Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), mkoani Mwanza umedhamiria kuunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana kupitia ujenzi wa Daraja la Mwasongwe lililopo Mto Nyashishi ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za usafiri na usafirishaji kwa urahisi,anaripoti Erick Mwanakulya (TARURA) Mwanza.
Muonekano wa Ujenzi wa Daraja la Mwasonge lenye urefu wa Meta 60 lililopo katika barabara ya Kaluluma-Mwasonge-Nyashishi ukiwa umefikia asilimia 65 kukamilika. Daraja hili linaunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Muonekano wa Barabara ya mawe ya Isamilo–Nyashana–Nyamuge yenye urefu wa Km 3.28 iliyopo Kata ya Isamilo katika Halmashauri ya Wilaya Nyamagana mkoani Mwanza.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mhandisi Alzabron Kayungi katika mahojiano maalum kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Daraja hilo lililopo katika Barabara ya Kaluluma–Mwasonge–Nyashishi yenye urefu wa Km 7 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, na Barabara ya Buhongwa–Mwasongwe yenye urefu wa Km 4 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana.
“Daraja hili la Mwasonge lililopo Mto Nyashishi lina urefu wa Meta 60 na limefikia asilimia 65 kukamilika na litagharimu shilingi Bilioni 1.78, Daraja hili linaunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na litakamilika mwanzoni wa mwezi Mei mwaka 2021”, alisema Mhandisi Kayungi.
Mhandisi Kayungi ameongeza kuwa kuwa Wakazi wa Kijiji cha Mwasongwe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi wanategemea daraja hilo ili kupata mahitaji yao kama mahitaji kama shule, hospitali na huduma nyingine za kijamii, huku Wakazi wa Nyamagana wanategemea malighafi za ujenzi kama Mawe, Mchanga, Kokoto kutoka katika Kijiji cha Mwasongwe hivyo uwepo wa daraja hilo litasaidia wananchi kufanya shughuli zao za kila siku kwa urahisi.
Ndugu Msani Said Faida Mkazi wa Kigongo Ferry, ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa Ujenzi wa Daraja hilo kwani litawasaidia kufanikisha kupata huduma zao za kijamii kama shule, hospitali pamoja na huduma ya masoko katika Soko la Buhongwa.
Muonekano wa Daraja la miti la Mwasonge lililopo Mto Nyashishi ambalo linatumiwa na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Amesema kuwa daraja lililopo kwa sasa ni la miti ambalo pia ni hatarishi kwa usalama wao katika kusafirisha bidhaa, pia katika kipindi cha masika wanatumia mtumbwi kuvuka ambapo si salama hali inayopelekea kukwamisha shughuli zao na kusababisha kuzunguka umbali mrefu kwa kupitia usagara ili kuweza kuzifikia huduma mbalimbali.
“Naishukuru sana Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kwa ujenzi wa Daraja hili la Mwasongwe na kutusaidia kufika Buhongwa kwa urahisi, tulikuwa tunateseka katika uvukaji kwa kutumia Daraja hili la Miti na kipindi cha masika tulikuwa tunatumia Mitumbwi kuvuka ambapo haikuwa salama kwetu”, alisema Bw. Msani Faida.
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana Mhandisi Mohamed Muanda amesema kuwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana wapo katika ujenzi wa Daraja la Fumagila lenye urefu wa Meta 30, lililopo katika Mto Nyashishi Kata ya Kishiri linalounganisha Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana, Halmashauri ya Wilaya Misungwi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95 na kugharimu shilingi Milioni 552 mpaka kukamilika kwake.
Muonekano wa Ujenzi wa Daraja la Mwasonge lenye urefu wa Meta 60 lililopo katika barabara ya Kaluluma-Mwasonge-Nyashishi ukiwa umefikia asilimia 65 kukamilika. Daraja hili linaunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
“Daraja hili la Fumagila lililopo katika Mto Nyashishi katika barabara ya Kishiri – Fumagila limefikia asilimia 95 na ni muhimu kwa wakazi wa maeneo haya kwani kipindi cha masika ilikuwa tabu kuvuka, pia wakazi wa Magu, Misungwi wanategemea kupata huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana Kata ya Kishiri, daraja hili ni mkombozi kwa wakazi wa maeneo haya kwa kuwa wanategemeana sana”, alisema Mhandisi Muanda.
Aidha, mbali na ujenzi wa Daraja la Fumagila na Mwasongwe Mratibu wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Gaston Gasana amesema kuwa kwa kutumia malighafi za ujenzi kama mawe zilizopo kwa wingi mkoani Mwanza wameweza kujenga Barabara za Mawe maeneo ya milimani zenye urefu wa Km 11 kwa gharama nafuu.
Muonekano wa Barabara ya mawe ya Isamilo–Nyashana–Nyamuge yenye urefu wa Km 3.28 iliyopo Kata ya Isamilo katika Halmashauri ya Wilaya Nyamagana mkoani Mwanza.
TARURA Mkoa wa Mwanza inahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa Km 8,628 katika Halmashauri zote 8 ambazo ni Nyamagana, Buchosa, Sengerema, Ukerewe, Ilemela, Magu, Misungwi pamoja na Kwimba ambapo kazi za maboresho na ujenzi wa Miundombinu katika Halmashauri zote zinaendelea ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za usafirishaji na usafiri kwa urahisi na kuhakikisha barabara na madaraja zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.