Serikali yatoa maagizo kwa waganga wakuu wote wa halmashauri

Waganga Wakuu wa Halmashauri zote nchini wamekumbushwa kujitathimini kuhusu uandikishaji wa wananchi kwenye Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF), anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Kanda ya Magharibi).
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Ntuli Kapologwe alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na timu za afya za halmashauri katika mikoa ya Singida, Tabora na Katavi wakati wa ziara ya kuhamasisha usimamizi shirikishi katika vituo vya kutolea huduma za afya. 

“Suala la wananchi kujiunga na CHF bado liko chini sana yaani hamfanyi vizuri kabisa katika eneo hili, pasipokuwepo na uwajibikaji wa pamoja na kujitoa kwa dhati ni vigumu sana kufanikiwa katika hili, wananchi wengi wanakosa huduma bora za afya kwa sababu tu hawajajiunga na bima hii,”amesema Dkt.Ntuli. 
Ameendelea kusema kuwa timu za uendeshaji zinapaswa kuweka mikakati ya kufikisha elimu kwa wananchi na kuwahamasisha kujiunga ili kupunguza gharama za papo kwa papo mara mtu anapougua. 

Gharama za kujiunga na Bima ya Afya ya Jamii ni nafuu sana na zimewekwa zikimlenga mwananchi wa kipato cha chini kabisa ili aweze kupata matibabu mara anapougua,"ameongeza Dkt.Ntuli. 
"Nataka kila Mganga Mkuu wa Halmashauri ajitathmini pamoja na timu yake ya Uendeshaji wa Huduma za Afya je? wameandikisha wananchi kwa kiwango gani katika eneo lake kujiunga na Bima ya Afya ya Jamii,"alisisitiza Dkt.Ntuli. 

Mikoa inayofanya vizuri kidogo ni pamoja na Dodoma na Morogoro lakini, mingi ni ile ambayo uandikishaji uko chini na hauridhishi. 
"Miaka ya nyuma Mkoa wa Singida ulikua unafanya vizuri, mpaka maeneo mengine walikua wanaenda kujifunza, lakini kwa sasa wameshuka na wako kwenye asilimia tano tu, ni wakati wa kujitathmini kwanini mmeshuka katika uandikishaji na mchukue hatua za makusudi kuhakikisha mnarudi kwenye kiwango chenu cha awali,"amesema Dkt. Ntuli. 

Ameongeza kuwa, kwa ujumla uandikishaji mpaka Kitaifa tumefikia jumla ya kaya 438,882 (sawa na asilimia 4.0) zenye watu 1,871,850 ambapo kwa mwaka huu wa 2021 tunataka tufikie asilimia 20 ya uandikishaji hivyo kila mmoja wetu akasimamie hili liweze kufikiwa. 
“Tuwaelimishe wananchi kuwa wanapojiunga wanafaidikia na mtandao mkubwa wa huduma za tiba katika vituo vyote vinavyomilikiwa na serikali na vya mashirika ya dini vyenye makubaliano ya kutoa huduma, kuanzia zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mikoa. 

"Mwanachama anapojiunga na Bima ya Afya ya Jamii atapata huduma katika vituo takribani 6,000 nchi nzima ikiwemo Zahanati 4,922, Vituo vya Afya 716, Hospitali za Wilaya 179 na Hospitali za Mikoa 28 na anatibiwa popote nchini bila kizuizi,"amebainisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news