Siku chache baada ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC kuja na kauli mbiu yao ya War in Dar (WIDA) ambayo iliwachakaza FC Platnum kutoka nchini Zimbabwe kwa mabao 4-0 sasa wamekuja na Total War wakiwa wamekusudia jambo lao, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara (katikati) akizungumza na waandishi wa habari Februari 19, 2021 jijini Dar es Salaam, kulia ni Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo cha Habari, Ally Shatry na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko kwa Wekundu wa Msimbazi, George Abdulrahma. (Picha na Mwandishi Diramakini).
Ushindi huo ambao ulichagizwa na kauli mbiu yao hiyo uliwawezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aidha, baadaye katika hatua ya makundi waliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) dhidi ya AS Vita.
Total War ambayo ni mahususi kwa ajili ya kujikuasnyia alama tatu Februari 23, 2021 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa Afisa Habari wa Wekundu hao, Haji Manara imelenga kuzima ndoto za Al Ahly.
“Mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati yetu Simba na Al Ahly kutoka nchini Misri itapigwa saa 10:00 jioni siku ya Jumanne Februari 23, 2021. Ni mechi kubwa sana kwa Simba, Tanzania na Afrika Mashariki,"amesema Manara.
Manara ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Februari 19, 2021 jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa, kauli mbiu hiyo itumike ili kuwapa nguvu Wanasimba wote kuelekea mchezo huo ili kuchukua alama zao tatu.
Afisa Habari huyo amesema, ili kuipa nguvu zaidi kauli mbiu hiyo wameiongezea maneo ya kutorudi nyuma (point of no return) hivyo watasindikizwa na TOTAL WAR, POINT OF NO RETURN.
“Ndugu zangu, hii ni sawa na mtu kuwa porini halafu akutane na chui, lazima apambane bila kukata tamaa vinginevyo atauliwa, hiyo ndio maana halisi ya kauli mbiu yetu hiyo ambayo itawafanya wachezaji waingie uwanjani wakiamini kuwa hakuna nafasi nyingine zaidi ya kushinda,”amesema.
“Mabingwa wa Afrika ambao wametoka kushiriki ubingwa wa dunia wamefanikiwa kushika nafasi ya tatu watakuwa nchini kuwakabili mabingwa mara nyingi zaidi wa Afrika Mashariki. Rekodi hizo zitaufanya mchezo kuwa wa kipekee.Mara ya mwisho tulikutana hapa Dar tukawafunga goli 1-0 kwenye mechi tuliyosema YES WE CAN na tukaweza. Al Ahly mara zote tukicheza Tanzania tunawafunga.
“Tunao uwezo wa kuwafunga tena, tunao uwezo wa kushinda mechi hiyo. Dhamira hiyo ipo kwa kila Mwanasimba kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama na mashabiki wote. Al Ahly sio timu nyepesi. Tunaposema tunaweza kuwafunga tunajua ukubwa wao, lakini Simba hupenda mechi kubwa kama hizi.Tumejiandaa kiakili na tunakwenda kwenye mchezo huu hakuna jambo lingine ila ushindi ili kukaribia lengo letu la nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Mechi ya mwisho tuliita WAR IN DAR, mechi ya jasho na damu ndani ya dakika 90 na sasa tunasema TOTAL WAR : POINT OF NO RETURN hii sasa ni vita kamili ya ndani ya uwanja.Malengo yetu ni makubwa, tunataka kuleta heshima kwa Afrika Mashariki. Tunawakilisha zaidi ya watu 150 milioni, wote hao wanategemea timu moja Simba SC. Tunaenda kutetea Simba, Tanzania na Afrika Mashariki yote.
“CAF wametwambia wanaruhusu watu 30,000 pekee. Kwa timu kubwa kama Simba SC na Al Ahly kiingilio cha Mzunguko - Tsh. 3,000 ukibaki nyumbani Usimba wako ni wa mashaka. 15,000 - VIP B, 30,000 - VIP A . Viingilio hivi mwisho Jumatatu usiku. Ikiingia Jumanne Mzunguko - Tsh. 5,000, VIP B - 20,000 na VIP A - Tsh. 40,000,"amesema Manara huku Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo cha Habari, Ally Shatry akisema kuwa,
"Vikundi vya ushangiliaji tunaomba tukutane siku ya Jumapili (Februari 21, 2021 kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 4:00 asubuhi,”amesema Shatry.
Kwa upande wake,Mkuu wa Kitengo cha Masoko kwa Wekundu wa Msimbazi, George Abdulrahman amesema kuwa,
“Tumesikia changamoto ya vituo vya kuuza tiketi na sasa tumejipanga vizuri, tunawafikia kila sehemu na kesho Jumamosi tutakuwa na roadshow. Kwa mashabiki nawaomba mzingatie kuchukua tahadhari za Covid-19. Tunaomba mkae kwa kupeana nafasi ya kiti kimoja,”amesema.
Tags
Michezo