Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William Kijazi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
Wakati wa tukio hilo la kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John William Kijazi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Huku akianisha kuwa, marehemu Balozi Kijazi alikuwa mchapa kazi, kwani hata awali alikosa mtu wa kumteua kuwa Katibu Mkuu kiongozi baada ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Balozi
John Kijazi kustaafu mwaka 2017 na hivyo kuamua kumuongezea muda tena.
Rais Magufuli
amesema hayo Februari 19, 2021 katika ibada ya
mazishi ya Balozi Kijazi aliyefariki dunia usiku wa Februari 17, 2021
katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu jijini Dodoma.
Aidha, Rais Magufuli
amesema Balozi Kijazi aliyezaliwa mwaka 1956 umri wake wa kustaafu
ulifika mwaka 2017 na alilazimika kuendelea kufanya naye kazi kutokana
na kukosa mbadala wake.
“Alizaliwa mwaka 1956, lakini mpaka leo
alikuwa bado ni katibu mkuu kiongozi, maana yake ulipofika wakati wa
kustaafu mwaka 2017 nikajaribu kuangalia nani wa kuchukua nafasi yake
nikakosa.
“Nikamuongeza miaka miwili nikifikiri ndani ya muda huo
nitapata mwingine, lakini hadi mwaka 2019 sikupata, nikamuongeza tena
miaka mingine miwili, Mungu akasema umezoea kweli akamtumie yeye
mwenye,”amesema Rais Dkt.Magufuli.
Pia ametumia nafasi hiyo kutoa pole kwa
familia, mke wa marehemu na watoto huku akibainisha kuwa Kijazi alikuwa
mtu mwenye upendo mkubwa na alimpenda Mungu na siku za Jumapili
hakukosa kwenda kanisani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili kuliepusha Taifa dhidi ya virusi vya ugonjwa wa Corona (COVID-19) na kusisitiza kuwa hatatangaza kuwafungia watu ndani.
"Tusitishane na kuogopeshana Mungu yupo, Mungu ndiyo muweza wa yote, Tuendelee kusimama na Mungu, tulishiinda Corona mwaka jana. Naomba Tusimame na Mungu.
"Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, magonjwa ya vifua, magonjwa ya kupumua na kadhalika yatakuwepo na hayakuanzia hapa, Zipo Nchi ambazo zimepoteza watu wake wengi. Sisi Tanzania Mungu ametusaidia sana mwaka uliopita, tuendelee kuchukua tahadhari huku tukimuomba Mungu. Mungu hashindwi,"amesema Rais Dkt.Magufuli.
"Naomba tusitegemee nguvu za ubinadamu, bali tumtegemee Mungu. Narudia ndugu zangu tujue Mungu yupo. Mungu ndiyo muweza wa yote. Nashukuru viongozi wa dini mmeendelea kulihubiri hilo. Tuendelee ndugu zangu kusimama na Mungu. Tulishinda mwaka jana, inawezakana hili ni jaribu jingine, nalo tukisimama na Mungu tutashinda,"ameongeza.
Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu wakuu wakijiandaa kwenda kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021."Tusitishane na kuogopeshana, tutashindwa kufika.
"Inawezekana kuna
mahali tumemkosea Mungu. Inawezeakana kuna mahali tunapata jaribu kama
wana wa Israel walivyokuwa wanaenda Kaanani. Tusimame na Mungu ndugu
zangu Watanzania. Kufa tutakufa tu,unaweza kufa kwa malaria,ukafa kwa
Kansa,ukafa kwa magonjwa mengine kwa sababu kufa kupo lakini Kamwe
tusimuache Mungu. Huo ndiyo wito wangu.
"Tusimame na Mungu ndugu
zetu Waislamu walitangaza muda wao wa kuomba na niliambiwa na
Mufti,niwaombe tena Watanzania kama kuna mahali tumetetereka tuendelee
kumuomba Mungu. Tuanze leo kwa ndugu zetu Waislamu,kesho Jumamosi kwa
ndugu zetu Wasabato wanaosali Jumamosi na Jumapili kwa ndugu zetu
Wakristo kwa kumuomba kufunga kwa siku tatu. Mimi nina uhakika
tutashinda. Nataka niwape nguvu hiyo ndugu zangu Watanzania,"ameongeza
Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William Kijazi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
"Naomba viongozi wa dini muendelee kusisitiza
maombi. Tulishinda mwaka jana, tutashinda mwaka huu, tutashinda miaka
yote kwa sababu kamwe Mungu hajaweza kuliacha taifa hili.Tumeshinda
mwaka jana na tukaingia kwenye uchumi wa kati na Corona ipo,uchumi
ukaendelea kupanda na Corona ipo,miradi ikaendelea kutekelezwa wala
hatukuweka Lockdown hata sasa hatutaweka Lockdown kwa sababu tunajua
Mungu yupo siku zote. Taifa hili lipo mikononi mwa Mungu,"amesema Rais
Magufuli.
Mbali na hayo, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ameeleza kusikitishwa
na watu wanaozusha taarifa za uongo kwamba Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango amefariki dunia huku akisoma ujumbe mfupi aliotumiwa na Waziri Dkt. Mpango
kuhusu hali anayoendelea nayo.
"Imefikia mahali sasa
tunatishana sana. Leo asubuhi nilitumiwa meseji na Waziri wa Fedha, Dkt.
Mpango ambaye amelazwa Dodoma na ninaomba niiosome hapa kwa faida ya
wale waliokuwa wana 'Twiti' kwamba amekufa,"amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
Rais
Magufuli amesema katika ujumbe huo, Dkt. Mpango amemueleza kuwa kwa neema ya Mungu anaendelea vizuri, anakula vizuri na anaendelea
kufanya mazoezi ya kifua na kutembea na kwamba wale waliomzushia
mtandaoni kuwa amefariki dunia amewaombea kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.
“Mheshimiwa Rais, asante sana nimepata ujumbe wako kupitia kwa mke
wangu, kwa neema ya Mungu naendelea vizuri, ninakula, ninafanya mazoezi
ya kifua na kutembea, hao wanaonizushia kifo kwenye mitandao niliwaombea
msamaha kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.”
“Mheshimiwa Rais
Mungu akubariki na akupe neema na ujasiri zaidi katika kuliongoza Taifa
letu, katika wimbi hili naungana na wanafamilia katika kuomboleza kifo
cha Katibu mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rest in Peace,” amesema
Magufuli akimnukuu Dk Mpango.
Akifafanua kuhusu ujumbe huo
Magufuli amesema, “ni huyo ambaye aliambiwa jana amekufa, yeye amesema
katika sala yake jana jioni aliwaombea msamaha kwa Yesu.”
“Magonjwa
yapo na yatendelea kuwepo, magonjwa ya kupumua na vifua pia yataendelea
kuwepo na hayakuanzia hapa kwani zipo nchi zilizopoteza watu wengi
lakini Tanzania Mungu ameisaidia katika mwaka uliopita,"amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
Wakati huo huo akimzungumzia aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17, 2021
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu
na kuzikwa jana Mtamwe wilayani Wete kisiwani Pemba, Zanzibar, Rais Dkt.
Magufuli amesema baada ya kufanya mazungumzo naye wakati wa uhai wake alibaini kuwa
Maalim Seif alikuwa ni kiongozi wa tofauti sana.
“Maalim Seif
alikuwa ni kiongozi wa tofauti sana mwaka 2015 nilipokuwa rais baada ya
uchaguzi wa Zanzibar kufanyika ule wa marudio, Maalim Seif aliniandikia
barua akiniomba kuja kuniona nilisita kidogo kwamba kwa nini anataka
kuja kuniona na wakati hata kwenye uchaguzi hakushiriki, Maalim Seif
akaandika tena barua ya pili na baadaye akaandika barua ya tatu.
“Kila
nilipokuwa najaribu kupata ushauri kutoka Zanzibar nilikuwa naambiwa
nisubiri nimuache, lakini baadaye nikaamua ngoja nimuone Maalim Seif.
Alipokuja Ikulu Dar es Salaam nilipoanza kuzungumza naye nilimuona mtu
tofauti sana na jinsi picha ilivyokuwa imejengeka kwa sababu mazungumzo
yetu yalikuwa mazuri sana,”ameeleza Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
Rais Magufuli amesema,
Maalim Seif alimueleza kuwa hakushiriki kwenye uchaguzi wa marudio
Zanzibar uliofanyika Machi, 2016 baada ya ule wa Oktoba 25, 2015 kufutwa
akisisitiza kuwa licha ya jambo hilo kutokea, lakini Zanzibar itakuwa
salama na kwamba hatohamasisha fujo.
Akiendelea kumnukuu
Maalim Seif, Rais Magufuli amesema kuwa,“Pili lakini nataka
kukuhakikishia Zanzibar itakuwa salama sitahamasisha fujo yoyote na
miaka yote mitano aliyechaguliwa ataendelea vizuri kutawala kauli hiyo
niliiona mpaka baada ya miaka mitano alieleza yeye anapenda amani na
angependa Zanzibar na Watanzania wote wakae kwa amani, kauli hiyo
niliithibitisha kwa vitendo ulipotokea uchaguzi mwingine Maalim Seif
bado alishiriki katika Serikali ya Muungano, Serikali ya Umoja wa Kitaifa".
Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka akiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Bi. Dorothy Mwaluko wakibeba shada la maua lenyen herusi KMK yaani Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi
Balozi John William KijaZi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021. (Picha zote na Ikulu).
“Alikuwa
ni mtu mcheshi na siku zote katika ziara yake hata kule Chato alikuwa
akihubiri umoja wa Wanzanzibar umoja wa Watanzania kitu ambacho
amemaliza nacho, Maalim Seif amemaliza salama na dhamira yake ya
kuijenga amani na Wazanzibari na Watanzania kwa pamoja,”amesema.
“Natoa
pole kwa Watanzania wote kwa vifo vyote viwili, cha Maalim Seif pamoja
na cha Balozi Kijazi, Jana nilimtuma Makamu wa Rais na Dkt. Bashiru
waniwakilishe kwenye mazishi ya Maalim Seif". Kijazi ameondoka hapa
duniani kama Shujaa, Maalim Seif kaondoka hapa duniani kama shujaa.
“Balozi
Kijazi na Maalim Seif wametangulia zamu yetu sisi bado, Watanzania
katika matatizo yoyote yanapotokea yatufanye tuwe wamoja, hofu ni mbaya,
ukiona kitu hauwezi kukitatua wewe, mwambie Mungu ndiye muweza,
tumekuwa tunatishana sana, tusitishane,"amesema Rais.
Zanzibar
Awali wakati wa maziko, akisoma
wasifu wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamo wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu na Shughuli za Baraza la
Wawakilishi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema kuwa Marehemu
Maalim Seif alizaliwa tarehe 22 Octoba mwaka 1943 , Mtambwe Nyali na
alipata elimu ya Msingi katika Skuli ya Uondwe na Skuli ya Wete Boy’s
huko Pemba kati ya mwaka 1950 – 1957.
Alieleza
kuwa Maalim Seif alisoma Elimu yake ya Sekondari kuanzia mwaka 1958
hadi 1961 katika Skuli ya King Geoge VI Memorial mjini Zanzibar ambayo
kwa sasa ni Skuli ya Sekondari ya Lumumba na aliendelea na masomo ya
cheti cha cha sekondari katika skuli hiyo.
Mwaka
1972 -1975 , alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es –Salaam kwa masomo ya
Shahada ya Kwanza katika fani ya Sayansi ya Siasa, Utawala wa Umma na
Ushirikiano wa Kimataifa na kutumikia Digrii ya Heshima (BA
honours)mwaka 1975.
Marehemu
Maalim Seif Sharif alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa
Elimu kuanzia mwaka 1977 hadi 1980 na kubahatika kuwa mmoja wa Wajumbe
waanzilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mwaka 1980 na kuendelea
hadi mwaka 1989 na mwezi Februari, 1984-1988 alikuwa Waziri Kiongozi wa
Zanzibar.
Waziri
Khalid alimuelezea Marehemu Maalim Seif jinsi alivyoanzisha chama cha
CUF na baadae kujiunga na ACT Wazalendo mnamo Machi 2019 sambamba na
kuteuliwa kuwa Makamo wa Kwnaza wa Rais aliyoishikilia kaunzia Novemba
9,2010 hadi Machi 2016.
Pia,
Marehemu aliteuliwa tena kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais kufuatia
kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, na kuteuliwa kushika nafasi
hiyo tarehe 7 Disemba nafasi ambayo aliishikilia hadi alipofikwa na
mauti jana (tarehe 17 Februari,2021). Marehemu ameacha kizuka na watoto
wanne.