Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula ametaka kuundwa vikosi kazi kwa ajili ya kuendesha zoezi la upimaji ardhi katika mikoa ili kuongeza kasi ya upimaji ardhi,anaripoti Munir Shemweta (WANMM) GEITA.
Sehemu ya Watendaji wa Sekta ya Ardhi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayupo pichani) wakati wa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Geita tarehe 16 Februari 2021.
Dkt.Mabula ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Februari 2021 wakati wa ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Geita kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi.
Amesema, katika kuharakisha zoezi la upimaji katika maeneo mbalimbali nchini ni lazima mikoa kupitia ofisi zake za wilaya kwa kushirikiana na ofisi za ardhi kuunda vikosi kazi vya upimaji vitakavyopita wilaya moja hadi nyingine ili kuharakisha upimaji.
Ameongeza kuwa, cha muhimu ni wakati wa zoezi hilo ni kuangalia ni halmashauri gani yenye vifaa na iliyo tayari kupimiwa ambapo mkurugenzi wake atawajibika kuihudumia timu itakayofanya kazi na kubainisha kuwa pamoja na zoezi hilo kuongeza kasi ya upimaji lakini litasaidia kuondoa migogoro.
"Tunataka kila mkurugenzi katika eneo lake ahakikishe anapima maeneo yake kwa kuwa halmashauri ni mamlaka ya upangaji na tukifanya hivi ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tumepima maeneo mengi,"amesema Dkt Mabula.
Amegeukia suala la utoaji hati za ardhi kwa wamiliki, Dkt Mabula amezitaka ofisi za ardhi katika halmashauri kuanza kujiwekea malengo ya utoaji hati ambapo aliweka bayana kuwa kumekuwa na kasi ndogo ya utoaji hati kwenye baadhi ya halmashauri.
"Haiwezekani mkoa mzima wa Geita kwa miezi sita uwe umetoa hati 586 pekee hapa lazima kila ofisi ijiwekee malengo, kila mtumishi wa sekta ya ardhi awekewe malengo ya kuandaa idadi ya hati kwa siku," amesema Naibu Waziri Mabula.
Aidha, Dkt Mabula amezitaka halmashauri kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na zoezi la urasimishaji linalofanywa na makapuni ya upimaji katika maeneo mbalimbali mkoani Geita
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wakurugenzi pamoja na Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Geita wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi tarehe 16 Februari 2021. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Fadhili Juma.
Amesema, Makampuni ya upimaji katika mkoa wa Geita yamefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kupima maeneo kwa kutumia fedha zake hivyo halmashauri za mkoa huo zinatakiwa kuwaeleza wananchi umuhimu na faida ya kupimiwa maeneo yao.
Mwakilishi wa Kampuni ya Upimaji ya Amboni Land Survey Ngusa Juda alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa, pamoja na kampuni yake kukamilisha kazi ya upimaji katika maeneo iliyopangiwa likiwemo eneo la Nyalugusu katika mkoa wa Geita lakini wananchi wameshindwa kulipa fedha kwa wakati na kuiomba serikali kupitia halmashauri kusaidia kuhamasisha wananchi waweze kukamilisha malipo.
Tags
Habari