Serikali imeahidi kuendelea kukiwezesha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kuhakikisha kuwa kinatimiza wajibu wake wa kuandaa wataalamu katika sekta ya Uchukuzi kwa maendeleo ya Taifa letu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mkuu wa Chuo NIT, Profesa Zacharia Mganilwa (kulia) akisoma hotuba wa wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam, katikati ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Msongwe Kasenyeka na kushoto ni Mwenyekiti wa baraza la uongozi chuoni hapo, Mhandisi Blasius Bavo Nyichomba.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (MB) wakati wa mahafali ya 36 ya chuo hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka nguvu kubwa katika kuendeleza Sekta ya Uchukuzi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Barabara, Reli ya Kisasa, Ujenzi wa Meli na Ununuzi wa Ndege.
“Kwa kutambua umuhimu Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 ukurasa wa 95 imeelekeza Serikali kuendelea kukiwezesha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ili kiendelee kuzalisha wataalam watakaotumika katika sekta ya usafirishaji,”amesema.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema kuwa amepokea hotuba ya Mkuu wa Chuo kuhusu utekelezaji wa shughuli za chuo na malengo makubwa ya miaka mitano ijayo.
“Idadi hii ya wahitimu ni ushahidi tosha wa juhudi kubwa za Chuo katika kusimamia taaluma na kuhakikisha wanafunzi wetu wanasoma katika mazingira mazuri,”amesema.
Hivyo, pamoja na juhudi hizi kubwa mnazofanya natoa wito kwa Uongozi wa Chuo kuendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ili kufanya Chuo chetu kuwa mahali salama zaidi na sahihi pa kujifunzia. Hii itawavutia zaidi wanafunzi wengi kujiunga na Chuo hiki, amebainisha.
Kwa upande wa wahitimu, Naibu Waziri huyo amewapongeza kwa jitihada walizofanya wakati wote wa masomo yao hadi kupata sifa ya kutunukiwa vyeti .
“Hongereni sana. Ninatambua kuwa tuzo hii mliyopata ni ya msingi kwenu katika safari ndefu ya kuwa wataalamu wazuri na mahiri,” amesema na kuongeza; “Ninaelewa kuwa mitaala mliyopitishwa imewatayarisha kwenda kufanya shughuli zenu kama askari wa miavuli”.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Msongee Kasekenya (katikati) akiwa katika maandamano wakati wa mahafali ga 36 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Chuo hicho jijini Dar es Salaam, Kulia kwake ni Mkuu wa Chuo NIT Profesa Zacharia Mganilwa na kushoto ni Mwenyechuokiti wa baraza la uongozi chuoni hapo, Mhandisi Blasius Bavo Nyichomba.
Ameongeza kuwa; “Ushauri wangu kwenu msiridhike na utaalamu huu mliopata, endeleeni kutafuta utaalamu wa juu zaidi ili taifa liwe na wataalamu wa kutosha kwenye Sekta ya Uchukuzi na wenye sifa zote zinazohitajika.”
Amewataka wanafunzi wanaoendelea na masomo kuwa wabunifu na kusoma kwa bidii ili wanapomaliza masomo yao waweze kuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha, kwani itakuwa ni rahisi kujiajiri au kuajiriwa ukizingatia uchumi wa viwanda unahitaji nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi zaidi.
Amewataka wafanyakazi wa Chuo kudumisha na kulinda jitihada katika kufikia malengo ya kuwapata wahitimu wengi zaidi.
“Wanataaluma ni kwamba, Chuo chetu kina majukumu matatu ambayo ni Kufundisha, kufanya tafiti na Kutoa ushauri wa Kitaalamu. Ongezeni juhudi katika kutekeleza majukumu hayo kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda,"amesema.
Amesema kuwa, amefarijika kusikia kwamba chuo kimeendelea kutanua wigo katika sekta hii muhimu ya usafirishaji, ikiwa ni pamoja na kujiamarisha katika njia zote za usafirishaji yaani usafiri wa ndege, usafiri kwa njia ya maji, reli na barabara.
“Kozi hizi ni muhimu sana kwa Taifa letu kwani zitapunguza mzigo kwa Serikali kwa kugharamia mafunzo haya nje ya nchi ambayo hutolewa kwa gharama kubwa pamoja na kuwa na wataalam wengi watakao saidia kutunza miundombinu ya usafirishaji,”amesema.
Naibu Waziri amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inafahamu vizuri changamoto zinazozikabili Chuo ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ya majengo, uhaba wa ofisi za wahadhiri na uhaba wa nafasi za mabweni kwa wanafunzi.
Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Chuo katika kuhakikisha changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi.
“Ninauagiza uongozi kuendelea kutumia mapato ya ndani katika kuendeleza na kuboresha miundombinu ya Chuo ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi za umma na binafsi zinazoweza kusaidia katika upatikanaji wa mabweni kwa wanafunzi,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho, Prof Blasius Bavo Nyichomba amesema kuwa ni dhahiri kuwa mafanikio ya wahitimu ni juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na ushirikiano wa wadau mbali mbali ambao ni wafadhili wa ndani na nje ya nchi na wazazi.
“Napenda kuwapongeza na kuwashukuru wote kwani bila ya juhudi zao tusingekuwa hapa kushuhudia wahitimu wakitunukiwa tuzo zao. Pia, napenda kuupongeza Uongozi wa Chuo, wanataaluma na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri waliofanya hadi kufanikisha mahafali haya,"amesema.
Amesema katika kutekeleza wajibu wa kusimamia Chuo, Baraza la Uongozi limefanikiwa kusimamia uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.
Amesema Serikali imeendelea kufanya mapinduzi anuai katika sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji ambapo kwa juhudi za uongozi wa Awamu ya Tano Nchi yetu imeingia kwenye uchumi wa kati kabla ya kufika 2025.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mapinduzi hayo yameongeza uhitaji mkubwa wa Rasilimali Watu yenye weledi wa hali ya juu nchini na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukifanya Chuo kubuni na kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko na kutoa wahitimu bora katika nyanja zote za Usafirishaji (Barabara, Reli, Anga, Majina Mabomba).
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuidhinisha Bajeti ya Utekelezaji wa miradi ya Chuo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
“Vilevile naishukuru Serikali kwa kutoa fursa kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kuanza kutekeleza Mradi wa Kituo cha Kikanda cha Umahiri cha Mafunzo ya Usalama Barabarani (Regional Center of Excellence for Road Safety – RCoERS) kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleoya Afrika (AfDB)” alisema.
Amedokeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kutatua changamotoya uhaba wa miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia ili kukiwezesha Chuo kutoa wataalamu mahiri katika usafirishaji.
Kuhusu wahitimu, Mwenyekiti huyo amesema kuwa Chuo kimefanikiwa kutimizawajibu wake kwao na kwa Taifa nzima.
Amewaasa kujiepusha na magonjwa mbalimbali ikiwemo ukimwi na kuwa mfano bora kwa jamii watakamo kuwa wakiishi. Awali Mkuu wa Chuo hicho, Prof Zacharia Mganilwa alisema kuwa sekta ndogo ya usafiri wa anga inakuwa kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka .
Hivyo chuo kimejipanga kuendelea kutoa mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya kwanza.
Amesema pia chuo kimeendelea kutoa kozi ya wahudumu wa ndani ya ndege ambapo hadi sasa imekwisha dahili mikupuo mitatu.
Pamoja na hayo,Mhandisi Prof Mganilwa amesema kuwa idadi ya wanafunzi chuoni hapo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hivyo kuongeza idadi wa taalamu katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
“Idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa miaka 7 kwa asilimia 258 kutoka wanafunzi 3,248 kwa mwaka wa masomo 2014/15 mpaka wanafunzi 11,640 mwaka 2020/2021.
“Kwasasa chuo kinawafanyakazi 327 ikiwa wanataaluma ni 206 na na waendeshaji 121. Idadi hii ya wanataaluma ni ndogo kulinganisha na uhitaji wake na hivyo Chuo kimekuwa kikitumia fedha nyingi kulipa waalimu wa muda. Hivyo tunaamini kwa mwaka huu wa fedha tunaweza kupata kibali cha kuajiri na hivyo kutatua tatizo hili,”amesema.
Tags
Makala