Katika hatua ya kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na umoja msafara wa Yanga SC umefanya ziara ya kumtembelea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman ofisini kwake Ikulu ya Vuga iliyopo Unguja jijini Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Licha ya mazungumzo ya kina juu ya namna ya kutumia vipaji vyao kwa ajili ya kuwaunganisha Watanzania, kukuza ajira na kuibua vipaji, pia msafara huo ulimpatia Makamu wa Rais wa Pili zawadi ya jezi.
Awali Yanga SC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi walilazimishwa suluhu dhidi ya timu iliyoshuka daraja Zanzibar ya Jamhuri FC ya Pemba katika mechi yao ya kwanza ya michuano ya kombe hilo kwa mwaka 2021.
Kwa sasa klabu hiyo ina matumaini makubwa zaidi katika kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara kutokana na namna ambavyo imeendelea kushikilia nafasi ya juu huku ikiwa na matokeo mazuri katika msimamo wa ligi hiyo.