Viongozi wakuu Kanisa la EAGT mikononi mwa makachero wa TAKUKURU

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) makao makuu inawachunguza viongozi wakuu wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania (EAGT) akiwemo Askofu Mkuu wa kanisa hilo kwa tuhuma za rushwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Askofu Abel Mwakipesile.

Hayo yamebainishwa leo Februari 16, 2021 na Afisa Uhusiano wa TAKUKURU, Doreen Kapwani kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

"Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenenerali John Mbungo, napenda kuujulisha umma kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU makao makuu, inafanyia uchunguzi malalamiko dhidi ya viongozi wakuu wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania (EAGT) nchini.

"Bila shaka baadhi yenu mlisikia na kuona malalamiko ya baadhi ya wachungaji wa kanisa la EAGT ambao waliyatoa siyo tu kwenye vyombo vya habari, lakini pia katika ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

"Wachungaji hao, ambao kwa ujumla wao ni zaidi ya 540, kwa pamoja wanalalamikia vitendo vya rushwa,ufisadi pamoja na wizi ndani ya kanisa yakiwemo mambo yafuatayo;

"Mosi uingizwaji wa vyombo vya moto yakiwemo magari zaidi ya 50 na pikipiki kwa jina la Kanisa la EAGT, vyombo ambavyo inadaiwa viliingizwa nchini kwa kupitia jina la kanisa na kupata msamaha wa kodi lakini vyombo hivyo vya moto - kanisa halivitambui na wala halijawahi kuvipokea.

"Pili lalamiko jingine ni ubadhirifu wa fedha na mali ya kanisa unaodaiwa kufanywa na viongozi wa kanisa hilo kuhusiana na mkataba ulioingiwa kati ya kanisa la EAGT na wapangaji wa Duka la Imalaseko Suparmarket Investment kwani inadaiwa mapato yanayotokana na majengo hayo hayajawekwa wazi hivyo kuashiria kuwepo kwa ubadhirifu.

"Tatu ubadhirifu wa fedha za kanisa kwenye ununuzi wa shule iitwayo Oasis Education and Community Development iliyopo Kahama.

"Nne ni kuwepo kwa TIN tofauti zaidi ya tano zilizosajiliwa kwa jina la Kanisa la EAGT na TIN hizo kutumika kuingiza magari kwa jina la kanisa na kusamehewa kulipa ushuru wa forodha wakati magari hayo hayajanunuliwa na kanisa.

"Tano taarifa za mapato na matumizi ya kanisa kutokuwekwa wazi wala Kanisa halina Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani. Sita uingiaji wa mikataba mibovu na isiyo wazi inayoikosesha Serikali mapato yake halali,"amefafanua Kapwani kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

Ameongeza kuwa, kupitia taarifa hii tunapenda umma ufahamu kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) makao makuu ilishaanza kufanyia uchunguzi malalamiko haya ambayo baadhi ya tuhuma zinaangukia

chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 na kwamba mpaka sasa yafuatayo yameshafanyika:

"Tumeshafanya mahojiano na baadhi ya walalamikaji, tumekusanya baadhi ya vielelezo na tunaendela kuwaita na kuwahoji walalamikiwa na leo hii Februari 16, 2021 tumemhoji Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Abel Mwakipesile.

"Lengo la uchunguzi wetu huu pamoja na mambo mengine ni kutaka kufahamu ukweli wa malalamiko haya ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa," ameongeza Kapwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news