Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis amewataka
wahitimu wa Vyuo Vikuu nchini wakiwemo wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini kutumia vizuri ujuzi walioupata kuleta ufumbuzi wa changamoto
za kimaendeleo zinazoikabili jamii pamoja na kutafuta ajira katika sekta
isiyo rasmi ili kujiletea maendeleo,wanaripoti Walace Ng’wandu na
Farida Ramadhani (WFM), Mwanza.


Hayo ameyasema wakati wa Mahafali ya 34 ya Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini yaliyo fanyika kwa mara ya 8 katika Kituo cha Kanda
ya Ziwa – Mwanza kwa Wahitimu wa Shahada na Stashahada na Astashahada.
Mhe.
Mwanaidi Khamis alisema kuwa hakuna shaka vyuo vinatoa elimu bora
ambayo kama ikizingatiwa kikamilifu inatoa fursa ya kujiajiri na
kuajiliwa, hivyo kuwa chachu ya maendeleo yatakayoleta tija katika
nyanja mbalimbali.


“Serikali itaendelea kuchukua hatua
mbalimbali katika kuweka mazingira mazuri ya kujiajiri hususani kwa
kuboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuongeza fursa za
vijana wasomi kujiajiri na hatimaye kupunguza tatizo la ajira,"amesema
Bi. Mwanaidi Khamis.
Amesema kuwa, baadhi ya hatua zilizokwisha
kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya utoaji
mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia
Mamlaka za Serikali za Mitaa, kupunguza riba ya mikopo ya mabenki pamoja
na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda ili kuongeza ajira na kuongeza
mnyororo wa thamani wa mazao yanayozalishwa nchini.



Naibu Waziri
huyo amewaasa vijana wasomi nchini kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi
na kuzitumia fursa mbalimbali zilizopo hususani katika sekta binafsi
kujipatia kipato na kuwa na mchango kwa taifa.
Aidha amekitaka
Chuo cha Maendeleo Vijijini kuyafanyia kazi maelekezo ya Mhe. Waziri wa
Fedha na Mipango, Mh. Dkt. Phillip Isdor Mpango aliyoyatoa Jijini Dodoma
tarehe 22 Desemba, 2020 alipokutana na Watendaji Wakuu wa Mashirika na
Taasisi za Umma ambapo alizielekeza Taasisi za Elimu ya Juu kutumia
vyema fursa zilizopo katika kuongeza mapato ya taasisi husika hususani
kwa kuimarisha vitengo vya Ushauri na Utafiti ili viweze kuchangia
angalau asilimia 10 ili kupunguza utegemezi katika Serikali Kuu.


Amesema kuwa, Chuo Cha Mipango kinatakiwa kuwa mfano kwa Taasisi
nyingine za Elimu ya Juu ikizingatiwa kuwa kipo chini ya Wizara ya Fedha
na Mipango.
Aidha, kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Martha
Qorro, alisema kuwa jukumu la taasisi za elimu ya juu hususani Chuo cha
Mipango ya Maendeleo Vijini ni kuendelea kuchapa kazi kwa bidii, maarifa
na weledi wa hali ya juu ilikutoa huduma zinazo tatua changamoto za
maendeleo katika jamii.
Amesema kuwa, Chuo cha Mipango wamewezesha kuendelea kutoa mchango kwa jamii kwa kuendesha na
kutekeleza miradi ya maendeleo yenye kuwakwamua wananchi wengi kiuchumi
hususani katika eneo la mifugo, uvuvi na kilimo.
Pia amemuahidi
Naibu Waziri Mhe. Mwanaidi Khamis kuwa Chuo kinaendelea kupata hati safi
ya ukaguzi ambayo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali kuanzisha
mifumo mbalimbali ya udhibiti, utunzaji, na usimamaizi mapato na
matumizi ya fedha za umma.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha
Mafunzo cha Kanda ya Ziwa -Mwanza Prof. Juvenal Nkonoki, alisema kuwa
idadi ya watunukiwa wa tuzo mbalimbali katika mahafali ya 34
yaliyofanyika kwa mara ya nane katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa
Mkoani Mwanza ni 2571 wakiwemo wanaume 1009 na wanawake 1562.
Tags
Habari