Afrika kusambaziwa chanjo milioni 90 za Corona mwezi huu

Chanjo milioni 90 za ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) zitaanza kusambazwa barani Afrika mwezi huu katika kile ambacho kinaelezwa kuwa kitakuwa kampeni kubwa zaidi ya chanjo barani Afrika.

Hayo ni kwa mujibu wa mfumo wa kusambaza chanjo za COVID-19, COVAX ulioundwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Chanjo hiyo aina ya AstraZeneca/Oxford AZD1222 imeorodheshwa kwa matumizi ya dharura na WHO ambapo shirika hilo sasa linatathmini chanjo hiyo na matokeo yatatangazwa karibuni.

“Afrika imeshuhudia maeneo mengine yakianza utoaji wa chanjo ya COVID-19, yenyewe ikiwa kando. Mpango huu wa kupeleka chanjo ni hatua ya kwanza muhimu katika kuhakiisha kuwa bara hilo linapata fursa sawa ya chanjo kama maeneo mengine,”amesema Dkt.Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika akizungumza katika mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao huku akiongeza kuwa, “tunatambua kuwa hakuna aliye salama hadi pale kila mtu atakuwa salama.”

COVAX kupitia barua yaka ya Januari 30, mwaka huu ilijulisha nchi za Afrika kuhusu mpango huo wa upelekaji chanjo.

Kutokana na kiwango kikubwa cha mahitaji ya chanjo ya COVID-19, shehena za mwisho zitategemea kiwango cha uzalishaji kutoka kwa kampuni husika na utayari wa nchi kupokea chanjo hizo.

Nchi zinazopokea chanjo hizo zinatakiwa kuwasilisha mipango yao ya mwisho ya usambazaji na utoaji wa chanjo hiyo kutoka COVAX.

Chanjo dhidi ya COVID-19 iliyotengenezwa na Pfizer-BioNTech ni ya kwanza kuidhinishwa na baadhi ya nchi na inahitaji kuhifadhiwa ubaridi wa 70°C.

Kando mwa chanjo hiyo ya sasa, dozi 320,000 za chanjo aina ya Pfizer-BioNTech zimepangwa kwa mataifa manne ya Afrika ambayo ni Cabo Verde, Rwanda, Afrika Kusini na Tunisia.

Chanjo hii ilipokelewa na WHO na kuorodheshwa kwa mahitaji ya dharura, lakini inahitaji nchi kuwa na uwezo wa kuhifadhi na kusambaza katika kiwango cha nyuzi joto 70 chini ya sifuri katika kipimo cha selsiyasi.

Katika kuwasilisha ombi la chanjo hiyo ya Pfizer, nchi zilitakiwa kuwasilisha maombi ambapo nchi 13 ziliwasilisha na maombi yao kufanyiwa tathmini ikiwemo kiwango cha sasa cha vifo kutokana na COVID-19 na uwezo wa kuhifadhi chanjo chanjo hizo katika joto la -70°C.

Dkt.Moeti alisema, kwa tangazo hili, nchi zinapata fursa ya kujiandaa na kukamilisha mipango yao ya utoaji wa chanjo hiyo ikiwemo kuwa na mifumo sahihi ya majokofu ya kuhifadhi chanjo. “Hatuwezi kukubali kuharibika hata kwa dozi moja ya chanjo.”

Awamu ya kwanza ya dozi milioni 90 itasaidia nchi hizo katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kutoa chanjo kwa asilimia 3 ya wale walio hatarini zaidi wakiwemo wahudumu wa afya na makundi mengine yaliyo hatarini.

Katika kuunga mkono juhudi za COVAX, Muungano wa Afrika (AU), umepata dozi milioni 670 za chanjo ya COVID-19 ambazo zitasambazwa mwaka huu wa 2021 na 2022 kwa kuwa nchi zimepata fedha.

Benki ya African Export-Import itawezesha malipo kwa kupatia watengenezaji malipo ya awali ya dola bilioni 2 kwa niaba ya nchi husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news