Ofisi ya TAKUKURU mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, imemfikisha katika mahakama ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mwalimu Wilfred Emanuel Manumbu kwa makosa ya mawili, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kosa la kwanza ni wizi akiwa mtumishi wa umma ambapo anatuhumiwa kumwibia mwajiri wake ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha sh. 10,947,400/= na kosa la pili ni kumsababishia hasara mwajiri wake ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha sh. 10,947,400/=.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na H.M MUSSA, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 07/2021 mshtakiwa alikiri kutenda makosa hayo ambayo aliyafanya kati ya mwezi Oktoba 2013 na Januari 2016 huko katika Halmashauri ya wilaya ya Ushetu alikokuwa ameajiriwa kama Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyaweshi.
Mshtakiwa alikiri makosa yake na mahakama imemtia hatiani kwa makosa yote mawili na kumhukumu kwenda jela miaka mitatu (03) na kulipa fedha zote alizohujumu kiasi cha sh. 10,947,400/=
Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU ili kuhakikisha kuwa tunaondoa kero za rushwa katika mkoa wetu wa Shinyanga.
Tags
Habari