Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita(2015-2019), kwa wastani wa asilimia 6.8 na kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi barani Afrika baada ya nchi Ethiopia na Rwanda, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mtwara).
Waandishi wa habari wakimfuatilia kwa makini Mchumi wa BoT, Aristides Mrema (hayupo pichani) wakati akiwasilisha mada katika mafunzo hayo. (Picha na Mwandishi Diramakini).
Mchumi wa BoT, Aristides Mrema ameyasema hayo leo Februari 22, 2021 wakati wa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayofanyika mkoani Mtwara na kuandaliwa na Benki ya Kuu ya Tanzania (BoT).
Amesema, sekta zilizochangia zaidi katika ukuaji wa uchumi huo ni ujenzi asilimia 25,kilimo (20) viwanda (9.6),usafirishaji na uhifadhi mizigo (8.3) na biashara 7.3.
Mrema amesema, katika kipindi cha robo tatu za mwaka jana, uchumi umeendelea kukua japo ya uwepo wa changamoto ya Covid-19 bado haujatetereka.
"Takwimu za Januari hadi Septemba mwaka jana zinaonesha pato la taifa kukua kwa asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 7.9 mwaka 2019 na asilimia 6.9 mwaka 2018,"amesema.
Amesema, pato la taifa ukuaji wake umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchukuzi na uchimbaji wa madini.
Mrema amesema,ukuaji huo ulitokana na uwekezaji ambao serikali imeendelea kufanya katika miundombinu na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi na sera madhubuti ya bajeti ya serikali.
"Kasi ya ukuaji wa uchumi inatokana na uamuzi wa serikali kutokufunga shughuli za kiuchumi kufuatia mlipuko wa Covid-19.
"Matarajio yetu ni ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuwa asilimia 5.5 kwa mwaka 2020 na 6.0 au zaidi kwa mwaka huu,"amesema.
Amesema, mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya lengo kwa asilimia tano kwa mwaka ambapo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ulikuwa kwa wastani wa asilimia 4.2.