Waziri Mkuu aongoza maziko ya Mbunge Martha Jachi Umbullah

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaasa Watanzania kuyaenzi yale yote mazuri aliyoyafanya na kuyatekeleza kwa bidii na uaminifu mkubwa marehemu Martha Jachi Umbullah wakati wa uhai wake, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbulla yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Dongombeshi wilayani Mbulu, Januari 26, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Majaliwa ameyasema hayo leo Januari 26, 2021 wakati akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya misa ya marehemu Umbullah iliyoendeshwa na Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mbulu, John Nade ya kumsindikiza katika nyumba yake ya milele nyumbani kwake Dongobesh wilayani Mbulu mkoani Manyara.

Amesema, maisha ya Martha Umbulllah yawakumbushe wananchi namna sahihi ya kuishi na jamii, kwani wakati wote wa uhai wake Martha Umbulllah alikuwa akichapa kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa hali iliyomjengea umaarufu wa kupangwa katika kamati ya bajeti ya kuishauri serikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole , John Umbulla, Mume wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbulla katika mazishi ya Mbunge huyo yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Dongobeshi wilayni Mbulu, Janauri 26, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbulla katika mazishi yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Dongombeshi wilayani Mbulu, Januari 26, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

"Hakika hata kuja hapa mbele kuzungumza, tunakuja tu kwa kuwa inabidi, lakini ukifikiria mwenzetu yupo hapa amepumzika hata unakosa ujasiri, lakini kikubwa ni kuyaenzi yale yote aliyotuanchia Martha Umbulllah wakati wa uhai wake, hivyo nawapa pole nyingi wafiwa Mzee Umbulllah pamoja na watoto, Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na Dada yetu,mpendwa wetu Martha Umbullah,"amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Naye Naibu Spika Tulia Ackson amesema, wabunge wa Jamhuri ya Muungano walikua wakijivunia uwepo wa marehemu Martha Umbullah kwani wabunge wengi walikua wajipata ushauri mbalimbali kutoka kwa Martha Umbullah, hivyo kukosekana kwake bungeni ni pengo kubwa sana.

Amesema, Martha Umbullah alikuwa mtu wa aina yake, alikuwa kipenzi kikubwa kwa wabunge, jamii na wana Manyara kiujumla hususani akina mama, ambako alikuwa akipata kura nyingi kutoka huko ambazo zilimuweka madarakani kwa takribani vipindi vinne.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitupa udongo kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbulla katika mazishi yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Dongombeshi wilayani Mbulu, Januari 26, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbulla, nyumbani kwa Marehemu katika kijiji cha Dongobeshi wilayani Mbulu, Januari 26, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

"Sijui kama wana Manyara mnafahamu kama mlikuwa na mtu muhimu kiasi gani kwenu, Martha alikuwa ni mtu mwenye kupenda na kuwajali kimaendeleo wananchi wake hususani akina mama, na ndio maana kila kipindi alipokuwa akigombea alikua akipita kwa kishindo kweli kweli, hivyo ni vema tuendelee kuyakumbuka na kuyaenzi yote aliyotuchia, hata kwenye michango ya rambirambi wabunge huwa si rahisi sana kupokea na kukubali kutoa michango kirahisi rahisi kama mnavyofikiria, lakini kwa kukumbuka yale yote aliyokuwa akiyafanya Martha Umbullah wakati wa uhai wake na kumuheshimu ndio maana wameweza kuchangia kiasi kikubwa,"amesema Naibu spika.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT Taifa), Gaudensia Kabaka amesema, Martha Umbullah kwa kuwajali na kuthamini akina mama, alaanzisha mfuko wa kuwasaidia akina mama wa mkoa wa Manyara, mfuko ambao umewezesha kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wanawake wa Manyara.

"Huo mfuko aliouanzisha mpendwa wetu naomba usimamiwe kikamilifu ili uendelee kuongeza utoaji wa huduma, kwa kufanya hivyo utasaidia kuyaenzi aliyoyaanzisha mpendwa wetu wakati wa uhai wake na hivyo kuwa faraja kwa familia na jamii kiujumla, hata huu umati uliofika hapa kumsindikiza katika safari yake ya mwisho ni ishara tosha kuwa marehemu Marha Umbullah alikuwa akiishi na jamii vizuri kama ambavyo kila mmoja wetu anashuhudia,"amesema Mwenyekiti huyo.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge mkoani Manyara, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Paulina Gekul amesema Martha Umbullah alikuwa ni mbunge wa aina ya pekee huku akisema alikuwa akipenda kumuona kila mtu anaendelea kimaisha.

Gekul amesema, Martha Umbullah alikua ni mtu wa kimbilio la kila mtu kwa ajili ya kupata Ushauri mbalimbali, huku akisema hata wakati alipokua akigombea ubunge alikua ni mtu wa kuwatia moyo aliyewahi kugombea nao kwa kusema hiyo ni nafasi ya watu wrote,hivyo kila mmoja ajaribu bahati yake.

Kwa upande wa mume wa marehemu Martha Umbullah,Jachi Umbullah ameishukuru serikali kwa kujitoa katika majukumu mbalimbali hadi katika kumsindikiza safari yake ya mwisho, kwani wamefarijika kuona uwepo wao.

Pia ameongeza kuwa kuwashukuru wananchi mbalimbali waliotoka ndani na nje ya mkoa huo kwa kuwafariji katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mke wake Martha Umbullah.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news