Wafanyabiashara Geita wataka usiri ukaguzi wa dhahabu ATCL

Wafanyabiashara wanaosafirisha madini ya dhahabu nje ya nchi kutoka Mkoa wa Geita wameomba Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuweka utaratibu mzuri wa kukagua madini hayo kwa njia ambayo siyo ya wazi ili kuwahakikishia usalama wao na madini yao,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wakubwa wa Dhahabu katika Soko Kuu la Dhahabu mjini Geita, Stumai Tumaini (katikati) akiwa na wafanyabiashara wengine katika kikao kilichoitishwa na ATCL katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Wamesema wanapofika kwenye viwanja vya ndege kusafiri kwenda nje ya nchi wakiwa na dhahabu wafanyakazi wa ATCL wanakagua mizigo yao hadharani kila mtu akiwa anaona jambo ambalo wamesema ni hatari kwa usalama.

Wafanyabiashara hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wakubwa (dealers) wa Dhahabu mkoa wa Geita, Stumai Tumaini wamesema hayo wakati wa kikao cha pamoja cha ATCL na wafanyabiashara mbalimbali wa Mkoa wa Geita kilichofanyika leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha Mjini Geita (EPZA).

ATCL imefanya kikao hicho kwa ajili ya kutambulisha huduma na bidhaa zake kwa wafanyabiashara hao baada ya kupanga kuzindua safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Geita ulioko wilayani Chato Januari 9, mwaka huu.

Wameomba Shirika la Ndege Tanzania kubadilisha utaratibu wa kukagua madini hayo hadharani na badala yake uwekwe utaratibu wa kufanya ukaguzi sehemu ambazo abiria wote hawawezi kuona ambacho mfanyabiashara huyo amebeba.
Meneja wa Biashara wa ATCL, Edward Nkwabi akifuatilia majadiliano kati ya wafanyabiashara wa Mkoa wa Geita na ATCL katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha mjini Geita (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Wamesema, kwa sasa mfanyabiashara analazimika kuweka dhahabu juu ya meza ili mfanyakazi wa shirika hilo azikague huku watu wote wanaokuwa kwenye jengo hilo hasa abiria wakiwa wanaona jambo ambalo wanaona siyo zuri kwa sababu wanakuwa bado wanaendelea na safari na dhahabu ni kitu chenye thamani kubwa.

Wamesema wanakaguliwa na mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato (TRA), Wizara ya Madini kwa kupima uzito na kuwapa kibali cha kusafirisha,lakini wanapofika dirisha la ATCL wanakaguliwa upya.

Mkurugenzi Mkuu wa ATC, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema, wanaenda kulifanyia kazi jambo hilo ili wafanyabiashara wa dhahabu nchini wawe wanakaguliwa sehemu ambayo watu wengine wasiohusika hawawezi kuona ili kumfanya anayesafirisha dhahabu awe na amani.

Amesema, kuhusu kupima uzito kwa mara ya pili baada ya mamlaka nyingine kuwa zimeshapima, ni utaratibu wa kawaida wa kupata uzito wa mzigo wote utakaosafirishwa kwa ndege na uwiano wa vitu vingine kama vile hesabu ya mafuta.

Mhandisi Matindi amesema, lengo lao ni kuja kusikiliza wafanyabiashara hao ili kupata ushauri wao ili waweze kuwapa huduma nzuri.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert (mwenye koti nyeupe),kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi pamoja na wafanyabiashara wa Mkoa wa Geita baada ya kikao cha pamoja leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika kituo cha uwekezaji cha mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Amesema, mahitaji yao ya kuwakaguliwa sehemu maalum wameipokea na wataifanyia kazi haraka.

Mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema, wameanza safari za kwenda Geita baada ya kujiridhisha na uwezekano mkubwa wa kufanya biashara na wafanyabiashara wengi wa dhahabu.

Meneja wa Biashara wa Shirika hilo, Edward Nkwabi amesema kuw,a utafiti walioufanya ulionyesha mkoa wa Geita una uchumi mkubwa wa madini hivyo usafiri wa anga unahitajika sana.

Ameongeza kuwa, hata mkoa huo mahali ulipo unachochea kupata abiria wa ndege kwa mfano Geita iko mbali na uwanja wa ndege Mwanza,kulinganisha na Chato hivyo kiusalama ni vizuri kutumia uwanja wa ndege wa Geita hasa kwa kusafirisha dhahabu.

Amesema, kwa sasa ATCL inamilki asilimia 71 ya soko la usafiri wa anga Tanzania na itaanza safari za Dar es salaam kwenda Chato na baada Mwanza na kurudi Dar es salaam tarehe 9 Januari, mwaka huu kwa ratiba ya siku ya Jumatatu na Jumamosi.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema Mkoa umejipanga kiusalama kwa mfanyabiashara yeyote anayetaka kusafirisha dhahabu atapewa ulinzi wa uhakika.

Aidha, amewataka wafanyabiashara biashara wa mkoa huo kuchukua fursa za kibiashara kama kusafirisha abiria na kutoa huduma ya chakula.

Shirika la Ndege Tanzania linatarajia kuanza safari za ndege kutoa uwanja wa ndege wa Geita uliopo wilayani Chato kuanzia Januari 9, mwaka huu baada ya kupata ruhusa kutoka mamlaka ya viwanja vya ndege nchini na mamlaka ya anga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news