Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),
Justina Mashiba amesema mpaka sasa zaidi ya wananchi millioni 12 waishio
maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara pamoja na wale wa
mipakani na kanda maalum wamefikiwa na huduma mbalimbali za mawasiliano
ikiwemo simu, runinga, radio pamoja na mawasiliano ya posta,anaripoti
Celina Mwakabwale (UCSAF).
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba (kulia) akikabidhi taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko huo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile. Katikati aliyeshika vitabu hivyo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, Dodoma.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi wa pili kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi (wa kwanza kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote baada ya kikao chake na wajumbe hao, Dodoma.
Bi. Mashiba ameyasema hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile aliyetembelea tasisisi
hiyo na kufanya kikao na wajumbe wa bodi, menejimenti pamoja na
wafanyakazi. Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Zainab
Chaula, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Jim Yohazi pamoja na baadhi ya watendaji
wa Wizara hiyo.
Dkt.Ndugulile ameipongeza UCSAF kwa kufikisha
huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali nchini huku akiitaka
kuwekeza zaidi katika teknolojia yenye gharama nafuu ili kuyafikia kwa
haraka maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za mawasiliano. Hivi
sasa UCSAF inatumia shilingi milioni 350 kujenga mnara mmoja wa
mawasiliano.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa menejimenti ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote baada ya kikao chake na wajumbe hao, Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Justina Mashiba.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi wa pili kulia). (Wa pili kushoto) Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi (wa kwanza kushoto) wakiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Bi Justina Mashiba (wa kwanza kulia), Dodoma.
Ameongeza kwa kusema kuwa, sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya
habari inabadilika kwa kasi hivyo ameitaka wizara kukamilisha uandwaaji
wa sheria ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko hayo.
Akizungumza
na wajumbe wa bodi Dkt Ndugulile ameagiza kuwepo na utaratibu mzuri wa
kufanya kazi kwa ukaribu na kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya
mawasiliano Tanzania (TCRA) na UCSAF ili kuongeza kasi ya upelekaji wa
huduma mbalimbali za mawasiliano katika maeneo wanayoshirikiana.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi katikati) akifuatilia maelezo ya mjumbe wa bodi ya UCSAF (hayupo pichani). Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba, Dodoma.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula ameipongeza UCSAF huku akiitaka kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano ili kuendana na malengo ya kuanzishwa kwa wizara hiyo.
Hadi sasa mfuko wa mawasiliano kwa wote umefanikiwa kufikisha huduma mbalimbali za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuwasha minara katika kata 633 zenye vijiji 2,320, kuunganisha mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 711, kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 2,213 wa shule za UMMA kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na kujenga vituo 10 vya TEHAMA visiwani Zanzibar.