Wanajwangwani, Yanga SC wamefanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa penalti 4-3 , anaripoti Mwandishi Diramakini.
Ushindi huo ni kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 usiku wa Januari 13, 2021 katika dimba la Amaan,Unguja jijini Zanzibar.
Shujaa wa Yanga SC kwenye mchezo wa leo ambao mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibara na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ni kipa Farouk Shikaro aliyeokoa penalti ya mwisho ya Simba SC iliyopigwa na beki Joash Onyango.
Aidha, penalti za Yanga SC zimefungwa na Tuisila Kisinda, Abdallah Shaibu (Ninja), Zawadi Mauya na Said Ntibanzokiza huku ya Mukoko Tonombe iliokolewa na kipa Beno Kakolanya wa Simba SC.
Aidha, penalti za Simba SC zimefungwa na kiungo Francis Kahata, mshambuliaji Chriss Mugalu na beki mzawa Gardiel Michael, wakati mshambuliaji, Meddie Kagere na Nahodha wa amegongesha mwamba wa juu kulia.
Dakika 90 za mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nasor aliyesaidiwa na Mustafa Khamisi Hasira na Ali Ahmada Mbwana pembezoni mwa Uwanja, mezani Issa Haji Vuai na Kamisaa Muhidini Kamara zilikuwa za kusisimua zaidi.
Kwa ushindi huu, hii inakuwa mara ya pili kwa Yanga SC kutwaa Kombe la Mapinduzi baada ya mwaka 2007 , mashindano hayo yalipofanyika kwa mara ya kwanza na wakaifunga Mtibwa Sugar kwenye fainali.
Hii ndiyo orodha ya Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi tangu 2007 hadi 2021
Mwaka Bingwa Mshindi wa Pili
2007 Yanga SC Mtibwa Sugar
2008 Simba SC Mtibwa Sugar
2009 Miembeni KMKM
2010 Mtibwa Sugar Ocean View
2011 Simba SC Yanga SC
2012 Azam FC Simba SC
2013 Azam FC Tusker FC
2014 KCCA Simba SC
2015 Simba SC Mtibwa Sugar
2016 URA Mtibwa Sugar
2017 Azam FC Simba SC
2018 Azam FC URA FC
2019 Azam FC Simba SC 2-1
2020 Mtibwa Sugar Simba SC 1-0
2021 Yanga SC Simba SC 4-3
Pia inakuwa mara ya kwanza kuwafunga watani wao hao wa jadi kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mara mbili awali kati ya Januari 10, 2017 kwenye Nusu Fainali kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 na Januari 12, mwaka 2011 kwenye Fainali ilipochapwa 2-0, mabao ya Mussa Hassan Mgosi na Shijja Mkinna.
Nyota watatu wa Simba SC walijinyakulia tuzo baada ya mchezo huo, beki Joash Onyango Mchezaji Bora wa Mechi, Kiungo Francis Kahata Mchezaji wa Bora wa Mashindano na Mshambuliaji Miraj Athumani Mfungaji Bora kwa mabao yake manne.
Kipa Farouk Shikaro wa Yanga amejinyakulia tuzo ya Kipa Bora kufuatia kuruhusu bao moja tu kwenye mashindano hayo yalioanza mapema mwezi huu huku Sherehe rasmi za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zikiwa zimefanyika Januari 12, 2021.
Mwaka huu, sherehe hizo hazikuwa na shamrashamra kama ilivyokawaida, ikiwa ni baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuagiza fedha zitumike katika shughuli za maendeleo.
Tags
Michezo