Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameagiza maafisa kilimo mkoani Shinyanga kutoa elimu ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima wa zao la choroko ili waache tabia ya kuuza mazao yakiwa bado kuepuka kuwanufaisha wanunuzi badala ya wakulima ambao wanatumia nguvu nyingi kuandaa mazao hayo,anaripoti Anthony Ishengoma, Shinyanga.
Kiongozi huyo wa mkoa amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha siku moja kilichowakutanisha wadau wa zao la choroko mkoani Shinyanga ili kujadili namna bora ya matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kuhakikisha unaleta tija kwa wakulima wa zao hilo na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab. Telack akiongea na wadau wa zao la choroko katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Aidha,Telack ameongeza kuwa, kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani itawezesha wanunuzi wa zao la choroko kujua sehemu sahihi ya kupata zao hili likiwa katika ubora na kuepuka kuibiwa fedha zao na matepeli.
Telack ameongeza kuwa, ni agizo la serikali kuhakikisha mazao ya aina ya kunde yanatumia mfumo stakabadhi ghalani kama ilivyo kwa zao la korosho na sasa Shinyanga kwa kuanzia inaanza na zao la choroko na baadae itahamishia nguvu zake kwenye zao la dengu na mpunga lengo likiwa kuahakikisha wakulima wa mazao haya wanapata faida ya jasho lao na kujiletea maendeleo.
"Nataka kuona wakulima mkoani Shinyanga wakiwa na uwezo wa kusomesha watoto, kujenga nyumba bora na kufaidika na jasho lao sio mkulima analima mpunga katika maji mengi, lakini mnunuzi ananunua mpunga bado ukiwa shambani na kuvuna gunia sitini kwa kumlagai mkulima kwa kumpatia bodaboda,"amesema Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga Bi. Hilda Simon akiongea na wadau wa zao la choroko katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Aidha, Telack amemwagiza Kaimu Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Simon kukutana na viongozi wa vyama vya msingi na cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) kuweka mikakati ya pamoja ya kutoa elimu kwa wakulima ili wajue faida za kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Naye Kaimu Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Simon amesema kuwa, changamoto ya kushindwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani inapelekea kushindwa kuwa na takwimu sahihi za zao hilo, kuendelea kuwepo kwa utoaji vibali holela vilivyokuwa vikitolewa na halmashauri bila kupitia vyama vya msingi.
Hilda ameongeza kuwa, vibali hivyo vilikuwa vikitolewa kwa wanunuzi wa kati ambao kimsingi ndio wapinzani wa mfumo wa stakabadhi ghalani na hivyo kuendelea kumyonya mkulima kwa kununuoa choroko kwa bei za chini akitaja pia changamoto ya wakulima kukosa uvumilivu wa kusubili malipo kuwa ni sababu pia ya kushindwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Wadau wa zao la choroko Mkoa wa Shinyanga wakisimama kumpokea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amewaeleza wadau wa kikao hicho kuwa viongozi wa vyama msingi mkoani humo ni tatizo sana kwa kuwa hawajui uchungu wa wakulima kwani hawana hata shamba moja kazi yao imekuwa ni kuongea maneno maneno tu nakuwataka wakulima kuchagua viongozi ambao pia wana mashamba ya zao hilo.
Suala la Mfumo wa Stakabadhi Shambani sio jipya lakini kumekuwepo changamoto mbalimbali za utekelezaji wa mfumo huo ndio maana mkoa unajipanga upya kuhakikisha unaondoa changamoto zilizopo na kutafuta namna bora ya uendeshaji mfumo huo kwa kushirikisha wadau wa zao hilo.