WAZIRI MKUU: TUMUENZI MHESHIMIWA NDITIYE KWA VITENDO

Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa amesema sifa na maneno mazuri ambayo yamesemwa kuhusu aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye yatakuwa na maana tu endapo matendo mema aliyoyatenda wakati wa uhai wake yataenziwa na kuendelezwa.
Akizungumza katika ibada ya kumwombea marehamu, katika Kanisa la Anglikana la Kibondo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini mchango alioutoa wakati wa uhai wake na ndiyo maana Rais Magufuli amemtuma amwakilishe katika msiba huu.

Amewataka wana-Muhambwe, wabunge na Watanzania kwa ujumla wamwombee marehemu ili Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. “Nawasihi tuwe karibu na familia ya marehemu kama tulivyokuwa wakati wa uhai wake, hatua ambayo naamini itawapa faraja wanafamilia.”

Naye, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema Spika Ndugai amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Nditiye kwani alikuwa na mchango mkubwa katika Bunge kutokana na michango yake mizuri ya uzalendo, mapenzi makubwa kwa wapiga kura wake na Taifa pia.

“Kwa mara ya mwisho, Mhandisi Nditiye alichangia katika Bunge lililopita tarehe 9 Februari, 2021 wakati nikiwa kwenye kiti na hakuna aliyedhani kuwa leo tusingekuwa naye. Niwasihi ndugu zangu tuwe tayari wakati wote kwani hakuna ajuaye siku yake ya mwisho,” alisema.

Mwakilishi wa Wabunge wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema anaishukuru Serikali hasa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa misaada waliyoitoa wakati wa kumuuguza, wakati wa msiba na katika mazishi.

Aliishukuru pia Ofisi ya Bunge ikiongozwa na Spika Job Ndugai, Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Bw. Stephen Kagaigai na wabunge wote kwa ushiriki wao wa hali na mali katika ugonjwa, msiba na mazishi ya Mhandisi Nditiye.

Akitoa salamu zake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Thobias Andengenye alisema Mhandisi Nditiye alitumia muda wake mwingi kukutana na viongozi wa mkoa huo ili kujadili na kushauriana masuala mbalimbali yaliyohusu maendeleo ya mkoa huo.

Viongozi wengine walioshiriki mazishi hayo ni Mhandisi Isaack Kamwelwe, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante ole Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel na baadhi ya Wabunge.

Mhandisi Nditiye alizaliwa 17, Oktoba 1969 wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma. Alisoma shule ya msingi Kabwigwa kuanzia mwaka 1975 hadi 1981 na baadaye alijiunga na Chuo cha Ufundi Dar es Salaam ambako alisoma kuanzia mwaka 1984 hadi 1986 na kutunukiwa cheti cha uhandisi.

Katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mhandisi Nditiye alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa Bungeni Februari 12, 2021 na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alisema kuwa kifo hicho kimetokana na ajali aliyoipata Jumatano, Februari 10, 2021 katika eneo la Nanenane, jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news