NI JUKUMU LA JAMII KUWASAIDIA WATOTO WENYE ULEMAVU:PAROKO

Wito umetolewa kwa jamii ya Watanzania kuwasaidia watoto wenye ulemavu na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu, anaripoti Mwandishi Diramakini (Morogoro).
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Gonzaga Mvomero, jimbo Katoliki la Morogoro, Herman Kiangazi wakati wa tamasha la usiku wa mwangaza, tamasha mahususu kwa ajili ya kuwaenzi watoto wenye ulemavu.

Kiangazi amesema kuwa watoto ni baraka kutoka kwa Mungu, hivyo sisi wanadamu tunatakiwa kuzipokea baraka hizo kutoka kwa Mungu pasipo ubaguzi ya kuwa huyu ni mlemavu ama lah.

“Binadamu wote ni sawa, hali kadharika watoto wote ni sawa, tusiwabague watoto wenye ulemavu bali kama jamii tunapaswa kuwapenda, kuwasaidia, kuwaongoza na kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji yote muhimu ikiwa ni pamoja na elimu na ustawi wa afya zao,"amesema.

Kiangazi ameongeza kuwa ni vema jamii ikatupia jicho juu ya madhila yanayowapata watoto wenye ulemavu na wanaoishi kwenye mazingira magumu ili waweze kuishi kama wanavyoishi watoto wengine na kusaidiwa kufikia ndoto zao.

Akizungumza kwenye tamasha hilo, Mkurugenzi wa taasisi ya kulelea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo ya EMFERD, Josephine Bakhita, alisema kuwa jamii inapaswa kufahamu kuwa ulemavu sio kushindwa bali ni maumbile tu.

“Ulemavu sio kushindwa kila kitu. Watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kufanya mambo ambayo hata sisi tulio wazima hatuwezi,"amesema Bakhita.

Bakhita amesema kuwa ni vema jamii ikaondoa mtazamo hasi juu ya wenye ulemavu kuwa hawawezi chochote, kinyume chake wanapaswa kuwasadia kupata elimu na ujuzi wa aina mbali mbali ili waweze kupata ustawi na kuepukana na utegemezi kwa kujisaidia wenyewe.

"Wapo wenye ulemavu ambao wana vipaji, ujuzi na maarifa makubwa, hao wanachagia pato la familia na jamii kwa ujumla. Ni jukumu letu sisi tusio na ulemavu, kila mmoja kwa nafasi yake, kuondokana na mtazamo hasi juu ya ulemavu na kuwasaidia watu wenye ulemavu ili waweze kujisaidia wenyewe,"amesema Bakhita.

Akielezea kuhusu tamasha la usiku wa mwangaza, Bakhita alisema kuwa tamasha hilo hufanyika kila mwaka mahususi kuihamasisha jamii kuwaenzi na kuwapa nafasi ya heshima watu wenye ulemavu huku likiwa linafadhiriwa na mcheza kikapu maarufu wa nchini Marekani, Tim Tabew.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news