Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Februari 20, 2021 imeendelea na zoezi la utoaji mafunzo ya siku saba kuhusu upataji wa leseni ya biashara kwa njia ya mtandao kwa wafanyabiashara wa mifungo waliopo Pugu mnadani jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Afisa Tehama Msaidizi, Bw. Hillary Mwenda kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni -BRELA akimkabidhi Leseni ya Biashara kundi A, Bw. Adamu Ladislaus Kalya mara baada ya usajili wa papo kwa hapo katika mafunzo ya Uwezeshaji wa Upatikanaji wa Leseni za Biashara kundi A kwa njia ya mtandao katika Mnada wa Mifugo Pugu jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia juu ya dhumuni la mafunzo hayo, Afisa Biashara wa BRELA, Bw. Peter Riwa amesema lengo la kuu la kushiriki katika mafunzo hayo ni kutoa elimu na hamasa kwa wafanyabishara.
"Dhumuni kuu ni kuwafikia wadau wetu na kuwapa elimu juu ya huduma tunazotoa, kuwahamasisha wadau juu ya leseni za Biashara, kuwasogezea huduma karibu na kutatua changamoto za wadau wetu papo kwa hapo pindi wanapopatiwa elimu,"amesema.
"Aidha zoezi hili ni moja ya mkakati wa kuondoa na kupunguza urasimu wa uwepo wa watu wa kati (VISHOKA) wanaokwamisha taratibu za upatikanaji wa Leseni kwa wafanyabishara,"ameeleza Bw. Riwa.
Naye Mkuu wa mnada Bw. Kerambo B. Samwel alieleza baadhi ya changamoto wanazopitia lakini pia kupongeza juhudi za BRELA.
Afisa Tehama Msaidizi Bw. Hillary Mwenda kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni -BRELA akimkabidhi Leseni ya Biashara kundi A Bw. Gilbert Mkamba Chizua mara baada ya Usajili wa papo kwa hapo katika mafunzo ya Uwezeshaji wa Upatikanaji wa Leseni za Biashara kundi A kwa njia ya mtandao katika Mnada wa Mifugo Pugu jijini Dar es Salaam.
"Changamoto ambazo wafanyabiashara wanakumbana nazo ni pamoja na Leseni moja ya Biashara kutumika na zaidi ya mtu mmoja, na kutokuwepo kwa elimu ya kutosha kuhusu upatikanaji wa Leseni, pia kushindwa kufuatilia Leseni kutokana na kuogopa makadirio ya kodi na hivyo kuwapelekea kushindwa kupata Leseni za Biashara.
"Nimefurahi kuwaona BRELA kwa kuja hapa na nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya,"amesema Bw. Samwel.
Mafunzo ya upataji wa Leseni za Biashara kwa njia ya mtandao yalianza Februari 18, 2021 na yanatarajia kufikia tamati Februari 24, 2021.