Rais Nana Akufo-Addo aapishwa kwa muhula wa pili Ghana

Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo ameapishwa kama rais kwa mhula wa pili madarakani, siku moja baada ya kutokea vurugu bungeni mjini Accra, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mashirika).
Rais wa Ghana, Mheshimiwa Nana Akufo-Addo akihutubia Taifa mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Taifa hilo la Magharibi mwa Afrika. Sherehe za kuapishwa zimefanyika mjini Accra nchini humo. (Picha na Nipah Dennis/AFP via Getty Images/ Diramakini).

Mheshimiwa Akufo-Addo alimshinda mpinzani wake rais wa zamani, John Mahama katika uchaguzi uliofanyika mwezi Desemba, 2020 na ambao ulikuwa na ushindani mkali zaidi.
Akufo-Addo alipata asilimia 51.6 ya kura katika uchaguzi huo wa Desemba 7, 2020 huku mpinzani wake, Mheshimiwa Mahama akijipatia asilimia 47.4 ambaye aliwahi kuhudumu kati ya mwaka 2012 na 2017. 

Wabunge wa Ghana, ambao walichaguliwa hivi karibuni walipigana bungeni baada ya kukosa kukubaliana namna ya kumteua spika. 

Uchaguzi wa spika ulikuwa umepangwa kufanyika kwa njia ya siri, lakini wabunge kutoka chama kinachotawala cha New Patriotic NPP, walikuwa wakionyesha hadharani waliyempigia kura, jambo ambalo liliwakera wabunge wa upinzani. 

Wakati mmoja, mbunge wa chama kinachotawala alichukua karatasi za kupigia kura kwa lazima wakati uchaguzi ulikuwa unaendelea na hivyo kuzua mgogoro. Polisi wenye silaha na wanajeshi waliitwa bungeni katika juhudi za kurejesha utulivu. 

Chama kinachotawala na upande wa upinzani, wana idadi sawa ya wabunge. Kuna mbunge mmoja asiyekuwa na chama cha kisiasa. 

Mahakama ilimzuia mmoja wa wabunge wa upinzani kushiriki katika kura hio ya kujaza nafasi ya spika, baada ya kesi kuwasilishwa mahakamani kupinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu. Mbunge huyo hata hivyo alikubaliwa na bunge kushiriki uchaguzi huo.Wanasiasa wa upinzani wamedai kuwepo udanganyifu katika uchaguzi huo wa mwaka jana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news