NA FRESHA KINASA
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly ameziomba mamlaka za Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wanaobainika kuwafanyia watoto wa kike vitendo vya kikatili.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania Rhobi Samwelly akizungumza na Waandishi wa Habari nyuma yake ni wasichana wa Kituo Cha Nyumba Salama Kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama.
Miongoni mwa vitendo hivyo ni pamoja na kuwakeketa na kuwaozesha katika umri mdogo, jambo ambalo huwafanya washindwe kuyafikia malengo yao na kudhoofisha maendeleo ya Taifa.
Pia amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kutoa kauli kali itakayosaidia kutokomeza vitendo hivyo, kwani kauli yake amesema itachukuliwa kwa uzito na kila mwananchi kutokana na mamlaka aliyonayo.
Amesema, Rais akitoa kauli hiyo, vitendo hivyo vitamalizika na kuwezesha jamii imara inayozingatia na kujali haki za binadamu na usawa wa kijinsia.
Ameyasema hayo leo Januari 7, 2021 wakati akizungumza na waandishi habari katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari kilichopo Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Ni wakati wa zoezi la kuvunja kambi kwa wasichana waliokuwa wakihifadhiwa kituoni hapo baada ya kukimbia kukeketwa katika msimu ulioanza mwezi Novemba 2020, ambapo koo mbalimbali kutoka kabila la Kikurya ikiwemo
Sehemu ya wasichana wa Nyumba Salama Kiabakari Butiama wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly (hayupo pichani).
Wanyabasi, Wakenye, Walinchoka na Wairegi zilikuwa zikikeketa kutokana na likizo ya mwezi Desemba na kupelekea wasichana wapya 166 kupewa hifadhi, huku kituo kikiwa na jumla ya wasichana 224.
Wasichana hao 166 wapya wameanza kurejeshewa makwao kuanzia Januari 7, 2021 kwa kushirikiana na Ofisi za Dawati la Jinsia,Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii ambapo wazazi wa watoto hao watajaza fomu maalumu za kutowakeketa mabinti zao.
Aidha,baadaye zoezi la kujenga mahusiano na wazazi litafanyika ili kuhakikisha kwamba wasichana hao hawakeketwi hata wakiwa makwao na mzazi atakayekiuka atawajibishwa kisheria na kwa watakaokataliwa shirika litachukua mzigo wa kuwasomesha na kuwahudumia kama ambavyo limekuwa likifanya kwa waliopo kituoni hapo.
Rhobi ameongeza kuwa, vitendo vya ukatili vimekuwa vikirudisha nyuma juhudi za Serikali katika nyanja za kimaendeleo pamoja na kukwamisha ndoto za watoto wa kike kufikia malengo yao, ambapo baadhi yao huozeshwa katika umri mdogo na kukatizwa masomo yao, huku wengine wakikeketwa kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.
"Tumekuwa na wasichana jumla 224 katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari, kati yao wapya ni 166 hawa walikimbia ukeketaji kutoka wilaya za Tarime, Butiama, Bunda na kwa upande wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu Wilaya ya Serengeti kuna wasichana 123.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly akizungumza wakati wa kuvunja kambi ya wasichana waliokuwa wamehifadhiwa Kituo Cha Nyumba Salama Kiabakari baada ya kukimbia ukeketaji kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Mara,wengine ni maafisa kutoka Dawati la Jinsia Kiabakari na Butiama waliokaa.
"Hawa 224 wakiwa kituoni wamepewa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia, elimu kulingana na masomo yao wanayosoma pamoja na elimu ya afya ya uzazi, natumaini kwamba watakuwa mabalozi wa kupinga ukatili waendako,"amesema.
Katika hatua nyingine, Rhobi ameiomba pia Serikali kuwachukulia hatua wazee wa kimila ambao waliahidi mbele ya serikali kutohamasisha ukeketaji, lakini jambo la kusikitisha na kushangaza wazee hao kwa msimu huu wa ukeketaji wao walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha vitendo hivyo hatua ambayo inafanya viendelee kuwepo.
"Serikali isiwafumbie macho wazee wa kimila, kama ambavyo imekuwa ikiwachukukia hatua wachochezi. Wazee wa kimila wapo ambao wamekuwa wakichochea vitendo hivi kuendelea kufanyika katika jamii, tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii katika mikutano ya hadhara, elimu ya ukatili shuleni.
"Na wazee wa kimila tumekuwa tukiwaelimisha kuachana na ukatili kwani nafasi yao ni kubwa katika kutokomeza, lakini bado tena wao msimu huu wamehimizwa ukeketaji,"amesema Rhobi.
Janeth Joseph ambaye ni mhitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi St.Magreth iliyopo Tarime na Angel Amos kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini ambaye pia ni mhitimu wa darasa la saba katika Shule ya
Msingi Muungano wakizungumza kwa nyakati tofauti na Diramakini kituoni hapo wamelishukuru Shirika la HGWT kwa kuwapa hifadhi kwa kipindi chote cha msimu wa ukeketaji pamoja na mahitaji yao yote sambamba na elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia, elimu ya afya na haki zao.
"Nitaenda kuwaelimisha wazazi wangu madhara ya ukeketaji na kuwaomba waachane na mila hii yenye madhara kwetu watoto wa kike, nilitoroka nyumbani kwani baba yangu na mama walitaka kunikeketa nikakimbilia kwa Mwenyekiti wa Kijiji ambaye alinisaidia kufika Nyumba Salama tofauti na hapo ningekeketwa.
"Maandalizi yote yalikuwa yamefanywa natumaini wazazi watanipokea na wakikataa nipo tayari kurudi Nyumba Salama kuishi kusudi tu nisikeketwe namuomba Rais Magufuli aingilie jambo hili, ndoto yangu ni kuwa Mwanasheria,"amesema Eva Elias mkazi wa Rorya katika mazungumzo na Diramakini.
Tags
Habari