Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imewarejeshea wastaafu 17 mamilioni ya fedha walizodhulumiwa kupitia mikopo umiza, anaripoti Mwandishi Diramakini (Dodoma).
Hayo yamebainishwa leo Februari 18, 2021 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma,Sosthenes Kibwengo.
"TAKUKURU inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ambapo leo tunawapa taarifa ya fedha na mali tulizookoa. Kwanza, mwezi uliopita (Januari 2021) tuliwatangazia kwamba tunafanya uchunguzi dhidi ya kampuni ya Geneva Credit Shop ya Mjini Kondoa inayojishughulisha na ukopeshaji wa fedha, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wengi ambao wanadai kupatiwa mikopo umiza na Kampuni hiyo.
"Uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma umefanikiwa kumpata mmiliki wa kampuni hiyo Bw. Abubakary Idd Kinyuma maarufu kama Abubakary Mapesa ambaye hadi sasa amerejesha jumla ya shilingi milioni mia moja sabini na sita laki tano sitini na tano (176,565,000/=) na nyumba moja ambapo leo tunawakabidhi wakopeshwaji 17 wengi wao wakiwa ni Walimu wastaafu ambao uchunguzi wetu umeonyesha kwamba walilipishwa fedha hizo na kunyang’anywa nyumba na Bw. Mapesa kinyume na taratibu.
"Uchunguzi wetu umebaini kwamba baadhi ya watumishi wa umma wilayani Kondoa wanapokaribia kustaafu, kwakuwa wanatarajia kulipwa mafao yao, huchukua mikopo midogo kwa Bw. Mapesa ambaye amekuwa anachukua kadi zao za benki na kuzihifadhi na pindi mafao yao yanapotoka hujitwalia kiasi kikubwa cha fedha kwa riba kubwa hadi kufikia asilimia elfu kumi.
"Mfano, Mwalimu Mstaafu mmoja alikopeshwa shilingi 350,000/= lakini pamoja na kurejesha shilingi 4,600,000/= pia alinyang’anywa nyumba yenye thamani ya shilingi 37,000,000/= iliyopo kiwanja Namba 115 Kitalu C eneo la Ndachi East Jijini Dodoma.
"Leo Februari 18, 2021 tunamrejeshea nyumba yake na shilingi 1,830,000/= kwakuwa awali alisharejeshewa shilingi 2,000,000/=. Baadhi ya malipo yatakayofanyika leo kwa wastaafu ni: shilingi 27,488,000/=; shilingi 23,800,000/=; shilingi 23,400,000/=; shilingi 16,800,000,"amesema Mkuu huyo.
Pia amebainisha kuwa,kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaendelea kukokotoa kiasi cha kodi ambacho kampuni hiyo ya ukopeshaji inadaiwa.
"Aidha,tunaendelea kufuatilia shilingi milioni mia moja themanini na nne laki tano themanini na sita (184,586,000/=) za wakopeshwaji 22 ambazo pia zinapaswa kurejeshwa na Bw.Mapesa.
"Pili, tunamrejeshea Bw. Dismas Kweka, Mfanyabiashara na Mkazi wa Nkhuhungu jijini Dodoma, shilingi milioni tano (5,000,000/=) ambapo ufuatiliaji wetu umewezesha kuziokoa kutoka kwa Bw. Richard Mwambeje. Desemba 2021, tulimrejeshea Bw. Kweka ambaye aliuziwa kiwanja Na. 18 Kitalu B kilichopo Mbwanga Jijini Dodoma kinyume na utaratibu shilingi 9,700,000/= na leo anapatiwa kiasi kilichosalia. Kiwanja hicho kilitolewa na mwananchi mmoja kama sadaka kwa Jumuiya ya Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) lakini Bw. Mwambeje ambaye alikuwa Katibu wa UWATA alikiuza kwa kutumia mkataba wa kughushi.
"Tatu, TAKUKURU (M) Dodoma imefanikiwa kurejesha deni la shilingi 51,678,733/= kwa Chama cha Akiba na Kukopa cha Ufundi SACCOS baada ya kuwabana wanachama ambao ni wadaiwa sugu wa muda mrefu. Mwisho, tunawasihi wakopeshaji wa fedha mkoani Dodoma kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi na kuacha tabia ya kuwatoza wananchi riba umiza.
"Aidha, tunawakumbusha wananchi wa mkoa wetu kujihadhari na mikopo umiza na kamwe wasikubali kukabidhi kadi zao za benki kwa mtu yeyote,"amefafanua Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma,Sosthenes Kibwengo.
Tags
Habari