Mkutano wa Pili wa Baraza la Kumi la Wawakilishi umeanza tarehe 10/02/2021 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katika mkutano huo Baraza la Wawakilishi limewapitisha Wajumbe watano kuwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kutoka Baraza la Wawakilishi kwa kupata kura 72 sawa na asilimia 100 za kura zilizopigwa katika uchaguzi uliofanyika katika kikao hicho.
Uchaguzi huo wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaoingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano unafanyika kwa mujibu wa kanuni ya 137 ya kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2020.
Wajumbe wenyewe ni Mhe Ameir Abdallah Ameir Jimbo la Mwanakwerekwe, Mhe Bakari Hamad Bakar Jimbo la Wawi, Mhe Bahati Khamis Kombo Jimbo la Chambani , Mhe Mwantatu Mbarak Khamis Nafasi za Wanawake na Mhe Suleiman Haroub Suleiman Jimbo la Kiembe Samaki.
Aidha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamewapigia kura Mhe Mwanaasha Khamis Juma Jimbo la Dimani na Mhe Shaaban Ali Othman Jimbo la Mpendae kuwa Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi.
Katika hatua nyengine Wajumbe hao wamempitisha Dkt Sada Salum Mkuya kuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Wawakilishi Wanawake wa Baraza la Wawakilishi UWAWAZA, Mhe Mwantatu Mbarak Khamis Kuwa Makamo Mwenyekiti UWAWAZA, Mhe Anna Athanas Paul kuwa katibu UWAWAZA, Mhe Panya Ali Abdallah kuwa mtunza hazina UWAWAZA na Mhe Bahati Khamis Mussa, Mhe Mwanajuma Kassim Makame, Mhe Rukia Omar Ramadhan na Mhe Salha Mohammed Mwinjuma kuwa Wajumbe wa kamati tendaji UWAWAZA.
Pia shughuli nyingine iliyofanyika ni kiapo cha Uaminifu cha waheshimiwa Wajumbe watano kutoka chama cha ACT Wazalendo ambao ni Mhe Habib Ali Mohammed Jimbo la Mtambwe, Mhe Hassan Hamad Omar Jimbo la Kojani, Mhe Kombo Mwinyi Shehe Jimbo la Wingwi, Mhe Nassor Ahmed Mazrui uteuzi wa Rais na Mhe Omar Said Shaaban Uteuzi wa Rais.