Afrika Kusini imesitisha kwa muda kampeni yake ya chanjo dhidi ya virusi vya Corona (COVID-19) baada ya utafiti mpya kubaini kuwa chanjo ya AstraZeneca haifanyi kazi vizuri dhidi ya aina mpya ya virusi vinavyopatikana nchini humo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Utafiti huo, uliofanywa na Chuo Kikuu cha Witwatersrand huko Johannesburg umehitimisha kuwa chanjo ya Uingereza ilitoa tu kinga ndogo dhidi ya aina za wastani za ugonjwa unaosababishwa na aina tofauti ya virusi huko Afrika Kusini kwa vijana.
Haya yanajiri ikiwa tangu awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliwatahadharisha Watanzania na mataifa mengine ya Afrika juu ya matumizi ya chanjo za magonjwa mbalimbali zinazotoka mataifa nje ya Afrika kwa kwa ajili ya kukabili maambukizi ya magonjwa hayo.
Rais Magufuli akiwa katika hafla ya kitaifa iliyofanyika wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Dkt. Magufuli alitoa angalizo kwa watanzania kuacha kukimbilia chanjo dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na magonjwa mengine sugu.
Rais Magufuli ingawa hakusema moja kwa moja kwamba maambukizi ya ugonjwa wa Corona yapo nchini, alitaka tahadhari ichukuliwe ikiwemo wananchi kujifukiza, kula vizuri na pia kuendelea kumuomba Mungu kwani yeye ndiye muweza wa mambo yote.
Aidha, Rais aliwataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi huku wakichukua tahadhari za kiafya kwa vile hana mpango wa kuzuia watu kutoka nje kwa kusisitiza kuwa taifa la Tanzania halitaweza kujifungia ndani kutokana na changamoto za Corona.
Wakati huo huo, Afrika Kusini ilikuwa imepanga kuanza kuchanja watu wake kwa dozi milioni moja za chanjo ya AstraZeneca katika siku zijazo.
Utafiti uligundua kuwa chanjo hiyo ilikuwa na ufanisi wa asilimia 22 tu katika visa vya wastani vya aina ya ugonjwa huo wa Afrika Kusini.
Hatua hiyo inatajwa kuwa pigo kwa mipango ya awali ambayo ilielezwa kuwa, chanjo milioni 90 za ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) zitaanza kusambazwa barani Afrika mwezi huu katika kile ambacho kinaelezwa kuwa kitakuwa kampeni kubwa zaidi ya chanjo barani Afrika.
Hayo ni kwa mujibu wa mfumo wa kusambaza chanjo za COVID-19, COVAX ulioundwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.
Chanjo hiyo aina ya AstraZeneca/Oxford AZD1222 iliorodheshwa kwa matumizi ya dharura na WHO ambapo shirika hilo sasa lilikuwa linathamini chanjo hiyo na matokeo yatatangazwa karibuni.
“Afrika imeshuhudia maeneo mengine yakianza utoaji wa chanjo ya COVID-19, yenyewe ikiwa kando. Mpango huu wa kupeleka chanjo ni hatua ya kwanza muhimu katika kuhakiisha kuwa bara hilo linapata fursa sawa ya chanjo kama maeneo mengine,”alisema Dkt.Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika akizungumza katika mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao huku akiongeza kuwa, “tunatambua kuwa hakuna aliye salama hadi pale kila mtu atakuwa salama.”
COVAX kupitia barua yaka ya Januari 30, mwaka huu ilijulisha nchi za Afrika kuhusu mpango huo wa upelekaji chanjo.
Kutokana na kiwango kikubwa cha mahitaji ya chanjo ya COVID-19, shehena za mwisho zitategemea kiwango cha uzalishaji kutoka kwa kampuni husika na utayari wa nchi kupokea chanjo hizo.
Nchi zinazopokea chanjo hizo zinatakiwa kuwasilisha mipango yao ya mwisho ya usambazaji na utoaji wa chanjo hiyo kutoka COVAX.
Chanjo dhidi ya COVID-19 iliyotengenezwa na Pfizer-BioNTech ni ya kwanza kuidhinishwa na baadhi ya nchi na inahitaji kuhifadhiwa ubaridi wa 70°C.
Mbali na chanjo hiyo ya sasa, dozi 320,000 za chanjo aina ya Pfizer-BioNTech zimepangwa kwa mataifa manne ya Afrika ambayo ni Cape Verde, Rwanda, Afrika Kusini na Tunisia.
Chanjo hii ilipokelewa na WHO na kuorodheshwa kwa mahitaji ya dharura, lakini inahitaji nchi kuwa na uwezo wa kuhifadhi na kusambaza katika kiwango cha nyuzi joto 70 chini ya sifuri katika kipimo cha selsiyasi.
Katika kuwasilisha ombi la chanjo hiyo ya Pfizer, nchi zilitakiwa kuwasilisha maombi ambapo nchi 13 ziliwasilisha na maombi yao kufanyiwa tathmini ikiwemo kiwango cha sasa cha vifo kutokana na COVID-19 na uwezo wa kuhifadhi chanjo chanjo hizo katika joto la -70°C.