Viongozi waomboleza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

Viongozi mbalimbali wameendelea kutuma salamu za rambirambi kutoka ndani na nje ya Tanzania kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia alikuwa mwenyekiti huyo wa chama cha ACT-Wazalendo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli naye akitoa salamu za pole na kutangaza siku tatu za maombolezo.

Aidha, kabla ya kuhamia Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Maalim Seif ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 77 alizaliwa Oktoba 22, 1943 katika Kijiji cha Mtambwe, nje kidogo ya mji wa Wete, Pemba.

Historia inaonyesha Maalim Seif alivuka bahari ya mkondo wa Pemba kwenda Zanzibar kuendelea na masomo ya sekondari kutoka 1958 hadi 1963.

Alipitia shule za Uondwe na Shule ya Wavulana ya Wete kisiwani Pemba kati ya 1950 hadi 1957. Sekondari alisomea katika shule ya King George VI Memorial mjini Zanzibar, na aliendelea na masomo ya cheti cha cha sekondari katika shule hiyo.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia 1972 -1975 na kuhitimu na shahada ya sayansi ya siasa, utawala wa umma na mahusiano ya kimataifa.
 
Maalim Seif amekuwa katika siasa za Zanzibar tangu miaka ya 1970, akiwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa Elimu kati ya 1977-1980, na mjumbe mwazilishi wa baraza la wawakilishi visiwani humo.

Maalim Seif anatajwa kwenye siasa za Tanzania kwa kuwa alianza kuitikisa nchi hata kabla ya mfumo wa vyama vingi. Harakati zake zilianza mapema sana na kuishia kukutana na misukosuko kadhaa.

Katika medani ya siasa Maalim Seif alichaguliwa mjumbe wa Halamshauri Kuu ya Taifa ya CCM ambayo aliitumikia kwa miaka 11. 
 
Katika mwaka 1984 kufuatia kile kilichojulikana kama kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa visiwani Zanzibar kulikoshuhudia kulazimishwa kustaafu kwa aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, Maalim Seif alichaguliwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Lakini kauli zake za mara kwa mara za kuonyesha hafurahishwi na mwenendo mzima wa Muungano na kueleza Zanzibar haitendewi haki kwa baadhi ya mambo ndani ya Mungano kuliepelea kutimuliwa katika chama na pia kupoteza wadhifa wa Waziri Kiongozi kufuatia hatua hiyo ya chama.

Tokea wakati huo alipitia mambo mengi na kuonekana tishio la kisiasa.Mwaka 1989 alifunguliwa mashitaka baada ya kupatikana na nyaraka za siri za Serikali. Alikaa miaka miwili gerezani mpaka alipoachiwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Tanzania ilipofungua milango yake na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, Maalim Seif na baadhi ya wenzake aliofukuzwa nao Halmashauri Kuu ya CCM walikuwa miongoni mwa walioanzisha Chama cha Wananchi (CUF) na kuwa Makamu Mwenyekiti wake wa kwanza na baadaye Katibu Mkuu huku akigombea nafasi za uraisi tangu 1995 hadi alipotimkia ACT Wazalendo mwaka 2020, baada ya kutofautiana kimsimamo na wenzake ndani ya CUF.

Aidha, kutokana na historia ndefu na umaarufu wa Maalim Seif, salaam za rambirambi zimeendelea kutolewa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, Kimataifa na sekta binafsi.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ametuma salamu za pole kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wanachama wa ACT- Wazalendo pamoja na familia ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia leo Jumatano Februari 17, 2021.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, kiongozi mkuu huyo wa nchi ameandika, “nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote. Mungu amweke mahali pema peponi amina.”

Akihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi, amesema Maalim Seif alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.

''Majira ya saa tano na dakika 26 asubuhi Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alifariki dunia, Maalim amefariki wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili ambapo alikuwa amelazwa tangu tarehe 9 mwezi Februari mwaka huu,''amesema Rais Dkt. Hussein Mwinyi.

Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) amemtumia salamu za Rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharrif Hamad kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam leo tarehe 17 Februari, 2021.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Maalim Seif Sharrif Hamad, na kwa niaba ya Bunge natoa pole kwa familia ya marehemu, Rais wa Zanzibar, Chama cha ACT Wazalendo, Wazanzibari na Watanzania wote,” amesema Mheshimiwa Spika.

“Taifa limempoteza Kiongozi mahiri ambaye alitumia muda wake mwingi katika kuwatumikia wananchi na kwa hakika mchango wake katika kuleta maendeleo, kudumisha amani na umoja wa kitaifa Visiwani Zanzibar utakumbukwa daima,” amesema Mheshimiwa Spika.

Mheshimiwa Spika ameomba Mwenyezi Mungu awape subira, nguvu na faraja familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.
 
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, “pumzika kwa amani mzee wetu Maalim Seif, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa familia, Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na Watanzania wenzangu wote. Pumzika kwa Amani.”

Naye Mwanasheria Fatma Karume amesema, “inna lilahi wa inna ilayhi rajiun Nimehuzunika sana kusikia Maalim amefariki. He was a good man and a good friend.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa ameshtushwa na taarifa za kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, kilichotokea na kutoa pole kwa familia yake.

Mbowe ameyaandika hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, masaa kadhaa tu tangu kifo cha Maalim Seif, kitangazwe na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi.

"Nikiwa hapa Dubai, UAE, nimeshtushwa na taarifa za kutwaliwa kwa Mhe. Sharif Hamad, jabali la mageuzi Tanzania, Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, natoa pole nyingi kwa familia, chama chake, Wazanzibari na Watanzania wote, kwake tumetoka na kwake tutarejea. Amin", ameandika Mbowe.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameandika kuwa, "Mh Maalim Seif, alikuja kunisalimia nilipokuwa mahabusu, alinitia moyo, aliniambia mawazo imara na fikra thabiti juu ya ukombozi yana patikana jela, alinieleza kwa kifupi safari yake ndani ya magereza enzi zake, ninawapa pole familia na chama chake,tuchuke tahadhari Corona inaua".

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazelendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kitaendeleza maono na fikra za aliyekuwa mwenyekiti wake, Maalim Seif Sharif Hamad aliyetaka kuiona Tanzania inakuwa na demokrasia na Wazanzibari kuishi kwa maridhiano.

Ametoa kauli hiyo Februari 17, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Maalim Seif kilichotokea katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

"Leo nilikuwa hospitali hadi saa mbili na nusu asubuhi nilionana na jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia kwa hakika alikuwa anaonyesha matumaini," amesema Zitto.

Zitto amesema ilipofika saa 5 asubuhi alipokea simu kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyemueleza kuwa Maalim Seif amefariki.

“Najua taarifa hii itakuwa imeleta mshituko mkubwa kwa wanachama na watanzania kwa ujumla kwa kuondokewa na mwamba wa demokrasia nchini na katika chama chetu niwaambe wanachama na watanzania kwa ujumla kuwa wapole katika kipindi hiki kigumu," amesema.

Mwanaharakati Maria Sarungi ameandika, “kwa msiba huu mzito! Poleni Wazanzibari na pole zetu Watanzania na Tanzania kama Taifa! This is absolutely devastating news! Tumeumia sana! Inna Lillahi wa inna ilayhi rajun Maalim Seif.”

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha Maalim Seif na kwamba ni pigo kwa Taifa kwa kupoteza kiongozi shupavu.

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania ameandika kuwa, “Ninaungana na Watanzania wote - hususan Wazanzibari - kuomboleza msiba mkubwa wa kuondokewa Maalim Seif. Katika maisha yake akiwa mwanasiasa kwa zaidi ya miaka 40,


"Maalim Seif amekuwa kielelezo cha kiongozi mtumishi anayewaweka watu mbele kabla ya madaraka. Hatutaweza kuziba pengo lake, lakini tunaweza na ni lazima tuuenzi mchango wake adhimu.” – Dk. Donald Wright, Balozi wa Marekani nchini Tanzania.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa rambirambi kwa Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein kufuatia kifo cha Makamu wake wa Kwanza wa Rais Mhe. Seif Sharif Hamad.

Ikulu ya Kenya imeandika katika ukurasa wa twitter alikuwa kiongozi maarufu, mwenye busara na maendeleo na mchango wake kwa watu wake na ukanda wa Afrika Mashariki utakumbukwa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ametoa salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika ukurasa wake wa Twitter Lissu amesema Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye ushawishi, na mtetezi wa Wazanzibari asiye na woga.

Hata hivyo, mwili wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad utazikwa kesho Alhamisi Februari 18, 2021 mjini Pemba, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaeleza kuwa mwili wa mwenyekiti huyo wa chama cha ACT-Wazalendo aliyefariki dunia leo saa 5 asubuhi katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) utaondoka na ndege kesho asubuhi kwenda mjini Unguja ambako itafanyika sala katika viwanja wa Mnazi Mmoja.

Inaeleza kuwa saa 6 mchana utasafirishwa kwenda Pemba na sala itafanyika katika viwanja vya Gombani na kisha safari ya kueleka Mtambwe kwa mazishi yatakayofanyika saa 10 jioni itaanza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news