BITEKO: RAIS MAGUFULI ANATAMANI KUONA KIWANDA CHA KUSAFISHA MADINI KINAANZA KAZI

Imeelezwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatamani kuona kiwanda cha kusafisha madini cha Mwanza Precious Metals Refinery Ltd kinachoendelea na ujenzi wa kusimika mitambo ya kusafisha madini jijini Mwanza kinaanza kazi,anaripoti Tito Mselem (WM) Mwanza.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho.

Waziri Biteko amesema baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho, Tanzania kama nchi itapata faida nyingi ikiwemo ajira kwa watanzania, kukua kwa teknolojia nchini, kuongezeka kwa mapato ya Serikali, pia nchi kupitia Benki Kuu ya Tanzania itapata akiba ya dhahabu na Watanzania watashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa madini.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwa kwenye kikao cha Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kilichofanyika katika ukumbi wa Mwauasa uliopo jijini Mwanza

“Nchi nzima inakiangalia hiki kiwanda wakiwemo wachimbaji wadogo ambao watapata soko la uhakika kwa madini yao na kwa bei ya soko la dunia kwa siku husika na pia watapata madini mengine yaliyochanganyikana na madini yao, hivyo hakikisheni mnamaliza kusimika mitambo kwa muda ili kiwanda kianze kufanya kazi na kuleta faida kwa wana mwanza na watanzania kwa ujumla,” alisema Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteko amewataka STAMICO kuwatendea haki wabia wao na kuhakikisha wanawashirikisha kila jambo ambapo amewapongeza wabia hao kwa kutoa mitaji yao na kuamua kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Aidha, baada ya Waziri Biteko kutembelea kiwanda hicho, alipata fursa ya kuzungumza na bodi ya STAMICO ambapo ameipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya mpaka kupelekea Wizara ya Madini kupata heshima kubwa kupitia Shirika hilo ambalo kwa sasa linajiendesha kwa faida.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema, ili Shirika la Madini la Taifa liondokane na changamoto ya wafanyakazi, Shirika halina budi kuajiri wafanyakazi wa mikataba ambao watakuwa wa muda mfupi ambao wataangaliwa utendaji wao wa kazi kama ni nzuri waongezewe na kama ni mbovu mkataba usitishwe.

Pia Prof. Msanjila, amesema Wizara ya Madini imeshapeleka ombi la kupatiwa fungu la kununua mashine ya kuchoronga miamba ambapo mpaka sasa hivi lipo katika hatua za mwisho ili wapatiwe fungu hilo kutoka Wizara ya Fedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji STAMICO Dkt. Venance Mwase amesema, utegemezi wa STAMICO wa fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake umepungua kutoka asilimia 73.8 kwa mwaka wa fedha 2015/16 hadi asilimia 32.5 kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Aidha, Dkt. Mwase amesema kuwa, Shirika limeongeza bajeti ya makadirio ya kiasi cha mapato yake yanayotokana na vyanzo vyake vya ndani ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 makadirio ya mapato ya ndani ni shilingi bilioni 45.2 ukilinganisha na shilingi bilioni 19.4 za mwaka wa fedha 2020/21.

“Lengo kuu la mtambo huu ni kuongeza thamani ya madini ya dhahabu yanayochimbwa nchini kabla ya kusafirishwa, pia mradi huu utaongeza mapato kwa nchi kupitia mlabaha na kodi mbalimbali pamoja na kutoa ajira mbalimbali kwa watanzania,” amesema Dkt. Mwase.
aadhi ya wajumbe walioshiriki kikao cha bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika ukumbi wa Mwauasa uliopo jijini Mwanza.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia), katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela, na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila wakiwa kwenye kiwanda cha kusafisha madini cha Mwanza Precious Metals Refinery Ltd kilichopo jijini Mwanza wakati wakipewa ufafanuzi. (Picha na WM).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news