Ngorongoro Heroes wagawana pointi na Gambia michuano ya AFCON U20

Vijana wa Tanzania wanaotuwakilisha katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 (AFCON U20) timu ya Ngorongoro Heroes wametoshana nguvu baada ya sare ya 1-1 na Gambia katika mchezo wa Kundi C usiku wa kuhamkia leo huko nchini Mauritania, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanange baina ya Tanzania na Gambia. (Picha Caf/Diramakini).

Awali, vijana wa Gambia walitangulia kwa bao la Momodou Bojang dakika ya 40, kabla ya Novatus Dismas kuisawazishia Ngorongoro Heroes dakika ya 87.

Wamesema nini?

Man of the match – Kajally Drammeh (The Gambia)

Nina furaha kutajwa kuwa man of the match, lakini matokeo ya leo yamenivuruga sana. Tumetengeneza nafasi za kutosha kwa ajili ya ushindi, lakini mambo hayajawa hivyo. Sasa tunakwenda kujipanga zaidi kwa ajili ya mtanange kati yetu na Ghana kwa ajili ya kutafuta namna ya kusonga mbele katika michuano hii.

Mattar M’boge (Kocha Mkuu, Gambia)

Ulikuwa mchezo mzuri sana. Timu zote zilijaribu kushinda mchezo huu, lakini wote tumeishia suluhu, nafikiri hata waliotazama mchezo huu wamefurahi sana.

Timu zote zimejaribu kujihami na kushambulia kwa nguvu na kupata goli, hivyo nichukue nafasi hii kuipongeza Tanzania na pia kuwapongeza wachezaji wangu ambao wameonyesha bidii kubwa katika mchezo wa leo.

Ingawa tumeambulia goli moja, tunaweza kujilaumu maana tulikuwa na nafasi nzuri ya kushinda mabao mawili kwa sufuri, kwa ujumla ninaweza kusema, matokeo haya si ya kufurahisha kwani alama moja si nzuri kwa nafasi ambayo tulikuwa nayo kushinda leo.

Jamhuri Mussa Kihwelo (Kocha Mkuu, Tanzania)

Timu hii ya Wagambia ni miongoni mwa timu bora sana katika haya mashindano, hivyo ninawapongeza, lakini ninafikiri leo hatukuwa na bahati. Tulipaswa kushinda mchezo wa leo,lakini ninashukuru kwa kila jambo. Sasa tunajipanga kwa ajili ya mchezo wa mwisho na Morocco.

Hata hivyo, Tanzania iliyochapwa 4-0 na Ghana katika mechi yake ya kwanza, itakamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na Morocco Jumanne ijayo kuangalia mustakabali wake wa kusonga mbele katika mtanange huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news