Waziri wa Madini, Doto Biteko amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila kuagiza Mkaguzi wa Migodi nchini pamoja wataalam wa Mazingira Februari 27, mwaka huu kufika katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) ili kuchunguza tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu kupitia kwa Katibu wake Mariam Mkaka kwamba kuna vumbi lenye madhara kiafya kwa wananchi, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza wakati akifungua warsha kwa wadau wa sekta ya madini iliyoendeshwa na taasisi ya uhamasishaji uwazi na Uwajibikaji katika raslimali za madini,mafuta na gesi asilia (TEITI) katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Waziri Doto Biteko amesema kuwa, tuhuma hizo ni nzito hivyo timu ya wataalam ichunguze na impatie ripoti ili aweze kupata ukweli wa tuhuma hizo na ikibainika ni kweli aweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Amesema hawezi kwenda kutembelea eneo husika kabla ya wataalam wake kufanya uchunguzi wa kitaalum na kumpa ripoti sahihi ambayo itamuwezesha kufanya maamuzi sahihi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wadau wa sekta uziduaji katika warsha iliyoratibiwa na TEITI katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Waziri Biteko ametoa maagizo hayo wakati akifungua warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Raslimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) kwa wadau mbalimbali wa raslimali hizo.
Awali Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mariam Mkaka akitoa salamu za Mbunge wa Geita Mjini amesema kuwa, ameagizwa na Mbunge huyo kuwasilisha malalamiko hayo kwa Waziri wa Madini kuhusu wananchi wanaozunguka mgodi huo kukumbana na madhira mbalimbali.
Mariam Mkaka ametaja matatizo wananchi wanayokumbana nayo ni pamoja na kupata vumbi linalotoka katika mgodi huo na kuwaletea madhara kiafya na wakati mwingine kusababisha magonjwa na vifo.
Madhara mengine amesema ni kukamatwa wasichana na wanawake na kuwapeleka maeneo yasiyo rasmi kwenye eneo la mgodi yaani vichakani na Askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU ) na kuwachapa viboko na kuwatisha.
Mkaka amesema, wananchi zaidi ya 80 wamefika katika ofisi ya mbunge huyo ili kulalamikia manyanyaso hayo ambao ni wakazi wa eneo machimbo yasiyo rasmi ya Mzingamo katika leseni ya GGML.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza katika warsha iliyoendeshwa na TEITI kwa wadau wa sekta ya uziduaji katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere mkoani Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema serikali katika mkoa huo haitaruhusu mwananchi yeyote kunyanyaswa au kunyimwa haki yake na itaendelea kushughulikia matatizo yote.
Amesema ofisi yake iko wazi muda wote kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua huku akitaka viongozi wengine Kama wakuu wa wilaya ,viongozi wa kata , vijiji pamoja madiwani kutatua matatizo ya wananchi kwa nafasi zao.
Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Ludovick Utoh amesema kuwa ripoti za taasisi hiyo zinasaidia makampuni mengi kuwajibika kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali za serikali.
Katika ripoti ya TEITI ya mwaka 2017/2018 serikali ilikusanya sh. Bilioni 728 fedha za Kitanzania kutoka kwenye makampuni ya madini,mafuta na gesi asilia.
Katika ripoti hiyo inaonyesha mlipa kodi kinara mkuu ni GGML ambayo ililipa jumla ya sh.Bilioni 213.8 ikifuatiwa na North Mara Gold Mining Limited Bilioni 179.7 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) sh.Bilioni 78.2.
TEITI imeendesha warsha ya siku moja kwa wadau wa sekta ya uziduaji ambayo ilishirikisha madiwani wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita,wenyeviti wa vijiji pamoja na wachimbaji wadogo.