Rais Dkt.Mwinyi atuma salamu za rambirambi kifo cha Dkt. Mohamed Seif Khatib

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Dkt. Mohamed Seif Khatib aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar pamoja na Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi

Kifo cha Dkt. Mohamed Seif Khatib kimetokea leo Februari 15,2021 katika Hospitali ya Al-Rahma jijini Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa kesho saa nne huko kijijini kwao Umbuji, Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Dkt. Mohamed Seif Khatib.

Salamu hizo zimeeleza kwamba yeye binafsi, familia yake pamoja na wananchi wa Zanzibar na wa Tanzania kwa ujumla wamesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo hicho.

“Mimi namfahamu Dkt. Mohamed Seif Khatib kuwa ni kiongozi mahiri, aliyependa kazi, mvumilivu na aliekuwa na mashirikiano mazuri na wenzake wote ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,”imeeleza sehemu ya salamu hizo za rambirambi. Aidha, kupitia salamu hizo za rambirambi, Rais Dkt. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu kuwapa moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba, familia, marafiki, ndugu pamoja na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Salamu hizo zimeendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kumpa rehma na kumjalia makazi mema peponi. Amin.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news