Mara baada ya kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Mwadui FC, Timu ya KMC FC kwa mara nyingine itashuka dimbani leo kumenyana na Kagera Sugar katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katika mchezo huo, KMC ambao ni wenyeji dhidi wapinzani wao Kagera Sugar, utachezwa saa 14:00 mchana ambapo tayari maandalizi ya mwisho yamefanyika na kwamba wachezaji wote wapo kwenye morali nzuri kuelekea kwenye mtanange huo.
Hayo yamebainishwa na Afisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwangala huku akielezea kuwa timu ya KMC ambayo ipo chini ya kocha mkuu John Simkoko inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuweza kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara.
“Tunahitaji kushinda mchezo wetu wa kesho, ushindi ni mkakati wetu wa kwanza, tunajua duru hii ni ngumu kwasababu kila timu inahitaji alama tatu muhimu, kikubwa tunaendelea kujituma katika maandalizi yetu kila mchezo kwetu ni fainali lengo ni kuhakikisha kwamba kwenye mchezo huo tunakwenda kupata alama tatu,"amesema.
Hadi sasa KMC ipo kwenye nafasi ya sita ikiwa na alama 28 na kucheza michezo 20, mbapo Februali 16 ilipata ushindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya mwadui, mchezo uliopigwa katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Tags
Michezo