Waziri Ndumbaro awataka waliovamia maeneo ya hifadhi kuondoka wenyewe

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro Januari 1, 2021 ameongoza doria ya kuangalia hali ya uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Pori la Akiba la Gesimasowe pamoja na Litumbandosi na kutoa agizo kwa wavamizi walioanzisha shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo kinyume cha Sheria waanze kuondoka wenyewe, anaripoti Lusungu Helela (WMU).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Songea mara baada ya kufanya doria katika maeneo ya Hifadhi ambapo wameshuhudia baadhi ya maeneo yanaendeshwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.

Doria hiyo iliyofanyika kwa kutumia ndege ndogo mali ya Shirika la Hifadhi za Taifa ( TANAPA) imeshuhudia uharibifu mkubwa unaotokana na shughuli za kibindamu.

Katika doria hiyo Dkt.Ndumbaro amejionea makundi makubwa ya mifugo pamoja nyumba za kudumu zilizojengwa ndani ya maeneo ya hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika Uwanja wa Ndege wa Songea kabla ya kuanza safari ya kufanya doria ya kutembelea maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kujionea shughuli za uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba ya Gesimasowe na Litumbandosi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akisalimiana na watumishi wa Jeshi la Uhifadhi nchini katika uwanja wa ndege wa Songea kabla ya kuanza doria kwa kutumia ndege kujionea hali ya uhifadhi katika maeneo yaliyovamiwa na shughuli za kibinadamu.

Akizungumza mara baada ya doria hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amewataka wafugaji na wakulima nchi nzima ambao wanaendesha shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hifadhi waanze kuondoka wenyewe kabla operesheni ya kuwaondoa haijaanza.

"Kama mnanisikia anzeni kuondoka wenyewe kabla hatujawabaini, tutakamata mifugo na mtalipa gharama zote za kuharibu mazingira,"amesisitiza Dkt.Ndumbaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza na Kamishna Msaidizi Mhifadhi wa Kanda ya Kusini, Henock Msocha wakati wakielekea kupanda ndege kwa ajili ya kuanza kufanya doria katika maeneo ya hifadhi ambayo yamevamiwa na shughuli za kibinadamu katika Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Amesema, kwa mujibu wa sheria maeneo hayo yametengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi pekee na yeyote anayetaka kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo anarudisha nyuma juhudi za uhifadhi nchini.

"Katika kipindi changu cha uongozi sitakubali kuona uhifadhi unachezewa kwa sababu maeneo haya ni kichocheo cha Uchumi wa Taifa letu kupitia shughuli za utalii ikiwemo utalii wa picha na uwindaji wa kitalii ambapo kupitia utalii nchi imekuwa ikipata fedha nyingi,"amesema Dkt. Ndumbaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akiteremka kwenye ndege katika uwanja wa ndege wa Songea mkoani Ruvuma mara baada ya kuongoza kufanyika kwa doria katika maeneo ya Hifadhi ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Pori akiba la Gesimasowe pamoja na Litumbandosi, ambapo katika doria hiyo ameshuhudia makundi makubwa ya mifugo pamoja na nyumba za kudumu zilizojengwa ndani ya hifadhi hizo.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameziagiza taasisi za uhifadhi nchini zikamate mifugo itakayokutwa hifadhini bila kujali mifugo hiyo inamilikiwa na nani

"Nawaagize hata mkiikuta mifugo yangu, ninyi kamateni, msiogope kamateni tu,"amesisitiza Dkt. Ndumbaro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news