Mkutano wa Pili wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza kesho Februari 10, 2021, saa tatu asubuhi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Raya Issa Mselem.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu shughuli za mkutano wa pili wa Baraza la Kumi katika Ofisi ya baraza hilo Chukwani jijini Zanzibar, Katibu wa Baraza Raya Issa Mselem amesema maswali 91 yataulizwa na kujibiwa na mawaziri husika.
Amesema, ripoti ya nne ya Utekelezaji wa Kazi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mwaka 2019/2020 na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa wizara, mashirika na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2018/2019 zitawasilishwa.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi amesema, kutakuwepo na mjadala wa hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar aliyoitoa katika ufunguzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Novemba 11,2020.
Amesema, kutawasilishwa mwelekeo wa Mpango wa Taifa kwa mwaka 2021/2022 na mswaada wa dharura wa sheria ya mambo mbalimbali na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Katibu Raya ameongeza kwamba kutakuwa na ripoti ya jitihada ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar na uchaguzi wa wenyeviti wa Baraza pamoja na marekebisho ya jedwali ya Pili ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma Zanzibar Namba 4 ya 2015.
Kazi nyingine itakayotekelezwa katika Mkutano wa Pili wa Baraza la Kumi la Wawakilishi ni kufanya uchaguzi wa wajumbe wa tano kuingia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uchaguzi wa viongozi wa jumuiya mbalimbali za Baraza ikiwemo CPA, CWP, APNAC, UWAKUZA na Jumuiya ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi.