dhima kubwa ya kuleta wananchi maandeleo badala ya kujikita zaidi katika masuala ya kisiasa.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa taasisi hiyo pamoja na nyingine zote hapa nchini katika kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja, amani na mshikano kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alilipokea ombi la taasisi hiyo la kuwa na ofisi zake hapa Zanzibar na kuahidi kufanyiwa kazi kwa azma ya kuiwezesha taasisi hiyo kufanya kazi zake vyema.

Mapema Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amemueleza Rais Dkt.Mwinyi azma ya ujio wao ikiwa ni pamoja na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika Oktoba, 2020.

Amesema kuwa, ushindi huo ni ushahidi tosha unaoonesha kwamba kwa namna gani wananchi wa Zanzibar wanaimani kubwa na Rais Dkt.Mwinyi katika azma yake ya kuwaletea maendeleo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mhe. Joseph Butiku (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na (kushoto kwa Rais), Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Sambamba na hayo,taasisi hiyo pia, imetoa pongezi kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa kuwezesha kuendeleza tena Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa lengo la kufikia demokrasia ya hali juu na maendeleo.

Pamoja na hayo, Mzee Butiku amesema kwamba hivi sasa Zanzibar imeweza kuonekana ikiwa na amani, umoja, utulivu na mshikamano mkubwa kutokana na maridhiano yaliyofanyika.

Aidha, ametumia fursa hiyo kumpa maelezo mafupi Rais juu ya lengo kuu na malengo madogo ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, muundo wake, kazi zake, ikiwa ni pamoja na maagizo rasmi na maalum aliyoyaacha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake kwa taasisi hiyo.

Sambamba na hayo, Mzee Butiku amemueleza Rais Dkt.Mwinyi juu ya shughuli inazozifanya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na uongozi wa Asasi za Kiraia na Mrajis wao kuzungumza na viongozi wa ngazi za Wilaya na Shehia wakiwa na nia ya matokeo ya mazungumzo hayo kwa kuandaa mafunzo ya uongozi na uendeshaji wa viongozi wa ngazi mbalimbali nchini.

Amesema kuwa, katika zoezi hilo wamepata ushirikiano mkubwa katika maeneo waliyokwenda katika Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba ambapo katika maelezo yao walieleza jinsi madiwani wa mikoa hiyo walivyoeleza imani na matumaini yao makubwa kwa Rais Dkt.Mwinyi serikalini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news