Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametembelea baadhi ya maeneo ya mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) huku akitoa agizo la kuhakikisha hadi mwisho wa mwezi wa tatu sehemu zilizokuwa hazijakamilika katika eneo la barabara ya uwanja wa ndege wa Zanzibar hadi MnaziMmoja ziwe zimekamilika, anaripoti Mwandishi Diramakini (Zanzibar).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika matembezi ya ziara yake kutembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Huduma za Jamii Mjini Zanzibar (ZUSP) aliazia katika eneo la barabara ya Kiembesamaki Uwanja wa Ndege kutembea na kujionea utekelezaji huo na kumalizia matembezi hayo katika eneo la mnazi mmoja na kuzungumza na Uongozi unaosimamia Mradi huo, na (kulia kwa Rais) Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Mohamed na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.Rais Dkt. Hussein ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake hiyo ambayo
alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyomo kwenye mradi wa
ZUSP katika mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na kukagua dampo kuu la
Kibele huku akiwasikiza changamoto za baadhi ya wananchi aliokutana nao
njiani.
Akimalizia ziara yake aliyotembea kwa miguu kutoa uwanja
wa ndege wa Abeid Amani Karume hadi Mnazi Mmoja, akiwa amefuatana na
viongozi mbalimbali akiwemo Mama Mariam Mwinyi, Dkt. Mwinyi alieleza
kuridhishwa na maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya Disemba 9,
2020 licha ya kuwa baadhi ya maeneo hayajakamilika na kutaka hadi mwisho
wa mwezi ujao yakamilike.
Amesisitiza kwamba barabara hiyo ya
kutoka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume hadi MnaziMmoja ndio
iwe kigezo kwa barabara nyengine zote za Mji wa Zanzibar kwani
kinachoonekana ni kuwa bado barabara nyingi za mji ni chafu.
Rais
Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuzipongeza na kutoa shukurani kwa
kampuni zilizounga mkono katika kusaidia kuweka vigae, bustani na
matengenezo mengine pembezoni mwa barabara hiyo inayotoka uwanja wa
ndege hadi Mnazi Mmoja huku akivisifu Vikosi vya SMZ kwa kuunga mkono
matengenezo hayo katika maeneo yao.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi
alisikitishwa na tabia ya maeneo ya hifadhi ya barabara kufanywa sehemu
ya biashara na kuagiza kutafutwa taratibu za kuhakikisha kadhia hiyo
inaondoshwa.
Pia, alieleza jinsi ya miti iliyopandwa katika
barabara za Mjini pamoja na kuwepo baadhi ya taa ambazo haziwaki na
kutoa agizo kwa wale wote waliopewa jukumu hilo katika mradi huo wa ZUSP
kuhakikisha changamoto hiyo inafanyiwa kazi.
Hivyo, aliutaka
uongozi wa Serikali ya Mkoa, Wilaya pamoja na Manispaa katika
kuhakikisha suala la usafi na mipango ya Miji linafanyiwa kazi huku
akisisitiza umhimu wa kukusanya kodi na kuwataka Wakurugenzi wa Manispaa
kuhakikisha wanakusanya kodi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati akiwa katika matembezi ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Huduma za Jamii Mjini Zanzibar (ZUSP) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana, wakiwa katika ziara hiyo kutembelea mradi huo wakipita katika eneo la Kilimani na (kushoto) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi.
Aidha, akieleza juu ya vyombo vya usafiri kupita katika maeneo ya
Mji Mkongwe, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi waliolalamikia suala la
usafiri katika eneo hilo kwamba usafiri wa bodaboda umekatazwa katika
eneo hilo kutokana na sababu maalum za uhifdhi wa Mji Mkongwe.
Pia,
kwa upande wa wananchi alisema kuwa utaratibu wa kuzuia vyombo hivyo
kwa watu binafsi unakwenda kwa awamu hivyo, hairuhusiki kuwazuia
wananchi kupita katika sehemu hizo bila ya kuwawekea utaratibu maalum na
kuutaka uongozi wa Mkoa na Wilaya kulisimamia hilo.
Rais Dk.
Mwinyi, pia aliutaka uongozi wa Mkoa na Manispaa ya Mjini kukaa na
wananchi waliotoa wazo la kujengwa mtaro katika eneo la MnaziMmoja ili
kuuhami uwanja huo ambao umekuwa ukituama maji wakati wa mvua pamoja na
pembezoni mwa Hospitali ya Mnazi Mmoja katika eneo la Dodoma.
Katika
ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi aliitaka Wizara ya Mawasiliano kupitia
Wakala wa Barabara kuhakikisha inalitengeneza vizuri eneo la barabara
iliyokaa muda mrefu bila ya kutiwa lami na kuleta usumbufu kwa wapita
njia.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo na kutowa maagizo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mradi wa (ZUSP) akiwa katika eneo la kilimani akiendelea na matembezi yake ya ukaguzi wa mradi huo na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ. Mhe. Masoud Ali Mohamed, Waziri wa Maji na Nishati Mhe. Suleiman Masoud Makame na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliani na Uchukuzi Ndg. Amour Hamil Bakari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi na Viongozi wa Serikali wakati wa ziara yake ya kutembelea Mradi wa Huduma za Jamii Mjini Zanzibar (ZUSP) katika maeneo ya mnazi mmoja wakati wa kumalizia matembezi ya ziara yake kukagua mradi huo, (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.
Akiwa katika eneo la Kilimani baada ya kupokea na kusikiliza malalamiko
ya mwananchi mkazi wa nyumba za maendeleo za Kilimani, Rais Dkt. Mwinyi
amesisitiza haja ya wananchi kulipa kodi za makazi katika nyumba hizo
ili pesa zinazopatikana ziweze kufanyia ukarabati wa nyumba hizo.
Aidha,
aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuangalia sheria
zinasemaje kwa wale wenye baa kuweko na utaratibu maalum wa kuhakikisha
hawawabughudhi wananchi wanaoishi karibu ya baa hizo kwa kupiga miziki
masaa yote.
Rais Dk.Mwinyi alitoa agizo hilo baada ya kupata
masikitiko kutoka kwa Hamida Ali Mwinyigogo aliyeeleza kwamba wamekuwa
wakipata kadhia kubwa ya kupigiwa miziki masaa yote.
Nae Mkuu wa
Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana alitoa shukurani kwa Rais wa
Zanzibar kwa ziara yake hiyo pamoja na kuzishukuru Kampuni zote
zilizojitolea pamoja na vikosi vya SMZ katika kutengeneza maeneo ya
pembezoni mwa barabara kutoka uwaja wa ndege hadi MnaziMmoja.
Baada
ya kuondoka hapo Rais Dk. Mwinyi alielekea Maruhubi katika kituo cha
kukusanya taka na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Mkoa wa Mjini
Magharibi pamoja na uongozi wa ZUSP ambapo Rais alisisitiza kwamba bado
kituo hicho hakijafanya kazi yake ipasavyo.
Hivyo, aliziagiza
taasisi husika kuhakikisha inazitoa taka katika eneo la mji wa Zanzibar
pamoja na kuhakikisha wanazifanyia ukarabati gari zao ili kurahisisha
zoezi hilo huku akiwataka kuacha urasimu.
Akiwa katika eneo la
Kwamtumwa Jeni, Rais Dk. Mwinyi alisikiliza malalamiko ya wananchi juu
ya kutuama kwa maji katika eneo hilo la makaazi yao licha ya kujengwa
mtaro katika mradi wa ZUSP na kuagiza kampuni ya CRJE ya China,
kuhakikisha inarudi tena kurekebisha tatizo hilo kabla ya kupewa fedha
zao.
Rais Dkt. Mwinyi pia, alifika katika kituo cha kukusanya
taka Kwa Binti Hamrani, huko Mpendae Mjini Unguja na kupewa maelezo juu
ya huduma zitakazotolewa katika kituo hicho.
Akiwa katika eneo
la Kwarara, Wilaya ya Magharibi B, Rais Dkt. Mwinyi alieleza hatua
zitakazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kituo cha Polisi
kinakuwepo katika eneo hilo pamoja na kutatua changamoto ya barabara
kituo cha afya pamoja na maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.
Wananchi wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati akizungumza na Viongozi na Wananchi juu ya ziara yake kutembelea na kujionea utekelezaji wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini Zanzibar (ZUSP) akimalizia matembezi ya ukaguzi wa mradi huo katika eneo la mnazi mmoja. Matembezi hayo yameazia barabara ya Kiembesamaki Uwanja wa Ndege ulikoazia mradi huo hadi mnazi mmoja.
Mwananchi mkazi wa Kikwajuni Ndg Adam Natepe akizungumzia kero ya Uwanja wa Mpira wa Mnazi Mmoja kujaa maji wakati wa mvua na kutoa mchango wake kuondoa kero hiyo, kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) wakati wa ziara yake kutembelea Mradi wa Huduma za Jamii Mjini (ZUSP) (Picha zote na Ikulu).
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana alieleza jitihada zilizochukuliwa katika kuzuia uchimbaji mchanga katika eneo hilo pamoja na utupaji taka ovyo kwa kushirikiana na ulinzi shirikishi ambapo wamezikamata gari 6 za ng’ombe na ng’ombe 8 huku akilitaka Shirika la Umeme Zanzibar ZECO kusimami ulinzi katika nguzo lizopita umeme mkubwa katika eneo hilo.
Baada ya hapo, Rais alifika eneo la Jaa la Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, na kueleza haja ya kuwa na orodha ya gari zote zinazotoa huduma za maji machafu ili iwe rahisi kuweza kuondoa changamoto ya kumwanga maji katika maeneo yasiyoruhusika badala ya kumwaga katika eneo hilo na zile zitakazokaidi zifutiwe leseni.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadidu Rashid alimueleza Rais changamoto ya ukosefu wa maji taka yanayotakiwa katika eneo hilo kwa ajili ya mradi huo katika eneo hilo la Kibele.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alizitaka Manispaa za Mkoa wa Mjini Mgharibi kukusanya taka na kupeleka katika eneo hilo na wasione mzigo kwani taka ni mali kwa ajili ya kupata umeme sambamba na kujua kiasi cha taka wanazozalisha.
Akizungumza na wananchi waliokwenda kutoa malalamiko yao juu ya fidia katika eneo hilo la Kibele, Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Wizara ya Nchi (OR) Fedha na Mipango kuhakikisha unafanya uhakiki na kuhakikisha zoezi la fidia linafanyika kwa uadilifu kwani kuna baadhi ya wafanyakazi katika ofisi hiyo si waadilifu.
Sambamba na hayo, aliwataka wananchi hao kwa upande wao kuridhika na kile wanachopewa badala ya kufuatwa utaratibu uliowekwa kwani kila mtu atapewa fidia kwa vigezo vilivyowekwa.